Usafiri
baiskeli mkoani Tabora wazidi kuimarisha ajira kwa vijana hatua ambayo
sasa imefanya kuwepo kwa ongezeko la vijana wengi mjini kuliko
ilivyokuwa hapo awali,kwa hivi sasa imeshuhudiwa baadhi ya vijana wa
vijiji jirani na Tabora mjini wamekuwa wakijidamka mapema asubuhi kuja
mjini kufanya kazi ya kusafirisha abiria kwa usafiri huo wa baiskeli na
kujipatia fedha kwa ajili ya kujikimu kimaisha wakati huu wa majira ya
kiangazi ambapo vijijini hakuna shughuli za kilimo.Hata hivyo licha ya
vijana hao kupata fursa ya kujiajiri wenyewe lakini wamekuwa katika
mazingira hatarishi kutokana na ukweli kwamba wengi wao hawajui sheria
za usalama barabarani na hivyo kujikuta wanavunja sheria na kusababisha
ajali zinazochangia vifo visivyo vya lazima au kubaki na ulemavu wa
kudumu.Jambo hili linahitaji kuchukuliwa hatua ya kuwadhibiti vijana hao
bila kuathiri mwenendo mzima wa ajira zao kwakuwa wengi wao kutokana na
ajira hizo wanategemewa na familia zao.Ajira za vijana kwa kutumia
usafiri wa baiskeli katika mtazamo wa harakaharaka ni dhahiri kwamba ni
ajira tulizozitegemea kwa kile kinachoonekana katika fikra za haraka kwa
vijana waliowengi ni kujipatia fedha za chapchap kupitia mpango huo
usio rasmi.Aidha kwa upande mwingine ni kweli kwamba kwasasa mkoa wa
Tabora hakuna viwanda au kazi nyingine zaidi ya kupata vibarua kwenye
majengo ya watu binafsi ambayo malipo yake ni kati ya shilingi 3000 na
5000 kwa kutwa nzima.Ukiachilia mbali ajira kwenye makampuni ya ulinzi
imekuwa na usumbufu kwa vijana kutokana na kutolipwa mishahara kwa
wakati jambo ambalo linawafanya vijana wengi kuona ni bora zaidi
aendeshe baiskeli kuanzia majira ya saa 12 asubuhi hadi saa tatu usiku
ambapo hujipatia wastani wa kiasi cha shilingi elfu kumi.Hii inawafanya
idadi kubwa vijana kuingia kwenye ajira hii bila kikwazo kwani kwa
wanaoishi mjini huweza kumudu kulipa kodi ya pango ya shilingi elfu kumi
kwa mwezi lakini hata kuendesha maisha yake na familia ya watu wanne
yaani Mke,watoto wawili na yeye mwenyewe.Kuendesha baiskeli hakuhitaji
leseni wala kikwazo chochote kinachowabana kisheria zaidi ya kujaza
upepo kwenye tairi za baiskeli na kuanza kunyonga pedeli kulingana na
uzito wa mteja aliobebwa kwenye usafiri huo.Ni kazi nyepesi kama
waionavyo vijana wenyewe.Lakini kwa wachunguzi wa mambo wanasema kuwa
hata wimbi la vibaka katika maeneo mbalimbali Tabora mjini limepungua
kwa kiasi kikubwa kwakuwa kijana anayejihusisha na ajira hiyo ya usafiri
wa baiskeli anapomaliza muda wake hiyo saa tatu usiku huwa amechoka
sana hata hawezi kwenda kukaa vijiweni na kujihusisha na vitendo
viovu. |
No comments:
Post a Comment