NA LUCAS RAPHAEL,TABORA
Wananchi wa wenye hasira katika kata
ya Igurubi wilayani Igunga mkoani Tabora, wameyakimbia makazi yao kwa ajili ya
kukwepa kukamatwa na jeshi la polisi baada ya kutuhumiwa kuchoma nyumba tano
za mtu anayedhaniwa kuwa ni jambazi sugu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
juzi baadhi ya wananchi Richard Ngilya na Amosi Makeleja walisema kuchomwa kwa
nyumba hizo tano kumesababishwa na jeshi la polisi wilaya ya Igunga kuwakamata
wananchi wanane (8) wa kata hiyo huku wakiendelea kumlinda jambazi huyo.
Aidha Ngilya alidai kuwa
kilichowashangaza wananchi ni kitendo kiilichofanywa na jeshi la polisi kwenda
katika kata hiyo majira ya saa saba usiku pasipo kutaarifu uongozi uliopo na
kuanza kuwafunguza huku wakiwalazimisha wakimama kuwaonyesha waume zao ambao hawajafanya
kosa la uchomaji nyumba.
Mwenyekiti wa kitongoji cha
Mwakwangu kilichopo katika kata hiyo Luhende Swala alisema askari hao waliingia
katika kitongoji chake bila kumtaarifu yeye ambapo waliwakamata baadhi ya
wananchi wa kitongoji hicho na kuondoka nao.
Aliendelea kusema baada ya kubebwa
wananchi hao ndipo wananchi walishikwa na hasira na kujikusanya na kwenda
kuchoma nyumba tatu za matembe ambazo jambazi huyo alikuwa amewajengea
ndugu zake huku idadi ya nyumba zilizochomwa zikifika tano.
Aliongeza kuwa baada ya kuchomwa
nyumba hizo tatu kundi la wananchi hao lilielekea katika nyumba za baba yake na
jambazi huyo kwa ajili ya kwenda kuzichoma lakini muda mfupi polisi wa kituo
kidogo Igurubi walifika na kuanza kufyatua risasi za moto zilizasaidia
kuwatawanya wananchi
Naye Mtendaji wa kata ya Igurubi
Mdeka Said alibainisha kuwa kuchomwa kwa nyumba hizo kumetokana na baadhi ya
wananchi kukamatwa na polisi kufuatia tukio la kuchomwa nyumba za jambazi huyo
mwishoni mwa mwaka 2014 aliongeza kuwa hadi sasa ni nyumba tano zilizochomwa
huku akifafanua nyumba mbili za bati na tatu za matembe ambapo hakutajwa
thamani ya nyumba zote.
Mtendaji huyo alitaja majina ya
wananchi walikamatwa Mbeshi Reuben, Shija Jilala, Ng’ombe Igoye, Masesa Pamba,
Martin Charles, Lushuminkono Maige, Emmanuel Mwizamhindi, Mwandu Shusha alisema
kitendo cha kukamatwa wananchi hao kimeleta mtafaruku mkubwa katika kata ya
Igurubi.
Diwani wa kata ya Igurubi ,Edson
Sadani alikiri kukamatwa kwa wananchi wake na kusema kuwa kitendo kilichofanywa
na polisi sio cha kiungwana kwa kuwa hawakushirikisha uongozi wowote hata
walipomaliza kuwakamata wananchi wake.
“Mimi kama diwani wa kata hii
natambua Mahona Malendeja ni miongoni mwa majambazi ambao wamekuwa wakiisumbua
kata ya Igurubi kwa kuwapora wananchi lakini cha ajabu polisi wameendelea
kumlinda mtu huyo huku wakiwakamata wananchi ambao hawana hatia” alisema
Akijibu tuhuma hizo Mahona
Malendeja akiwa kituo cha polisi Igunga huku akivinjari bila mashaka alisema
yeye sio jambazi wala hajawahi kupatikana na shitaka lolote linalohusu
ujambazi.
Alisema kilichosababisha nyumba
zake kuchomwa moto ni sababu ya kumwonea wivu wa kibiashara aliongeza kuwa yeye
amekuwa mfanyabiashara mkubwa anayeuza mafuta ya petrol, diesel ikiwa ni pamoja
na kununua ngozi sambamba na mazao mchangannyiko ikiwa ni pamoja na kuwakopesha
wananchi kwa riba.
Kwa upande kamanda wa polisi kamishna msaidizi mkoa wa Tabora
Suzana Kaganda alidai kuwa yuko likizo hivyo hawezi kuzungumzia kitu chochote
naomba umpigie kamanda aliyepo mimi nipo likizo.
Hata hivyo juhudi za kumpata Kaimu kamanda wa polisi Juma Bwile
alisema kuwa mpaka sasa hajapata taarifa zozote zinazohusiana na tukio hilo ila
anafuatilia leo.