Wednesday, November 27, 2013

WILAYA YA KALIUA KUHAMIA MKOA MPYA WA KATAVI -HOYA YANGU





Ramani inayoonyesha ulipo Mto Igombe ambao  ni tuzo ya “Kilimo Kwanza” mkoani Tabora

  1.0  Utangulizi
Katika kikao cha Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kilichofanyika tarehe 8 Novemba 2013,  Mkuu wa Wilaya  alimkabidhi Mwenye  Kiti barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, ikiwataarifu wana Kaliua, kupitia Halmashauri yao, kuwa Serikali imeridhia maombi ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapiduzi, CCM  Kaliua, yaliyo wakilishwa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu  na Mwenye Kiti wa CCM,  kuomba wilaya yake ihamishiwe Mkoa mpya wa Katavi. Madiwani wengi walishangazwa na taarifa iliyokuwa ikielezwa na barua hiyo,  kwa vile hawakuwa na taarifa ya maamuzi ya kikao chochote cha Halmashauri yao mpya ya Kaliua au hata ya halmashauri ya Wilaya ya Urambo walikokuwa,  kupitisha uamuzi wa Wilaya ya Kaliua kuhamishiwa Katavi. Hata hivyo Mwenye Kiti,  John Kadutu, akiungwa mkono na madiwani, aliyapokea maagizo ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya kutaka kulifikisha suali hili kwenye kamati za maendeleo za kata, ili kupitia kamati hizo, wananchi wapate nafasi ya kulijadili suala zima la kuhamia Katavi na kulikubali au kulikataa. Maoni na mapendekezo yoyote yatakayopatikana kutokana na vikao hivyo vya kata ndiyo yatakayokuwa msingi sahihi wa mjadala wa Baraza la Madiwani, yaani Halmashauri ya Kaliua na kamati zake.

2.0  Hoja ya Kuhamia Katavi
Kumekuwapo na maelezo mbali mbali kuhusu suali la Wilaya ya Kaliua kuhamishiwa Mkoa wa Katavi.  Mheshimiwa Profesa Juma Kapuya, Mbunge, ndiye kiongozi pekee ambaye amekuwa akilielezea jambo hili kwenye majukwaa na kutangaza kuwa ni uamuzi wa Serikali unaopaswa kutekelezwa bila kuchelewa. Inasemekana anaamini kufanya hivyo “kutaiwezesha wilaya ya Kaliua kuharakisha maendeleo yake” .  Anaamini Katavi kuna maendeleo kuliko Tabora!

Wilaya za Mkoa wa Tabora

3.0  Uchambuzi wa Hoja ya Mheshimiwa Kapuya
Haikuweza kuelewaka mara moja nini maana ya hoja hii kwa vile kimsingi inajulikana maendeleo yanahusu maisha mazuri ya jamii kuwa na chakula cha kutosha na lishe bora, afya bora na usalama wa maisha yao na mali zao, miundo mbinu imara na mawasiliano ya kisasa kupitia barabara, reli na kadhalika. Uhuru wa vyombo vya  habari; utawala bora na uhuru wa wananchi kushiriki katika maamuzi yanayohusu maisha yao, na kadhalika. Ingawa Serikali ina nafasi kubwa katika kuwawekea wananchi wake mazingira mwafaka ya kuwezesha  mambo haya yote yashamiri, bado ni jukumu la wananchi wenyewe, mmoja mmoja na kama jamii, kuamua kujiletea maendeleo mahali walipo. Watu wanapofikiria na kupanga mambo yao, Serikali kupitia wawakilishi wake, (madiwani, wabunge, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na mashirika ya dini) huona umuhimu wa kuwaletea misaada mbali mbali pamoja na fedha, maji ya bomba, hospitali kubwa na madaktari bingwa, shule na vyuo, viwanda, na kadhalika.  Maendeleo hayafuatwi nchi nyingine au mkoa mwingine.

4.0  Hoja za Kubaki Mkoa wa Tabora.
4.1 Historia
Hoja ya kufikiriwa kwanza ni ile ya kihistoria. Wilaya ya Kaliua,  hususani tarafa ya Ulyankulu , ndiyo chimbuko la Wanyamwezi. M ji wa Tabora  una historia ndefu – biashara ya utumwa na utawala wa waarabu, utawala wa Wajeremani na Waingereza, uanzilishi wa Chama ca TANU, na kadhalika. Yote haya  yameifanya Serikali ya awamu ya nne iheshimu nafasi ya Mkoa waTabora katika utamaduni wa nchi mpaka ikaweka makumbusho ya Mtemi Miranbo kule Uyankulu. Hivyo kuipekleka Ulyankulu Katavi ni kuupunguzia hadhi Mkoa wa Tabora bila sababu ya msingi.

4.2  Barabara ya Kigoma
Kwa vile sasa kuna barabara kuu itokayo Tabora kwenda Kigoma, mawasiliano kati ya Wilaya ya Kaliua na Mkao makuu ya mkoa, yaani mji wa Tabora, yatakuwa  mazuri zaidi.  Kwa upande wa tarafa ya Ulyankulu, sasa hivi si rahisi kusafiri kutoka baadhi ya kata za Ulyankulu kwenda Kaliua – barabara si nzuri. Inawapasa watendaji kutoka Mwongozo[1], kwa nfano, kupitia Tabora mjini  (Tazama kielelezo cha raani ukurasa wa 5) ili kupata usafiri wa haraka wa kuwafikisha wilayani Kaliua. Hivyo umbali ni kigezo kimojawapo tunachopaswa kukizingatia tunapotaka kuwahudumia wananchi wa sehemu yeyote kwa karibu zaidi.

4.3  Kilimo Endelevu Wilayani Kaliua
Wilaya ya Kaliua ina ardhi nzuri, mito na mabonde [2] yanayofaa kwa kilimo cha umwagilizaji. Uendelezaji wa kilimo hicho katika  mabonde haya utahitaji juhudi za mkoa wenye uzoefu, kama Mkoa wa Tabora. Wilaya ya Kaliua ikihamia Katavi ittachelewa kupanga maendeleo yake; sio kuyaharakuisha,  kwa vile mkoa mpya bado unandaa mikakati yake ya maendeleo kabla haujaanza kuitekeleza.
Rmani inayoonyesha jinsi wilaya za Kaliua na Urambo Mashariki zinavyowiana  na wilaya zingine za Mkoa wa Tabora kijografia

 
4.4 Mradi wa Mto Igombe
Tarafa ya Ulyankulu ina mipango ya kushirikiana na wawekezaji siku zijazo kuendeleza matumizi ya mto Igombe. Mto huu unapita katikati ya Ulyankulu na sehemu kubwa ya tarafa Uyowa, ukianzia sehemu za Uyui na Itaga karibu na mji wa Tabora. Serikali kupitia Wizara ya Maji, walipotengeneza bwawa la maji kwenye chanzo cha mto huu (Tabora Igombe Dam), walibadilisha mtiririko wa maji ya mto huu. Maji sasa mengi yanabaki kwenye bwawa. Maji kiasi tu ndio yanaenda ndani ya mto.  
Walipokuwa wakijenga bwawa la kupeleka maji Tabora Mjini, walipaswa pia kujenga bwawa la kina kidogo (gravity dam Tazama mchoro wa kushoto hapo juu) kilometa 100 hivi magharibi mwa Mto Igombe, kama reservoir (hifadhi ya maji ya mto). Kwa kufanya hivyo matumizi ya mto huu kwa watu wa Ulyankulu na Uyowa yangeendelea kuwapo. Hii ingewezesha maji kuendelea kuwapo muda wote.
Matokeo ya makosa yaliyofanyika Tabora yamekuwa mabaya kwa Ulyankulu na Uyowa: Hakuna tena samaki wanaovuliwa kwenye mto huu, kwa vile maji sasa yanabaki Tabora Dam! Hata wale viboko na wanyama wengine wanaopatikana kwenye maji sasa wametoweka.
Utekelezaji wa mradi huu unaweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa zaidi Wilaya ya Kaliua akishirikiana kwa karibu zaidi na mdau mkubwa wa maji ya Mto Igombe, ambaye  ni Mji wa Tabora.

5.0  Sheria na Utaratibu wa Kuihamisha Wilaya Kaliua
Umekuwako uvumi na minong’ono kuwa wazo la kuhamia Katavi limeletwa na mbunge Profesa Juma Kapuya, ambaye amekuwa akilieleza kila apatapo wasaa wakufanya hivyo. Wananchi wamekuwa wakijiuliza  kwa nini Mheshimiwa Profesa Juma Kapuya amelivalia njuga jambo hili? Je, ana masilahi gani nalo?
Si vizuri kuamini maneno yanayosemwa semwa na watu jimboni kwa mbunge huyu; lakini pia si vizuri pia kuyafumbia macho, kwa vile wananchi ndio wapiga kura na wachaguzi wa mwisho. Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, ibara ya 8, kifungu kidogo cha (1) (b) hadi kile cha (c), vinasema  “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote ya Serikali;  na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.”  Kifungu (b) ”Lengo kuu la Serikal litakuwa ni ustawi wa wananchi.  (c) Serikali itawajibika kwa wananchi wake na (d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.” Hivyo tangu mwanzo Mbunge Kapuya angekuwa amepata ridhaa  ya wananchi kwanza baada ya kuwashirikisha, kuwaelimisha na kuwashawishi kwa semina na vikao halali katika ngazi ya kata, kama inavyoagiza Ofisi ya Waziri Mkuu  sasa.
Katika suala hili zima la wilaya ya Kaliua kuhamia mkoa wa Katavi,  bado kuna masuali mengi yanayohitaji maelezo:
·        Ombi la kamati ya siasa ya Chama Tawala CCM, lilipelekwa Serikalini na Mwenye  Kiti wa CCM kwa misingi gani?
·         Kikao cha kamati hiyo hakikuwashirikisha wajumbe wa Halmashauri ya Kaliua.  Kikao hicho kilikaa lini na kwa kanuni au sheria ipi?
·        Kikao hicho kilipata mamlaka ya kuwasilisha ombi  Serikalini kwa mujibu wa kanuni au sheria gani?
·        Makadirio ya asilimia 80 ya wananchi wa Kaliua wanaopendelea wilaya yao ihamie  Katavi yalipatikana vipi?

6.0  Matarajio ya Wilaya ya Kaliua Ikibaki Tabora
Wilaya ya Kaliua, hususani tarafa ya Ulyankulu, imejiwekea malengo mbali mbali ya kimaendeleo, ambayo utekelezaji wake utategemea ushirikiano uliojengwa mkoani Tabora.  Muhimu katika miradi ya maendeleo ni pamoja na hii:-
·        Kuendeleza kilimo, hususani kilimo cha umwagiliaji,  kwa kitumia mto Igombe, ili kuongeza uzalishaji wa chakula. Chakula cha ziada kitauzwa  nje ya wilaya yetu ya Kaliua..
·        Kujenga barabara za taarafa zote za Wilaya ya Kaliua,  hususani barabara zinazoziunganisha kata na tarafa za Kaliua  na makao makuu ya mkoa,Tabora, na wilaya jirani za Kahama, Urambo, Uyui.
·        Kuboresha huduma ya afya kwa wakaazi wa Wilaya ya Kaliua, hasa afya ya akina mama wazazi na watoto, kwa mujibu wa yale Malengo manane ya Milenia.  Mkazo utakuwa kupunguza au kutokomeza magonjwa ya kuambukiza, hususani malaria, ukimwi, na kifua kikuu.
·        Kuboresha miundo mbinu ya mawasiliano, yaani mawasiliano ya simu, radio, tv, na magazeti.
·        Kuendeleza miradi ya kuchimba visima ili kuwapatia wananchi  maji safi na ya uhakika. Wilayani Kaliua hakuna  mipango-majiendelevu inayo weza kuleta maji muda wote hata kiangazi
·        Kuunda vikundi vya  ushiriki ikiwa ni pamoja na Saccos, Vicoba na vyama vya ushirika wa mazao ya biashara, hususani tumbaku na pamba.
Mipango ya matarajio haya yanaendana na mipango ya Mkoa wa Tabora; hivyo utekelezaji wake utazorota Wilaya ya Kaliua ikihamishiwa Tabora sasa.

7.0  Angalizo
Yote haya yameelezwa vizuri kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Utekelezaji wake utachelewa Kaliua ikihamia Katavi. Wachunguzi wa siasa wanatabiri kuwa  Chama tawala CCM kitapoteza imani ya wananchi wa Kaliua na wanachama wake kikiwalazimisha kuhamia Katavi kwa shinikizo la mbunge wa sasa Mheshimiwa Profesa Juma Kapuya. Wanachama wa CCM na wananchi wa Wilaya ya Kaliua hawakubali suala hili liwagawanye: wanao taka kuhamia Katavi nawanaotaka kubaki Mkoani Tabora. CCM  kitakosa kura muhimu ya wanaKaliua.




[1] Kutoka Mwongozo mpaka Kaliua in umbali wa kilometa 148; na kutoka Mwongozo kijijini  mpaka Mpanda (Katavi) ni umbali wa kilometa 420.
[2] Kama yale mabonde ya Mto Malagarasi na Mto Igombe

"MAHUSIANO MAZURI KATIKA JAMII PASIPO KUJALI DINI WALA KABILA NDIO NYENZO PEKEE YA KUPATA MAFANIKIO"


Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Tabora  mjini  Bw.Emmanuel Adamson Mwakasaka alipokaribishwa katika  Kongamano la dini ya Kiislam lililofanyika katika viwanja vya Uyui Sekondari mjini Tabora ambapo Sheikh Shariff Mikidadi alikuwa ndio kiongozi wa Kongamano hilo lililohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Tabora.

"ALIYEPIGWA KATIKA OPERESHENI TOKOMEZA HALI YA AFYA YAKE INAZIDI KUWA MBAYA"-SIKONGE

Juma Shabani Kunguwala(50)mkazi wa kijiji cha Tutuo wilaya ya Sikonge ambaye alipatwa na masahibu ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya na watu wanaodaiwa kuwa ni maaskari wanaoendesha Operesheni Tokomeza akituhumiwa kuwa alikuwa akimiliki silaha na uwindaji haramu.Majeruhi huyu kwasasa hali yake ya kiafya si nzuri na bado anaendelea kudhoofika siku hadi siku. 
Sehemu ya mkono wa majeruhi huyo.
Juma Kunguwala akiwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Sikonge akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya.


KADA AKINUSURU CCM KWA KUWACHIMBIA KISIMA WANANCHI,WALICHOSHWA NA AHADI HEWA

 
Baadhi ya  viongozi  wa CCM wilaya ya Tabora mjini wakiangalia kisima cha maji ya kunywa kinachotumiwa na wakazi wa kijiji cha Kabila manispaa ya Tabora ambapo licha ya kupiga kelele kwa Serikali lakini tatizo la maji bado limeendelea kuwa sugu.
Mama akichota maji ya kunywa katika moja ya kisima ambacho kinategemewa na idadi kubwa ya wanakijiji cha Kabila,ambapo hutumia zaidi ya saa tisa kusubiri maji hayo yanayotiririka katika kisima hicho na kusababisha muda mwingi kutumika kutafuta maji badala ya shughuli nyingine za kiuchumi.Hata hivyo pia imeelezwa kuwa baadhi ya wanawake wamejikuta ndoa zao zikiwa matatani kutokana na adha hiyo ya kutafuta maji.  
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora mjini Bw.Moshi Abrahamu NKONKOTA akikata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua kisima cha maji kilichojengwa kwa ufadhili wa Mjumbe wa kamati kuu ya CCM wilaya ya Tabora Bw.Emmanuel Adamson Mwakasaka ambaye aliguswa na tatizo hilo la maji akaamua kushirikiana na wananchi katika kijiji cha Kabila la kuchimba kisima hicho.
Hapa kinamama hawa wanaonesha kufurahia huduma hiyo ya maji ya kisima baada ya kusumbuka kwa muda mrefu,huku Serikali ikitumia zaidi ya shiringi Milioni 360 kueneza huduma ya maji ambayo hayakuweza kupatikana mpaka sasa.
Wananchi wa kijiji cha Kabila wakiwasikiliza viongozi wa CCM baada ya kuzinduliwa kwa huduma ya maji ya kisima na kuahidi kuendelea kukipa ushirikiano chama hicho ambacho walianza kukisusa kutokana na ahadi hewa zilizokuwa zikitolewa na viongozi wake. 

SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA-TABORA LIMETOA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA TABORA MJINI


Meneja wa Shirika la nyumba la Taifa NHC Bw.Ladislaus Bamanyisa akimkabidhi Meya wa manispaa  ya  Tabora Bw.Ghulam Dewij msaada wa vifaa  vya ujenzi  wa hospitali ya wilaya ya Tabora mjini ambapo alikabidhi mabati ya aluminium 144 yenye thamani ya shilingi 5,472,000/=na mifuko ya Saruji 245 yenye thamani ya shilingi 4,655,000/=.Jumla ya thamani ya msaada wote ni shilingi 10,127,000/=

"MBUNGE ALIYESHINDWA KUTEKELEZA AHADI ZAKE APIGWE CHINI 2015,TUSIMUONEE AIBU ANATUHARIBIA CHAMA"-CCM

Mwenyekiti mstaafu wa CCM mkoa wa Tabora Bw.Juma Samwel Nkumba akizungumza na baadhi ya  wananchi wa mjini Tabora kata  ya  Mtendeni  ambapo  alisisitiza kuwa makini wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015,kuchagua viongozi ambao wapo karibu na wananchi wakisaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali na si kuchagua viongozi hususani Wabunge ambao hawana muda wa kukaa karibu na wananchi waliowapigia kura na hivyo kuwataka wawapige chini  ambao waliahidi ahadi kibao wakati wa kuomba kura na mara baada ya kuchaguliwa wamekuwa hawataki kusogea karibu na wananchi,jambo ambalo limekuwa likishusha heshima ya CCM kwa wapiga kura. 
Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Tabora mjini Bw.Emmanuel Mwakasaka akizungumza katika hafla fupi ya shukrani ya  diwani wa kata ya Mtendeni Bw.Ngalu,...Katika hotuba yake Bw.Mwakasaka alitumia fursa hiyo kusisitiza juu ya umuhimu wa kukiimarisha CCM kabla na baada ya uchaguzi jambo ambalo limekuwa likipigwa vita na baadhi ya Viongozi wa CCM  ambao wanashindwa kuwa karibu na wananchi na kufanya mikutano ya mara kwa mara itakayosaidia kukijenga Chama hicho.Aidha ameongeza kusema kuwa ni vema wanaCCM wakajenga mazingira ya ushirikiano utakaowawezesha kuwatumikia wananchi waliokipatia ridhaa  chama hicho kuongoza dola badala ya kuendelea na marumbano yasiyo na tija hasa wakati huu ambao uchaguzi umekwisha kilichobaki ni kutekeleza ilani ya chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora  mjini Bw.Moshi Abraham  maarufu  Nkonkota naye alipata fursa ya kuzungumza katika hafla hiyo ambapo pamoja na mambo mengine Mwenyekiti  huyo alisema kuwa kwasasa Chama hakina nafasi ya kumuonea aibu kiongozi yeyote aliyeshindwa kutekeleza ahadi zake kwakuwa jambo hilo litaendelea kukichafua CCM mbele ya wananchi....Nkonkota aliongeza kuwa  nia ya CCM ni kutaka kutoa huduma bora kwa wananchi waliowachagua na kamwe hakita kubali kumkumbatia kiongozi anayeshindwa kutekeleza majukumu yake kama alivyoahidi na kubwa zaidi CCM itakuwa macho kuangalia mtu anayekubalika kwa wananchi na si kuwalazimisha wachague kiongozi mjanja mjanja wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015 utakapowadia.