Tuesday, April 16, 2013

HAKIMU KIZIMBANI KWA RUSHWA

 
 Na Lucas Raphael,Tabora



TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa,(TAKUKURU),mkoani Tabora imemkamata na kumfikisha mahakamani  hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Urambo,Oscar Bulugu kwa tuhuma tatu za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni tano.



Mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya mkoa Issa Magoli ilidaiwa na mwanasheria wa Takukuru Simon Mashingia kuwa mtuhumia alitenda makosa hayo kati ya tarehe 15 marchi na 22 mwaka huu huko wilayani Urambo.



Upande wa mashitaka ulidai kuwa march 15 mwaka huu mtuhumia akiwa ni hakimu wa mahakama ya wilaya ya Urambo alimshawishi Lucas Raymond Changala ampe fedha hizo ili aweze kumpa dhamana ndugu yake aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya wizi wa fedha za benki ya NMB.



Mashingia alidai katika shitaka la pili kuwa tarehe 18/03/2013 hakimu huyo ambaye ni mtuhumiwa alipokea  shilingi milioni moja toka kwa Changala kama malipo ya awali ili aweze kumpa dhamana Phillipo Raymond aliyekuwa mtumishi wa benki ya nmb anayetuhumiwa kuiba zaidi ya shilingi milioni mia moja.



Mwanasheria huyo wa Takukuru alidai katika  shitaka la tatu kuwa tarehe 21/03/2013 mtuhumiwa huyo alipokea tena shilingi milioni moja ikiwa ni endelezo la malipo aliyoomba aweze kumpa dhamana mtumishi huyo wa nmb.



Hakimu huyo baada ya kusomewa mashitaka hayo matatu yote alikana na yuko nje kwa dhamana na kesi hiyo imepangwa kutajwa tena 14/05/2013.



Cha kushangaza mahakama ilimwamuru mtuhumiwa huyo kujidhamini mwenyewe kitendo ambacho kiliwashangaza watu waliokuwepo mahakamani hapo.



Mwisho.


RUFAA KESI YA UCHAGUZI WA JIMBO LA IGUNGA

 
Na Lucas Raphael,Tabora
 
Mahakama. Ya rufaa nchini  jana imeahirisha  rufaa ilifunguliwa na
mwanasheria wa serikali kupinga maamuzi yaliyomnyanganya ubunge wa
jimbo la Igunga Peter Kafumu – CCM  hadi tarehe 3/05/2013 ili
kusikiliza kwa pamoja rufaa nyingine iliyowasilishwa na mgombea huyo .
 
Uhamzi huo ulifikiwa na jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa
lilichini ya uenyekiti wa jaji Nathalia Kimaro baada ya kuridhika na
hoja za mawakili wa pande hizo mbili ambapo kwa upande wa walalamikiwa
kulikuwa na Profesa Abdalah Safari na Kamaliza Kayaga huku upande wa
serikali ukiwakilishwa na wakili Malata.
 
Jopo hilo la majaji wa mahakama ya rufaa lilitoa hoja kwa mawakili wa
pande hizo kwamba maombi ya rufaa  na 18/2013 iliyowasilishwa na
mwanasheria wa serikali na yale yaliyofunguliwa na Peter Kafumu
yanafanana na yanawahusisha watu wale wale ni vizuri yakasikilizwa kwa
pamoja.
 
Kabla ya kutolewa kwa uhamzi huo prof Safari aliiambia mahakama hiyo
kuwa wateja wao Joseph Kashindye na Wenzake kupitia chama cha
Demokrasia na Maendeleo -  CHADEMA wamechelewa kupata nakala ya hoja
za muomba rufaa na ili kutenda haki shauri hilo lisogezwe mbele.
 
Chumba cha mahakama kilijazana wafuasi na wanachama cha CHADEMA
waliokuwa wakiongozwa na mwenyekiti wa mkoa huo Kansa  Mbarouk na wale
wa wilaya za Igunga na Tabora mjini.
 
Kufuatia  uhamzi huo jopo hilo la majaji akiwemo jaji William Mandia
na jaji Semistrocles Simon Kaijage wameahirisha rufaa hiyi hadi mei
tatu mwaka huu waweze kusikiliza rufaa hizo kwa pamoja.
Kukatwa rufaa hizo kunafuatia maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Tabora, iliyotengua matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo la
Igunga mkoani hapa baada ya kubainika kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na
vitendo vya rushwa, kampeni chafu na vitisho dhidi ya wapiga kura.
 
Jaji Mary Nsimbo Shangali wa mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora,
alitangaza kutengua matokeo hayo baada ya mahakama hiyo kuridhika na
hoja saba  zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji  kati ya hoja  17
zilizowasilishwa katika mahakama hiyo.
 
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mlalamikaji aliyekuwa mgombea wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Joseph kashindye, ambaye
aliwakilishwa na wakili Maarufu nchini Profesa Abdallah Safari  ambapo
alipinga mtokeo ya uchaguzi huo akilalamikia kukiukwa kwa sheria ya
uchaguzi mkuu.
 
Upande wa Utetezi  uliwakilishwa na  mawakili Mohamed Salum Malik na
Gabriel Malata kutoka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali, Msimamizi
wa Uchaguzi jimbo la Igunga,  na mawakili Antony Kanyama na Kamaliza
Kayaga waliokuwa wakimtetea mbunge wa Igunga Peter Dalali Kafumu.
 
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa nne, Jaji Shangali alisema kuwa
mahakama imeridhika na upande wa mlalamikaji katika malalamiko yake
saba, ambayo alisema yanathibitika na kuonyesha kuwa uchaguzi huo
mdogo wa jimbo la Igunga haukuwa huru na haki.
 
Alivitaja baadhi ya kasoro zilizopelekea kutengeliwa kwa uchaguzi huo
ni pamoja na  Ahadi  iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi  Dk. John Pombe
Magufuli, kuhusu  ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo alidai kwamba  kama
wananchi hawataichagua CCM daraja hilo halitajengwa, wakati ambapo
katika kipindi hicho kulikuwa na shida kubwa ya usafiri katika eneo
hilo.
 
Alisema Kitendo pia kilichofanywa na mbunge wa Tabora mjini Ismail
Aden Rage, hakikuwa cha uungwana kwani alitumia lugha ya uongo kwa
lengo la kupotosha wapiga kura ambapo alidai mgombea wa chama cha
Demokrasia na Maendeleo  ( Chadema) amejitoa katika uchaguzi huo.
 
Jaji Mary pia alisema kitendo cha serikali kugawa mahindi ya msaada
kwa wakazi wa Igunga katika kipindi cha kampeni kitu ambacho kimeleta
fadhaa kubwa kwa wapiga kura, huku akihoji je ni nani aliyekufa njaa
katika kipindi hicho na kwamba kulikuwa na umuhimu gani wa kugawa
mahindi katika kipindi cha kampeni.
 
MWISHO.

UKATILI:-BABA AWANYONGA WATOTO WAKE WATATU MBELE YA MAMA YAO



UKATILI wa kusikitisha! Watoto watatu wa famila moja, wameuawa kikatili kwa kunyongwa huku mama yao akishuhudia. Miili yao pamoja na mama yao akiwa hai, wakatumbukizwa katika kisima cha maji. Baba wa watoto hao, Justine Albert (24) anatuhumiwa kufanya unyama huo.


Kabla ya mauaji hayo, inadaiwa baba huyo alimfunga kamba mkewe na kumziba mdomo kwa kitambaa ili asipige kelele, kisha akaanza kuwanyonga watoto wake wote watatu kwa zamu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema mauaji hayo ya kikatili yalifanyika juzi saa 11:30 alfajiri katika Kijiji cha Majimoto, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Mlele mkoani humo.


Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, kisa cha kufanya mauaji hayo ni mzozo wa mtuhumiwa na mkewe, Jacqueline Luvika (21), kwamba baadhi ya watoto hao mama huyo kazaa na jirani yao.

Watoto hao ni Frank Justine (6), Elizabeth Justine (4) na kitinda mimba Maria Justine, mwenye umri wa miezi minne.

Baada ya kuwanyonga watoto hao,

inadaiwa baba huyo alibeba miili ya watoto Frank na Eliza, na kwenda kuwatumbukiza kwenye kisima cha jirani yao, Kawaida Jonas.


Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Kidavashari, mtuhumiwa baada ya kuwatumbukiza watoto hao kisimani, alimfungua

kamba mkewe na kumtoa kitamba alichomziba mdomoni, kisha akamburuta hadi kwenye kisima hicho na kumtumbukiza.


Kugundulika Baada ya matukio hayo yanayodaiwa kufanyika alfajiri, kulipopambazuka baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, waliodamka kwenda katika shughuli zao, waliuona mwili wa mtoto ukiwa umetelekeza kando ya njia na kutambua kuwa ni Maria, ambaye ni kitindamimba katika familia hiyo.


Inadaiwa wakazi hao walisitisha safari yao na kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa, kumpatia taarifa hiyo ya kuhuzunisha, huku wakiuliza mama wa mtoto aliko.

Kamanda Kidavashari alidai mtuhumiwa aliwaeleza wakazi hao kuwa mama wa mtoto huyo, alikuwa ametoroka kwenda kusikofahamika na watoto wote.


Majibu hayo ‘rahisi’ kwa mujibu Kamanda Kidavashari, yalisababisha wakazi hao wamtilie shaka mtuhumiwa, wakaamua kutoa taarifa kituo cha Polisi kijijini hapo, ambao walifika ulipo mwili wa mtoto Maria.

Wakati wakiwa katika eneo la tukio, Kamanda Kidavashari alidai walibaini alama za mburuzo ardhini, wakaanza kuifuatilia na zikawafikisha kisimani. Walipofungua mfuniko wa kisima hicho, walishtuka kuona miili wa watu watatu, ikielea kwenye maji kisimani humo.


Askari Polisi kwa kushirikiana na wakazi wa kijiji hicho, waliopoa miili yote, lakini watoto hao wawili tayari walikuwa wamefariki, huku mama yao akiwa amekunywa maji mengi na kupoteza fahamu.


Kutokana na hali hiyo, wakazi hao walipandwa na hasira na kwenda kuvamia nyumba ya mtuhumiwa na kumkamata ili wamchome moto. Hata hivyo, Kidavashari alisema polisi walifanikiwa kufika kwa wakati katika eneo hilo na kumwokoa mtuhumiwa, ambaye kwa sasa bado ameshikiliwa Polisi kwa mahojiano.


Mama wa watoto hao kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Kijijini cha Mamba wilayani humo, ambako amelazwa kwa matibabu, lakini hadi jana bado alikuwa amezirai. Mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lake kukamilika.

NDEGE YA MAREHEMU BOBO SAMBEKE YAANGUKA


Click image for larger version. 

Name: DSC00017.JPG 
Views: 0 
Size: 163.3 KB 
ID: 90009Click image for larger version. 

Name: DSC00006.JPG 
Views: 0 
Size: 164.3 KB 
ID: 90003Habari zilizonifikia hivi punde ni kwamba ndege iliyokuwa inamilikiwa na Wakili maarufu Marehemu Nyaga Mawala aliyefariki wiki 3 zilizopita na kuzikwa huko Nairobi imeanguka ikiwa katika hatua za mwisho za kutua (final approach) katika kiwanja cha ndege cha arusha.

Taarifa zinasema kuwa ndege hiyo ilikuwa na rubani pekee anayejulikana kwa jina Babu Sambeke, au maarufu kama Bob Sambeke aliyekuwa anatokea West Kilimanjaro.


Taarifa zaidi zinasema kuwa hali ya rubani huyo si nzuri sana, na amekimbizwa kwenye hospitali ya Mount Meru kwa matibabu.


Maelezo zaidi kuhusu ajali hiyo ni kwamba ndege hiyo ilijaribu kutua baada ya masaa ya kawaida ya kufunga kiwanja(saa 12.30jioni) kupita.



ALIYEIGIZA FILAMU YA THE PASSION OF CHRIST, MAMBO SI MAZURI HOLLYWOOD


Taarifa hii ni kwa hisani ya Gospel Kitaa...

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu cha ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu


Leo katika kipengele chetu ni kwamba mwigizaji wa Hollywood aliyeigiza filamu ya "The Passion of Christ" ambayo ilipokewa kwa hisia tofauti ikiwemo watu kuripotiwa kufariki dunia mara walipoitazama na baadhi ya Wayahudi kuiponda namna walivyoigizwa, bwana Jim Caviezel amesema tangu aigize filamu hiyo mambo yake hayako sawa ndani ya mji wa Hollywood kutokana na kutopewa tenda za kutosha za ugizaji na kwamba hata zinapokuja sehemu anayotakiwa kuigiza haziendani na utaalamu au kiwango chak

Jim ambaye ni Mkristo Mkatoliki pamoja na mkewe, amesema licha ya filamu hiyo kuuza zaidi ya nakala milioni 400 lakini mambo si shwari kwake kwakuwa hapewi tena nafasi ya kuigiza lakini amesema alishapewa onyo na muongozaji wa filamu hiyo Mel Gibson ambaye alimwambia uamuzi wake wa kutaka kuigiza nafasi ya Yesu katika filamu hiyo utamfanya kutoigiza tena katika Hollywood na kufikia tamati ya uigizaji wake,muigizaji huyo alimjibu akisema kila mmoja atabeba msalaba wake, kwasababu anakiamini kile anachotaka kukifanya hivyo kila mmoja abebe msalaba wake lasivyo uzito wake utatudondokea wenyewe tusipoibeba kwahiyo achana na hayo twende tufanye kazi.

Aidha mwigizaji huyo amekiri kuwa alijua fika kwamba kuigiza nafasi ya Yesu katika filamu hiyo ilikuwa ni kuiweka uigizaji wake matatani lakini hakujali hilo na kuamua kuigiza huku muongozaji wake bwana Gibson amewahi kushutumiwa na watu mbalimbali kuhusu mwenendo wake ikiwemo suala la ulevi jambo ambalo Jim amesema watu waache kuhukumu kama wameona Gibson ni mtenda dhambi jambo wanalotakiwa kufanya ni kumuombea ili aache nasio kumuhukumu. Ameongeza kwamba imani yake ndio muongozo wake binafsi na katika utaalamu wake katika uigizaji.

Jim akipata maelezo kutoka kwa Mel Gibson wakati wakirekodi filamu hiyo.
KWA TAARIFA YAKO tangu kutoka kwa filamu hiyo mwaka 2004 hadi leo hii mwigizaji huyo ameigiza katika tamthilia na filamu nyingine ambazo hata hivyo kwa mtazamo wmingine ni kwamba labda angepata kazi nyingi zaidi. Lakini hata hivyo mwigizaji huyo ametoa kazi yake mwenyewe ya sauti hivi karibuni aliyoipa jina "Words of Promise" Ikiwa ni biblia waliyoweka kwa njia ya sauti akiwashirikisha waigizaji wenzake. Hata hivyo licha ya mambo ya uigizaji Hollywood kutokuwa kama alivyotegemea lakini kwasasa anaonekana kukaza msuli zaidi katika utumishi wa kidini kwakuzungumza kwenye makongamano na mambo mengineyo... Kwahiyo hakijaharibika kitu

WANAFUNZI 1605 WA KIDATO CHA KWANZA URAMBO ‘HAWAJARIPOTI SHULENI’

 
Na Lucas Raphael, Urambo
JUMLA ya wanafunzi 1605 kati ya 4604 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu katika wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, wameshindwa kuripoti katika shule za sekondari walizopangiwa kwa ajili ya kuanza masomo licha ya kupewa muda wa kutosha kuripoti katika shule hizo.
Hayo yalibainishwa jana na ofisa elimu (taaluma) anayeshughulikia elimu ya sekondari wilayani  Urambo, Grace Nghambi Monge, katika taarifa iliyoandaliwa na idara hiyo ikionyesha idadi halisi ya wanafunzi walioingia kidato cha kwanza mwaka huu, ambapo taarifa hiyo inaonyesha kwamba wanafunzi 1605 sawa na 35%  ya waliotakiwa kuingia sekondari hawajaripoti.
Nghambi alieleza kuwa kati ya wanafunzi hao 1605 wavulana ni 800 na wasichana ni 805, na walioripoti mpaka sasa hivi ni 2989 sawa na 65% tu ambapo wavulana ni 1713 na wasichana ni 1276, aliongeza kuwa idadi hiyo ya watoto walioshindwa kuripoti ni kubwa sana ukilinganisha na mikakati waliyokuwa wamejiwekea.
Nghambi alibainisha sababu zilizochangia wanafunzi hao kushindwa kuripoti shuleni kuwa ni baadhi yao kuolewa mapema, kukosa ada na mahitaji muhimu yanayotakiwa shuleni ikiwemo sare  za shule, madaftari, kalamu na kadharika, na hii inatokana na umaskini wa wazazi walio wengi katika wilaya hii ambao unawafanya kuwa na mwamko mdogo katika suala la elimu.   
Nghambi aliongeza kuwa mambo mengine yaliyochangia kutoripoti ni kitendo cha wazazi kuwatumikisha watoto wao katika shughuli za kilimo hasa tumbaku na wazazi wengine kuwazuia watoto wao kuendelea na masomo kwa kisingizio cha kupoteza nguvu kazi katika kilimo hicho.
Aidha Nghambi aliongeza kuwa watoto wengine hususani wale wanaotoka katika jamii ya wafugaji wameshindwa kuripoti sekondari kwa sababu ya kuhamahama kwa wazazi wao kwa ajili ya kutafuta malisho ya mifugo yao, jambo linalowafanya kuishi umbali mrefu na mahali shule ilipo.
Akizungumzia mikakati ya kupambana na changamoto hizo, Nghambi alisema kwamba halmashauri ya wilaya hiyo imekusudia kuwasaka na kuwafungulia mashtaka wazazi wote waliowazuia watoto wao kujiunga na wenzao sambamba na kuwaelimisha wazazi hao juu ya umuhimu wa kumsomesha mtoto na madhara ya kumkosesha haki hiyo ya msingi.
Aidha, halmashauri hiyo pia imekusudia kuongeza nyumba za waalimu na hosteli za wanafunzi kwa baadhi ya shule ili kupunguza kero ya umbali mrefu uliopo kati ya shule na makazi ya watu.
Naye Coleta Hassan, ambaye ni Ofisa elimu idara ya msingi, akizungumzia mikakati iliyowekwa na halmashauri hiyo katika suala la kuboresha elimu, alisema kuwa wamekusudia kukarabati madarasa, ofisi, nyumba za waalimu, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wazazi  kuchangia chakula ili kuanzisha utaratibu wa kuwapatia chakula cha mchana wanafunzi wote wanapokuwa shuleni.

TFF YAMPIGA FAINI KOCHA WA RHINO KWA VITENDO VYA KISHIRIKINA


 

KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha daraja Rhino Rangers kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo kwenye mechi mbili tofauti.

Mechi hizo ni kati ya Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu hiyo waingie bure uwanjani.

Mchezaji wa timu ya Pamba ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya kumrushia chupa ya maji mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.

Nao wachezaji Joseph Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya vitendo vinavyoshiria ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Morani iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. 

Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.
Klabu ya Villa Squad imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United wakati Majimaji imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.

Vilevile Msimamizi wa Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda aliwatukana waamuzi kwenye mechi hiyo, na suala lake litafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Pia uongozi wa Uwanja wa Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za FDL msimu ujao.

MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 11 mwaka huu) litakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari. Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)