HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora
imempongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa jitihada na dhamira yake ya dhati ya
kupambana na umaskini hapa nchini kupitia mpango wa kuzinusuru na kuziwezesha
kaya maskini kiuchumi.
Pongezi hizo zimetolewa juzi na Mwenyekiti wa
halmashauri ya wilaya hiyo Robert Kamoga alipokuwa akihitimisha warsha ya
kujenga uelewa wa wadau kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini unaoasisiwa na
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu.
Alisema uongozi wa Rais Jakaya Kikwete umeimarisha
zaidi dhamira ya nchi kupunguza umaskini kupitia mikakati yake mbalimbali na
kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii ambazo ni pamoja na elimu, afya na maji
kwa ushirikiano mkubwa na wananchi.
‘Nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhesh.Dr Jakaya Mrisho Kikwete kwa uongozi wake ambao
umeonyesha dhamira ya dhati ya nchi hii kupunguza umaskini wa wananchi sambamba
na kuboresha huduma za kijamii’, alisema Kamoga.
Alisema kitendo cha Rais Kikwete kuzindua Mpango
maalumu wa Kunusuru Kaya Maskini mnamo tarehe 15 Agosti 2012 kule Dodoma na
utekelezaji wake kuanza mara moja mwezi Februari 2013 kwa azma ya kufikia jumla
ya halmashauri 161 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba kililenga kutokomeza na
kundokana na umaskini katika kaya husika sambamba na utekelezaji wa miradi
mingine kwa nia ya kuzipatia kaya maskini uwezo wa kujikimu.
Kamoga alibainisha kuwa madhumuni ya mpango huu wa
awamu ya tatu ya TASAF ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato, fursa na
uwezo wa kugharamia mahitaji yao muhimu na familia zao mpango ambao
utatekelezwa kwa awamu katika kipindi cha miaka 10.
Aidha aliwakumbusha wanawarsha kuwa TASAF ni chombo
cha serikali kilichopewa jukumu la kuwezesha kufikia azma ya serikali ya
kupunguza umaskini kama ilivyoainishwa katika awamu ya pili ya MKUKUTA kwa
kutumia dhana ya ushirikishwaji jamii.
Aliongeza kuwa tangu nchi yetu ipate uhuru miaka 50
iliyopita, serikali imekuwa ikipambana na maadui watatu ambao ni umaskini,
ujinga na maradhi lengo likiwa kumwondolea mwananchi kero na vikwazo mbalimbali
vya kimaendeleo.
Kamoga alieleza kuwa serikali kwa kutambua kwamba
umaskini bado ni mkubwa miongoni mwa jamii hasa kule vijijini, ndio maana imeandaa
Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini ili kufikia malengo yake iliyoazimia katika
Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA ) awamu ya
pili.
Awali akizungumza katika warsha hiyo Mwakilishi wa
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw.Peter Luanda alisema mpango huo wa kunusuru
kaya maskini umelenga kuzinufaisha kaya masikini zilizo katika hali duni kule vijijini
na katika mitaa mbalimbali hususani watoto wenye umri chini ya miaka 5 na
wanaosoma shule na akina mama wajawazito.
Alisema kaya
hizo zitanufaika kwa kupewa ruzuku za aina mbili moja ni ruzuku ya msingi
itakayotolewa kwa kaya maskini iliyomo kwenye mpango huo na ruzuku ya pili
walengwa ni wale wanaotakiwa kutimiza masharti ya elimu na afya ili waweze kupatiwa
huduma za elimu na afya bure.
Akizungumza baada ya warsha hiyo, Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Sikonge Shadrack Mhagama alipongeza ujio wa
mpango huo wa TASAF wa kunusuru kaya maskini na kuongeza kuwa utasaidia
kuboresha maisha ya wananchi wake kwani wengi wao wamekuwa wakishindwa
kuchangia hata shughuli za maendeleo kutokana na kuwa na hali duni.
No comments:
Post a Comment