SERIKALI imefuta kozi zote za mafunzo ya ualimu
ngazi ya cheti kuanzia mwaka huu kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu hapa
nchini.
Tamko hilo limetolewa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Dr Shukuru Kawambwa alipokuwa akizungumza na wanachuo wa Chuo Cha
Ualimu Tabora kilichoko katika Manispaa ya Tabora.
Alisema kuanzia mwaka huu serikali imeamua kuondoa
mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti ikiwa ni mkakati maalumu wa kuanza kuboresha
kiwango cha elimu hapa nchini ambapo waalimu watakaoajiriwa kufundisha shule za
msingi na sekondari watatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha diploma na
kuendelea.
Alieleza kuwa kuanzia sasa wizara yake inataka ubora
wa elimu upatikane kutokana na ubora wa waalimu huku akibainisha kuwa waalimu
wote watakaoajiriwa katika shule za msingi na sekondari kuanzia mwaka huu
lazima wawe na elimu ya kiwango cha kuanzia diploma na kuendelea huku
akifafanua kuwa wale wasiokuwa na diploma watapewa fursa ya kujiendeleza bila
tatizo lolote.
Aidha alisema waalimu wa shule za msingi na
sekondari na wahitimu wa kidato cha sita waliopata daraja la 1-3 waliochaguliwa
kujiunga na kozi maalumu ya mafunzo ya ualimu tarajali ngazi ya cheti wote
watapelekwa vyuoni kupata masomo ya ngazi ya diploma katika vyuo maalumu
vilivyoandaliwa.
Aidha katika kuhakikisha mpango huu mpya
unatekelezwa, Dr Kawambwa alisema wizara inaandaa waraka maalumu wa maelekezo
utakaotumwa kwa wakurugenzi wote wa halmashauri zote hapa nchini.
Akijibu swali la wanafunzi wa chuo hicho waliotaka
kujua ni kwa nini mda wa kwenda kufanya
mazoezi (BTP) umepunguzwa na kuwa wiki 3 badala ya siku 60, waziri alisema
utaratibu huo ni wa dharura tu kutokana na uhaba wa fedha ila akaahidi kuwa
watajitahidi kurekebisha hali hiyo kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu.
Aidha kuhusiana na ombi la kuongezwa posho ya
mazoezi kutoka sh 4500 wanazolipwa sasa wanafunzi hao wa mafunzo ya ualimu hadi
sh 7500 wanazolipwa wanafunzi wa ngazi ya shahada, waziri aliahidi kulifanyia kazi
kutokana na bajeti ya wizara yake itakavyokuwa.
Aidha waziri aliwataka wanafunzi wote wa vyuo vya
ualimu kuhakikisha wanafaulu masomo yao yote wanayofundishwa chuoni ili waweze
kuajiriwa na serikali vinginevyo watalazimika kukaa benchi.
‘Wakati naingia wizarani nilisema sitaajiri waalimu waliofeli na
nitaendelea na msimamo huo huo kwa nia njema kabisa, jitahidini kufaulu masomo
yenu yote ya kufundishia na yale ya ziada vinginevyo hatuwapi kazi, alisema Dr
Kawambwa.