Wednesday, January 14, 2015

WANANCHI WENYE HASIRA WACHOMA NYUMBA TANO ZA MTU ANAYEDAIWA KUWA NI JAMBAZI SUGU POLILSI WAWATAWANYA KWA RISASI.

NA LUCAS RAPHAEL,TABORA

 
Wananchi wa wenye hasira katika kata ya Igurubi wilayani Igunga mkoani Tabora, wameyakimbia makazi yao kwa ajili ya kukwepa kukamatwa na jeshi la polisi baada ya kutuhumiwa kuchoma nyumba tano za mtu anayedhaniwa kuwa ni jambazi sugu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi baadhi ya wananchi Richard Ngilya na Amosi Makeleja walisema kuchomwa kwa nyumba hizo tano kumesababishwa na jeshi la polisi wilaya ya Igunga kuwakamata wananchi wanane (8) wa kata hiyo huku wakiendelea kumlinda jambazi huyo.

Aidha Ngilya alidai kuwa kilichowashangaza wananchi ni kitendo kiilichofanywa na jeshi la polisi kwenda katika kata hiyo majira ya saa saba usiku pasipo kutaarifu uongozi uliopo na kuanza kuwafunguza huku wakiwalazimisha wakimama kuwaonyesha waume zao ambao hawajafanya kosa la uchomaji nyumba.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwakwangu kilichopo katika kata hiyo Luhende Swala alisema askari hao waliingia katika kitongoji chake bila kumtaarifu yeye ambapo waliwakamata baadhi ya wananchi wa kitongoji hicho na kuondoka nao.

Aliendelea kusema baada ya kubebwa wananchi hao ndipo wananchi walishikwa na hasira na kujikusanya na kwenda kuchoma nyumba tatu za matembe  ambazo jambazi huyo alikuwa amewajengea ndugu zake huku idadi ya nyumba zilizochomwa zikifika tano.

Aliongeza kuwa baada ya kuchomwa nyumba hizo tatu kundi la wananchi hao lilielekea katika nyumba za baba yake na jambazi huyo kwa ajili ya kwenda kuzichoma lakini muda mfupi polisi wa kituo kidogo Igurubi walifika na kuanza kufyatua risasi za moto zilizasaidia kuwatawanya wananchi

Naye Mtendaji wa kata ya Igurubi Mdeka Said alibainisha kuwa kuchomwa kwa nyumba hizo kumetokana na baadhi ya wananchi kukamatwa na polisi kufuatia tukio la kuchomwa nyumba za jambazi huyo mwishoni mwa mwaka 2014 aliongeza kuwa hadi sasa ni nyumba tano zilizochomwa huku akifafanua nyumba mbili za bati na tatu za matembe ambapo hakutajwa thamani ya nyumba zote.

Mtendaji huyo alitaja majina ya wananchi walikamatwa Mbeshi Reuben, Shija Jilala, Ng’ombe Igoye, Masesa Pamba, Martin Charles, Lushuminkono Maige, Emmanuel Mwizamhindi, Mwandu Shusha alisema kitendo cha kukamatwa wananchi hao kimeleta mtafaruku mkubwa katika kata ya Igurubi.

Diwani wa kata ya Igurubi ,Edson Sadani alikiri kukamatwa kwa wananchi wake na kusema kuwa kitendo kilichofanywa na polisi sio cha kiungwana kwa kuwa hawakushirikisha uongozi wowote hata walipomaliza kuwakamata wananchi wake.

“Mimi kama diwani wa kata hii natambua Mahona Malendeja ni miongoni mwa majambazi ambao wamekuwa wakiisumbua kata ya Igurubi kwa kuwapora wananchi lakini cha ajabu polisi wameendelea kumlinda mtu huyo huku wakiwakamata wananchi ambao hawana hatia” alisema

Akijibu tuhuma hizo Mahona Malendeja akiwa kituo cha polisi Igunga huku akivinjari bila mashaka alisema yeye sio jambazi wala hajawahi kupatikana na shitaka lolote linalohusu ujambazi.

Alisema kilichosababisha nyumba zake kuchomwa moto ni sababu ya kumwonea wivu wa kibiashara aliongeza kuwa yeye amekuwa mfanyabiashara mkubwa anayeuza mafuta ya petrol, diesel ikiwa ni pamoja na kununua ngozi sambamba na mazao mchangannyiko ikiwa ni pamoja na kuwakopesha wananchi kwa riba.

Kwa upande kamanda wa polisi kamishna msaidizi mkoa wa Tabora Suzana Kaganda alidai kuwa yuko likizo hivyo hawezi kuzungumzia kitu chochote naomba umpigie kamanda aliyepo mimi nipo likizo.

Hata hivyo juhudi za kumpata Kaimu kamanda wa polisi Juma Bwile alisema kuwa mpaka sasa hajapata taarifa zozote zinazohusiana na tukio hilo ila anafuatilia leo.

 


MWISHO:

No comments:

Post a Comment