(Picha zote na Kibada Kibada –Mlele Katavi)
Na Kibada Kibada –Mlele Katavi.
Wimbi la mauaji kwa watu wenye
umri kuanzia miaka 60 na kuendelea Wilayani Mlele Mkoani Katavi
linaonekana kushika kasi na kutishia hali ya ulinzi na usalama kama
hatua za makusudi hazitachukuliwa.
Hii ni kwa Mujibu wa Taarifa ya
Hali ya ulinzi na Usalama Wilayani humo iliyotolewa na Mkuu wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa wilaya hiyo , Zabron Ibeganisa kwenye
Mkutano Mkuu wa Baraza la Madiwani uliokuwa ukipokea taarifa ya
utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizotekelezwa kwa kipindi cha
mwaka wa 2013/2014.
Mkuu huyo wa upelelezi wa makosa
ya jinai alieleza kuwa changamoto zitokanazo na matukio ya mauaji ni
kubwa katika wilaya hiyo na watu wanaolengwa na mauaji hayo ni wale
wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea ambapo kwa sehemu kubwa mauaji
hufanyika nyakati za usiku kwa kuwavamia walengwa kwenye makazi yao.
Alisema katika matukio 24
yaliyotokea, watu 24 kwa kipindi cha januari hadi juni mwaka
2014 wameuwawa na waliolengwa hasa ni watu wa umri huo.
Alisema kuwa wauaji hao hutumia
silaha zenye makali kama panga,shoka, na sime kuwakata waliowalenga na
kisha kutoweka bila kuchukua kitu chochote.
Mauaji haya yanafanana sana na jinsi yanavyotokea katika mikoa ya Shinyanga kwa kuwaua vikongwe kwa imani kwamba ni wachawi.
Aidha akifafanua zaidi alieleza
kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita kuanzia mwezi januari hadi
juni 2014 , yametokea mauaji 24 na watu 24 wameuwawa ambapo kati ya
mauaji hayo watuhumiwa sita walikamatwa.
Akibainisha hali ya uhalifu katika
wilaya hiyo alieleza kuwa matukio mbalimbali ya makosa madogo ya
kuwania mali yalikuwa 107 makosa makubwa dhidi ya binadamu kwa mauaji
yalikuwa 24, kubaka 23,kulawiti mawili ,makosa madogo dhidi ya Binadamu
yalikuwa 194, makosa madogo dhidi ya uvunjwaji wa maadili yalikuwa 108,
ajali zilizosababisha vifo ni mbili,ajali zilizosababisha majeruhi
zilikuwa 39, ajali za kawada 17, makosa mengine 844.
Makosa makubwa dhidi ya maadili ya
jamii kama kupatikana na bangi yalikuwa manane, kupatikana na pombe ya
moshi 8, makosa ya kupatikana na nyara za serikali yalikuwa matatu na
kupatikana na silaha moja
Ipo changamoto kutokana na ugumu
uliopo wa kuwatambua wauaji ,hata hivyo jeshi la polisi linatoa wito kwa
jamii kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo na kuwaasa wana
jamii kuendeleza ule utaratibu wa daftari la wakazi kwa kuwaorodhesha
wakazi kwenye maeneo kwa kuwa ni muhimu na litasaidia kuwatambau wageni
wanaoingia kwenye maeneo na iwapo watakuwa na nia mbaya watabainika.
No comments:
Post a Comment