Monday, August 25, 2014

"CCM WAMKATAA KATIBU WA WILAYA YA TABORA MJINI,WAMEDAI ANAKIPELEKA CHAMA PABAYA"

 

Katibu wa CCM mkoa wa Tabora Bw.Idd Ame akitoka nje baada ya kuahirishwa kwa mkutano wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ambapo wajumbe walianza kwa kumkataa Katibu wa CCM wilaya ya Tabora mjini  Bw.Bakari Mfaume na kushinikiza uongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho kumhamisha katibu huyo ambaye walidai kuwa amekuwa chanzo cha migogoro ndani ya Chama. 
Pamoja na kuahirishwa kwa mkutano huo lakini wajumbe hao bado wameendelea kusisitiza kuwa hawatakuwa tayari kufanyakazi na Katibu wa CCM wilaya ya Tabora mjini ambaye tayari malalamiko ya wajumbe hao walishayafikisha kwa Katibu mkuu wa CCM Taifa Bw.Abdulrahman Kinana licha ya kuwa hadi sasa wajumbe hao  hawajaona mafanikio.Hata hivyo Chama cha mapinduzi wilaya ya Tabora mjini kimekuwa katika sekeseke la mvurugano wa wanachama na viongozi hali ambayo imeelezwa na baadhi ya wanaCCM imetokana na Katibu huyo kudaiwa kuwa anatumiwa na baadhi ya vigogo hasa kwenye maandalizi ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
 Na Mwandishi wetu 

Sakata la Wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Tabora mjini kuendelea kumkataa Katibu wa CCM wilaya ya Tabora mjini bado linaendelea kuchukua kasi na hivyo kuanza kusikika hadharani baada ya wajumbe hao kutoka nje ya kikao cha kupokea utekelezaji wa ilani ya Chama hicho,mkutano uliowakutanisha wajumbe hao na timu ya wataalamu kutoka halmashauri ya manispaa ya Tabora.
Katika mkutano ulioanza majira ya saa nne na nusu ulifanyika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi,ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Katibu wa CCM mkoa wa Tabora Bw.Idd Ame,mara baada ya hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo wajumbe walinyoosha mikono na kudai kuwa hawamtaki Katibu wa CCM wilaya ya Tabora Bw.Bakari Mfaume kutokana na kukosa imani naye na hivyo kuhitaji aondolewe katika mkutano huo muhimu kwa maendeleo ya wilaya ya Tabora.
Hata hivyo pamoja na Katibu wa CCM mkoa wa Tabora  Bw.Ame kuingilia kati na kujaribu kuwatuliza wajumbe kwa kuwafahamisha kuhusu lalamiko lao dhidi ya Katibu wa wilaya lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda kutokana na baadhi ya wajumbe kuanza kutoka nje ya kikao hicho.
"Tafadharini wanaCCM wenzangu suala la Katibu inaeleweka wazi kuwa linashughulikiwa na makao makuu kwahiyo sisi tuvute subira,tusubiri maamuzi ya Katibu mkuu Kinana,nawaombeni tuliache kwa muda ili tuendelee na kikao chetu hili lisituharibie mipango yetu jamani"alisisitiza Bw.Ame
Pamoja na rai hiyo ya Katibu wa mkoa Bw.Ame Wajumbe waliendelea kutoka nje ya kikao hicho mmoja baada ya mwingine licha ya kuwa baadaye kililazimika kuahirishwa kutokana na kutokuwepo kwa Meya wa halmashauri ya manispaa ya Tabora Bw.Ghulam Dewij ambaye alikuwa kwenye ziara ya kichama jumuiya ya Wazazi mkoa wa Tabora.
Kufuatia kuendelea kuwepo kwa sakata hilo la wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Tabora mjini na baadhi ya wanachama wa chama hicho kumkataa Katibu wa wilaya ni wazi kwamba Chama cha Mapinduzi kimekwishaingia kwenye mgogoro ambao suluhisho la  msingi wake ni kuondolewa kwa Katibu huyo wa CCM wilaya ya Tabora Bw.Bakari Mfaume kama madai ya baadhi ya wanachama wa chama hicho wanavyoeleza.
''Sisi tunachojua Katibu huyu anatumiwa na viongozi wachache wenye pesa kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu,mpaka viongozi hao wamefikia kuwa wanachangishana wanamlipa mshahara mwingine nje ya mshahara anaolipwa na CCM,sasa tunasema hatumtaki,atuachie chama chetu,kwanza amekwishafanya madudu kwenye Wilaya karibu zote za Tabora,anakiharibu chama jamani"    
Aidha kwa upande mwingine baadhi ya Wazee wa Tabora mjini ambao hawakutaka kutajwa majina yao wameeleza kuwa endapo viongozi hawatakuwa makini kuhusu madai ya wajumbe na wanaccm kwa ujumla,kuna wasiwasi mkubwa wa kupoteza viti vingi vya serikali ya mtaa na pengine hata nafasi za udiwani na ubunge pia.
Hata hivyo kabla ya kuanza kwa mkutano huo Katibu huyo wa CCM wilaya ya Tabora mjini Bw.Mfaume aliwafukuza waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mkutano huo kwa madai kwamba yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuwaita waandishi endapo kama watahitajika na kuwatishia kuwa anaweza akawalalamikia kwa kuharibu mkutano huo jambo lililoleta tafsiri mbaya kwa waandishi wa habari na watu walioshuhudia kitendo hicho.
"Sasa huyu Katibu anataka kuficha nini wakati hiyo taarifa itakayosomwa kwa wajumbe wa halmas  hauri kuu inatakiwa wananchi wajue nini Serikali yao imefanya,au ana ajenda za siri?baadhi ya watu waliokuwa nje ya ukumbi huo walisikika wakihoji uhalali wa Katibu huyo Bw.Mfaume kuwafukuza waandishi wa habari eneo la mkutano huo.

No comments:

Post a Comment