JUMLA
ya wanafunzi 1605 kati ya 4604 waliochaguliwa kujiunga kidato cha
kwanza mwaka huu katika wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, wameshindwa
kuripoti katika shule za sekondari walizopangiwa kwa ajili ya kuanza
masomo licha ya kupewa muda wa kutosha kuripoti katika shule hizo.
Hayo yalibainishwa jana na ofisa elimu (taaluma) anayeshughulikia elimu ya sekondari wilayani Urambo,
Grace Nghambi Monge, katika taarifa iliyoandaliwa na idara hiyo
ikionyesha idadi halisi ya wanafunzi walioingia kidato cha kwanza mwaka
huu, ambapo taarifa hiyo inaonyesha kwamba wanafunzi 1605 sawa na 35% ya waliotakiwa kuingia sekondari hawajaripoti.
Nghambi
alieleza kuwa kati ya wanafunzi hao 1605 wavulana ni 800 na wasichana
ni 805, na walioripoti mpaka sasa hivi ni 2989 sawa na 65% tu ambapo
wavulana ni 1713 na wasichana ni 1276, aliongeza kuwa idadi hiyo ya
watoto walioshindwa kuripoti ni kubwa sana ukilinganisha na mikakati
waliyokuwa wamejiwekea.
Nghambi
alibainisha sababu zilizochangia wanafunzi hao kushindwa kuripoti
shuleni kuwa ni baadhi yao kuolewa mapema, kukosa ada na mahitaji muhimu
yanayotakiwa shuleni ikiwemo sare za shule, madaftari,
kalamu na kadharika, na hii inatokana na umaskini wa wazazi walio wengi
katika wilaya hii ambao unawafanya kuwa na mwamko mdogo katika suala la
elimu.
Nghambi
aliongeza kuwa mambo mengine yaliyochangia kutoripoti ni kitendo cha
wazazi kuwatumikisha watoto wao katika shughuli za kilimo hasa tumbaku
na wazazi wengine kuwazuia watoto wao kuendelea na masomo kwa kisingizio
cha kupoteza nguvu kazi katika kilimo hicho.
Aidha
Nghambi aliongeza kuwa watoto wengine hususani wale wanaotoka katika
jamii ya wafugaji wameshindwa kuripoti sekondari kwa sababu ya
kuhamahama kwa wazazi wao kwa ajili ya kutafuta malisho ya mifugo yao,
jambo linalowafanya kuishi umbali mrefu na mahali shule ilipo.
Akizungumzia
mikakati ya kupambana na changamoto hizo, Nghambi alisema kwamba
halmashauri ya wilaya hiyo imekusudia kuwasaka na kuwafungulia mashtaka
wazazi wote waliowazuia watoto wao kujiunga na wenzao sambamba na
kuwaelimisha wazazi hao juu ya umuhimu wa kumsomesha mtoto na madhara ya
kumkosesha haki hiyo ya msingi.
Aidha, halmashauri
hiyo pia imekusudia kuongeza nyumba za waalimu na hosteli za wanafunzi
kwa baadhi ya shule ili kupunguza kero ya umbali mrefu uliopo kati ya
shule na makazi ya watu.
Naye
Coleta Hassan, ambaye ni Ofisa elimu idara ya msingi, akizungumzia
mikakati iliyowekwa na halmashauri hiyo katika suala la kuboresha elimu,
alisema kuwa wamekusudia kukarabati madarasa, ofisi, nyumba za waalimu,
ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wazazi kuchangia chakula ili kuanzisha utaratibu wa kuwapatia chakula cha mchana wanafunzi wote wanapokuwa shuleni.
No comments:
Post a Comment