Monday, February 2, 2015

RAGE AANDAMWA NA WAPAMBE WAKE - CCM


Mbunge wa jimbo la Tabora mjini Mh.Ismail Aden Rage.

Mwandishi wetu -Tabora
 
Katika hali ambayo si ya kawaida ingawa kisiasa ni jambo la kawaida kabisa na huenda likawa ni jambo ambalo hataweza kulisahau maishani mwake Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Ndugu Aden Rage kutokana na mbinu chafu zinazodaiwa kuanza kufanyiwa mbunge huyo na kuhakikisha anapoteza nafasi yake wakati wa kura za maoni kupitia Chama cha Mapinduzi

Mtandao huu wakati unaendelea kufuatilia makundi ndani ya CCM kwa mkoa wa Tabora katika maandalizi ya kuwania nafasi mbalimbali ikiwemo ya Udiwani na Ubunge, imebainika kuwa kundi linalodai kumuunga mkono Mbunge wa jimbo la Tabora mjini Aden Rage limekuwa ni miongoni mwa wasaliti wa kwanza wa kupanga mipango na mbinu chafu za kumuhujumu kwa wajumbe ambao watakaoingia kupiga kura za maoni wakati utakapowadia.

Moja kati ya mbinu chafu ambazo hata Mheshimiwa Rage hazitambui zinazodaiwa kufanywa na wapambe wake ni pamoja na kuwataka wajumbe ambao kati yao ni makatibu wa matawi, kata, wanajumuiya mbalimbali zikiwemo za wazazi, UWT na kiasi kwa UVCCM na kuonesha hali ya kumuunga mkono mbunge huyo wakati anapokutana nao kwenye vikao vya siri na vya hadharani jambo ambalo ni kinyume.

Hata hivyo mwanya huo pia unadaiwa kutumiwa na Wapambe hao kumuhadaa Mheshimiwa Rage ajione kuwa yuko pamoja nao kumbe miongoni mwao wamejipanga kuvuta fomu wakati wa kura za maoni jambo ambalo Rage hajalijua na hasa kwa wengine ambao wamepandikizwa katika kambi yake huku ikionesha namna anavyowaamini na kujihakikishia kuwa ndio watu watakaompa msaada mkubwa wa kupiga debe wakati wa uchaguzi katika kura za maoni.

Aidha kwa upande mwingine wapo wapambe ambao ni viongozi ndani ya CCM wameonesha hali ya kumsaidia katika masuala mbalimbali lakini pindi Mheshimiwa Rage anapokuwa hayupo katika jimbo lake hutumia nafasi hiyo wao kujinadi na hata kutoa fedha kwa wanaccm huku wakiendelea kumchafua kisiasa.

Katika hali hiyo pia baadhi yao wamefanikiwa katika mpango mahususi wa kumjengea mazingira Mheshimiwa Rage akosane na baadhi ya viongozi wa CCM ngazi za wilaya na mkoa jambo ambalo ni hatari kisiasa ingawa mpango mwingine ulikuwa umeandaliwa na wapambe wake kuhakikisha wanamuingiza kwenye mgogoro mkubwa wa Waislamu katika msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni mpango ulikwama baada ya mbunge huyo kutahadharishwa mapema na kadhia hiyo.

Wapambe hao wanaodaiwa kumuandama kimyakimya Mheshimiwa Rage ambao wamegawanyika katika makundi mawili hadi matatu,Wachache ni wale ambao wamejipanga kuvuta fomu kuwania nafasi ya Ubunge kwa kutambua madhaifu aliyonayo,Wapili ni wale ambao wametumwa kuwa karibu naye na kujifanya wanamuunga mkono na kujaribu kumpandikizia chuki dhidi ya watu wengine ili Rage aendelee kuwathamini pamoja na kuvujisha siri za vikao vya ndani,wengine ni wale ambao wapo kwa ajili ya kutaka kujipatia fedha ingawa kundi hili Rage amekuwa makini sana na kuchukua tahadhari.

Kwawale ambao ni wapambe waliotumwa kuwa karibu na Mheshimiwa Rage kwa lengo la kuchimbua habari mbalimbali na kuandaa mazingira ya siasa chafu dhidi yake,mtandao huu umebaini kuwa malipo yao yanatokana na taarifa wanazochukua kwa mbunge na kuzipeleka kwa waliowatuma ili kuweza kufanikisha mikakati yao. 

MAONI YA MTANDAO:
Mheshimiwa Rage jaribu ulipitie upya na uwe makini sana na kila anayejidai anakuunga mkono kwakuwa hadi sasa kwa wapambe wote ulionao ni mmoja tu ndiye yupo pamoja nawe na Mungu anajua hilo.Kumbuka yaliyowatokea waheshimiwa kama Prof.Mgombelo, Mwanne Mchemba na Aziza Suleyum ambao walijenga mazingira ya kuwaamini watu wao wa karibu na hatimaye Kijani ikageuka kuwa Nyekundu. 

Kuna watu upo nao wenzako wapo kazini,ni lazima wafikishe taarifa ili wapate malipo yao,zipo fedha zinatoka ndani ya mkoa na nyingine inatoka nje ya mkoa,tumia mbinu ulizotumia wakati ukiongoza klabu ya Simba najua lazima utawabaini.

No comments:

Post a Comment