Serikali
wilayani Nzega katika mkoa wa Tabora imeagiza wananchi wote waliovamia
misitu ya hifadhi ya Ipala iliyoko katika kijiji cha Ugembe, kata ya
Mwakashanhala wilayani humo kuondoka mara moja kwa hiari yao, vinginevyo
wataondolewa kwa nguvu.
Agizo
hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Nzega, Bi. Zaituni Msangi wiki
iliyopita katika doria maalumu ya kutembelea misitu hiyo ambayo
iliripotiwa kuvamiwa na wananchi hao na kuendesha shughuli za aina
mbalimbali kinyume na taratibu.
DC
alisema kuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona vitendo vya
uvamizi wa maeneo maalumu yaliyohifadhiwa na serikali vikiendelea
kuongezeka hapa nchini hali inayochangia kwa kiwango kikubwa uharibifu
wa mazingira.
‘Hawa
watu hawastahili kuishi katika maeneo haya, uwepo wao ni kinyume na
sheria, lakini pia wanaharibu mazingira ya hifadhi hizi za serikali, kwa
sababu wanakatakata miti ovyo kwa ajili ya shughuli zao za kilimo,
ufugaji na uchomaji mkaa sambamba na uvuvi wa samaki’, alisema DC.
Aidha,
DC alibainisha kuwa wananchi waliovamia hifadhi hiyo ya Ipala wamekuwa
wakidanganywa na baadhi ya watu wanaojifanya kuwa ni maofisa wa serikali
ili watoe hela kwa kisingizio cha kuwamilikisha maeneo hayo bila
kutambua kuwa mtu yeyote haruhusiwi kuweka makazi katika maeneo ya
misitu ya hifadhi.
‘Tayari
tumeweka kikosi kazi cha kufanya doria katika maeneo hayo, na
tumeshapewa taarifa za uwepo wa mtu mmoja anayewarubuni wananchi hao kwa
kujifanya kuwa yeye ni ofisa wa serikali na ameahidi kuwagawia viwanja
katika maeneo hayo ya hifadhi, tumeshaweka mtego wa kumkamata’,
aliongeza DC.
DC
alibainisha kuwa doria hiyo inayofanywa na watu 18 kutoka vikosi vya
FFU, wanyama pori, wataalamu wa maliasili na mgambo, tayari imefanikisha
kukamatwa kwa magunia 400 ya mkaa ambao ulikuwa umehifadhiwa katika
nyumba zilizoko ndani ya msitu huo wa hifadhi, japo watuhumiwa wote
walifanikiwa kukimbia.
Katika
msako huo mbali na kukamatwa kwa magunia hayo ya mkaa, kikosi hicho pia
kilifanikiwa kukamata gobole 1 na silaha zingine za kijadi zilizokuwa
zikitumiwa na wavamizi hao katika msitu huo na bado msako unaendelea,
mpaka wahakikishe wavamizi wote wamerudi kwao sambamba na kukomesha
usafirishaji wa mkaa.
Aidha,
DC aliongeza kuwa katika jitihada za kuhakikisha kuwa uvamizi huo wa
hifadhi unadhibitiwa, wameamua kuitisha kikao cha ujirani mwema ili
kuweka mikakati ya pamoja na kulifanya zoezi hili kuwa endelevu kwa
kuwashirikisha wakuu wa wilaya jirani za Shinyanga, Kishapu na Nzega
yenyewe.
No comments:
Post a Comment