Mtaalamu
wa mawasiliano Mradi wa uwezeshaji wa demokrasia (DEP) kutoka Shirika
la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Nicodemus Marcus akizungumza
wakati wa kufunga warsha ya siku tatu ya kutathmini mradi wa uwezeshaji
wa demokrasia na amani (DEP) kwa wanamtandao wa Redio Jamii nchini
(COMNETA) yenye lengo la kuimarisha ushiriki wa redio za jamii nchini
kuelekea uchaguzi 2015 na kura ya maoni iliyoandaliwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP)
iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria Tanzania
jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wa pili kushoto ni Mshauri na
Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu,akifuatiwa na Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu Huria Tanzania, Prof. Tolly Mbwete, Mwenyekiti wa mtandao wa
Redio Jamii nchini (COMNETA) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii
ya Wilayani Karagwe ya FADECO FM, Bw.Joseph Sekiku na Mshauri wa UNESCO,
Balozi mstaafu Mh. Christopher Liundi.
Na Mwandishi wetu
SHIRIKA
la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini limetoa wito kwa redio
za jamii kujikita zaidi katika kutoa hamasa ya ushiriki wa wananchi
katika mchakato wa uchaguzi ukiwamo kujiandikisha katika daftari la
kudumu la wapiga kura.
Akizungumza
matumaini ya Umoja huo katika tathmini ya mradi wa Uwezeshaji wa
Demokrasia (DEP) kwa Redio za Kijamii nchini Tanzania zinazounda umoja
wa COMNETA, chini ya ufadhili wa UNESCO, mtaalamu wa masuala ya
mawasiliano wa UNDP Nicodemus Marcus alisema kwamba redio hizo zina kazi
5 muhimu kuelekea uchaguzi.
Alisema
pamoja na kutekeleza makubaliano kati ya Umoja wa Mataifa na redio hizo
kuhusu elimu kuelekea uchaguzi mkuu unaozingatia maadili ya uandishi na
uwajibikaji katika mradi huo ni matumaini ya UNDP kwamba redio hizo
zitatimiza wajibu wa kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa amani na
makundi mbalimbali yanajitokeza kupitia vyama vyao vya kisiasa kuwania
uongozi.
Akifafanua
alisema kwamba hamasa ya watu kujitokeza kujiandikisha katika daftari
la wapiga kura, kushiriki katika kura ya maoni,Kujitokeza kwa wingi
katika upigaji kura, kuendeleza amani kuelekea katika uchaguzi mkuu na
kuhamaisha makundi kuwania uongozi ni mambo matano ambayo Umoja wa
Mataifa unategemea redio hizo zitafanya.
Aidha
alisisitiza haja ya redio hizo kufuata makubaliano ya kuendesha elimu
kwa uadilifu mkubwa ili wasijiingize katika matatizo yoyote yale
yatakayokwamisha kazi ya kutoa elimu kwa umma kuelekea uchaguzi mkuu na
mchakato wake.
Naye
Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu,
Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu ambaye taasisi yake
ndiyo inayosimamia redio za jamii alisema kwamba Tathmini ya mradi wa
uwezeshaji wa demokrasia (DEP) kwa radio za kijamii, umeonesha kuwapo
kwa changamoto hasa katika utekelezaji wa makubaliano.
Alisema
kati ya redio 28 zilizomo katika umoja wa Comneta ni redio kama 8
zilizofanya juu ya kiwango na kuonesha kwamba inawezekana kuhabarisha
umma.
Ufanisi
wa redio hizo umeoneshwa katika ripoti ya Umoja wa Vilabu vya waandishi
wa UTPC uliopewa kazi ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya mwaka
jana kuhusu uendeshaji wa vipindi mbalimbali vya uchaguzi katika mradi
wa DEP.
Alisema
redio zilizofanya vyema ni pamoja na Mpanda iliyopata alama 80 huku
redio nyingine za Fadeco FM , Fadhila FM, Sibuka FM, Mazingira FM,
Kwizera FM Kyela FM na Micheweni zikiwa na alama 60.
Pamoja
na changamoto hiyo Bi. Rose Haji Mwalimu alisema wamejifunza kwamba
kumekuwepo na kuboreka kwa vipindi kiasi ya kwamba watu wengi wanavutiwa
kusikiliza redio hizo na wengine wakitaka kufanyanao kazi.
Aidha
wametambua kwamba redio za jamii ndio mhimili mkubwa wa kupata taarifa
mbalimbali za uchaguzi zilizofanyiwa kazi hasa uwapo wa watoa habari wa
kuaminika katika jamii.
Pia
alisema redio hizo zimeanza kuona umuhimu wa kufuata maadili,
ushirikishaji kijinsia, utoaji wa nafasi kwa makundi mbalimbali wakiwemo
walemavu na vijana katika kazi.
Hata
hivyo alisema kwamba mapungufu yaliyojitokeza yalisababishwa na
viongozi wa redio kupuuzia suala la uwajibikaji na pia kuwakoesha
vitendea kazi watumishi husika na umbali wa maeneo ambayo yanatakiwa
kufanyiwa kazi kutoka katika ofisi zilizopo redio husika.
Viongozi
pia katika tathmini walishauriwa kuwapa motisha watendaji wao kwani
walionekana kulalamikia suala la kukosa motisha katika kazi ambazo
wanastahili kuzifanya ili kufuata maelekezo ya mradi wa DEP.
Wakati
huo huo Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (THRDC) moja ya taasisi
inayotetea usalama wa waandishi wa habari maeneo ya kazi imewataka
washiriki katika warsha wasipofuata maadili hawataweza kufanyakazi zao
vyema ikiwa ni pamoja na kuingia katika migogoro na wadau wa habari.
Naye
Balozi Christopher Liundi mshauri wa UNESCO amesisitiza pia haja ya
kufuata maadili na pia kuhakikisha redio za jamii zinajijenga kupitia
mtandao wao na kujiuza kwa umma.
Aidha
alishauri kwamba ripoti ya UTPC igawiwe kwa wadau wote kwani
imetengeneza msingi wa utendaji kazi katika radio za jamii ambazo kwa
sasa zinakuja kasi katika kuhabarisha mambo mbalimbali kwa jamii hasa
vijijini.
Katika
tathmini hiyo ya mradi wa DEP walikuwepo wawakilishi kutoka Ofisi ya
Msajili, Tume ya taifa ya uchaguzi (baba nay a Visiwani), Under the same
Sun, Human Rights Defenders Coalition(THRDC) na taasisi nyingine
zinazogusa masuala ya uchaguzi na amani.
Mhariri
wa Redio Kwizera FM ya Ngara mkoani Kagera, Seif Omary Upupu akichangia
mada wakati wa warsha ya siku tatu ya kutathmini mradi wa uwezeshaji wa
demokrasia na amani (DEP) kwa wanamtandao wa Redio Jamii nchini
(COMNETA).
Mhariri wa Sibuka FM, Anita Balingilaki akishiriki kuchangia mada kwenye warshi hiyo.
Mshauri
na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akifafanua jambo kwa washiriki
wa warsha hiyo.
Pichani
juu na chini ni baadhi ya Wanamtandao wa redio jamii 28 nchini
(COMNETA) waliohudhuria warsha hiyo ya siku tatu ya kutathmini mradi wa
uwezeshaji wa demokrasia na amani (DEP) kwa wanamtandao wa Redio Jamii
nchini (COMNETA) yenye lengo la kuimarisha ushiriki wa redio za jamii
nchini kuelekea uchaguzi 2015 na kura ya maoni iliyoandaliwa na Shirika
la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni
(UNESCO) na kufadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo
(UNDP) iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria
Tanzania (OUT) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mshauri
na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO) Bi. Rose Haji Mwalimu akizungumza na wanamtandao wa
redio jamii nchini (COMNETA) waliohuhduria warsha ya siku tatu ya
kutathmini mradi wa uwezeshaji wa demokrasia na amani (DEP)
iliyomalizika mwishoni mwa juma lililopita katika ukumbi wa mikutano wa
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni
Makamu mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Habari na
Mawasiliano cha Telecentre Sengerema FM, mkoani Mwanza Bw. Felician
Ncheye pamoja na Mwenyekiti wa Gender and Media in Southern, Tanzania
Chapter (GEMSAT) Dominica Haule.
Mratibu
wa Mradi wa uwezeshaji wa Demokrasia na Amani (DEP) kutoka ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bi. Beatrice Stephano akizungumzia
ushiriki wao na majukumu kwenye mradi wa DEP kwa wana-COMNETA.
Makamu
mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Habari na
Mawasiliano cha Telecentre Sengerema FM, mkoani Mwanza Bw. Felician
Ncheye (kulia) akiwa na wadau kutoka Under the Same Sun walioshiriki
kutoa mada kwenye warsha hiyo.