Thursday, May 8, 2014

ZENA MOTTE NDIYE MSHINDI WA REDDS MISS TABORA 2014


Washindi wa Mashindano ya Redds Miss Tabora 2014 katikati ni Zena Motte mbaye ndiye mshindi wa kwanza,wapili ni Elizabeth Mkende wakati nafasi ya tatu ilichukuliwa na Lencer Kotato kati ya washiriki wanane walioshiriki mashindano hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Teofilo Kisanji mjini Tabora.
 

Redds Miss Tabora 2014

MWANAMKE AKAMATWA AKIMILIKI BUNDUKI ISIVYO HALALI -TABORA



Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Suzan Kaganda.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 05/05/2014.
Ndugu waandishi wa habari, Jeshi la Polisi mkoa wa Tabora ifuatayo ni taarifa ya tukio moja la kifo na taarifa ya  Operesheni inayoendelea katika wilaya zote za mkoa wa Tabora. Ambapo kufuatia operesheni hizo tulifanikiwa kukamata watuhumiwa wa makosa mbali mbali kama ifuatavyo:-


Mnamo tarehe 04.05.2014 majira ya saa 10:00hrs huko eneo la Utwigu wilaya ya Nzega FRANCE S/O AMBROSE HUSSEIN 11yrs, Mnyamwezi mwanafunzi wa darasa la Tano katika shule ya Msingi Mwanhala alifariki dunia baada ya kutumbukia katika bwawa la maji ambapo alikuwa ameenda kwa ajili ya kuogelea.


Tarehe 01.05.2014 huko wilaya ya Nzega alikamatwa FROLA D/O SHIJA, 28yrs, mnyamwezi, mkulima na mkazi wa kujiji cha Igalula akiwa na bunduki aina ya Gobore ambayo anamiliki kinyume na sheria. Mtuhumiwa amefikishwa mahakamani.


Aidha tarehe 02.05.2014 huko katika eneo la Utwigu kata ya Nyasa wilaya ya Nzega walikamatwa SHIJA S/O KAPONA, 39yrs, Mnyamwezi, Mkulima na BAHATI S/O SHIJA, 28yrs, wote wakazi wa Utwigu wakiwa na vipodozi aina ya Lemon Vate Cream 02, Beater Soap 02, Deproson chupa 15, Demason 01, na Banistar 01, vipodozi hivyo vilibainika kuwa havifai kwa matumizi ya binadamu na mtaalam kutoka TFDA. Watuhumiwa wote wamefikishwa mahakamani.


Katika opereheni hii pia wamekamatwa PILI D/O BUNDALA 65yrs, Mnyamwezi, MACHIBYA S/O MGETE 40 yrs, Mnyamwezi, KULWA S/O MASANJA, 35yrs, Msukuma, DAUDI S/O KABOGA 28yrs, Msukuma, MWAJUMA D/O RAJABU, 30yrs, Mnyamwezi, na MWASITI D/O MUHOJA 37yrs, wote wakazi wa kata ya Nyasa – Nzega wakiwa na Pombe ya moshi lita 15, pia watuhumiwa wote hawa ni watumiaji na wauzaji wa pombe hiyo haramu. Wote wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.


Jeshi la Polisi linazidi wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi lao ili kukomesha na kutokomeza vitendo vyote vya uhalifu na kuwafichua wahalifu, aidha wazazi napenda kuwakumbusha wazazi kuwaangalia watoto na kuwafuatilia katika michezo yao ya kila siku, pia napenda kuwaasa wananchi kufuata sheria za nchi na pia kwa wale wote ambao wanamiliki magobore kinyume na sheria wasalimishe magobore hayo kwa kuwa operessheni hii ni endelevu.

Imetolewa na :-

SUZAN KAGANDA – ACP

KAMANDA WA POLISI

MKOA WA TABORA.

Sunday, April 27, 2014

UKAWA WAMJIBU RAIS KIKWETE


ukawa5 eeb08
Na Hudugu Ng'amilo
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) warudi bungeni akidai hawana sababu ya kwenda kushitaki kwa wananchi kwa sababu watawacheka na kuwasikitikia, umoja huo umemjibu wakisema wapo tayari kuchekwa.

Akihutubia vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi, siku moja kabla ya sherehe za miaka 50 ya muungano, Rais Kikwete alisema kuwa huko nje wanakotaka kwenda UKAWA siko na siku yake sio sasa, hivyo akawaomba wasipoteze fursa hiyo muhimu ya kutoa mawazo yao bungeni ili yafanyiwe kazi.

Alisema wananchi hawahusiki wala hawana namna ya kuwasaidia kwani mengi ya hayo yanayowakasirisha ni matatizo waliyoyazusha wao.

Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa
kama Kikwete anafikiri kwamba watarudi bungeni kwenye mijadala ya dharau, ubaguzi na matusi inayofanywa na wajumbe wa CCM, basi hajui chimbuko la tatizo.

"Kadiri anavyoendelea kuliacha Bunge liendelee na mijadala ya kibaguzi na matusi, taifa linazidi kupasuka na washauri wake hawamwelezi tatizo hilo," alisema.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atalitumbukiza taifa kwenye machafuko ingawa yeye anafanya utani kwa kuipasua nchi na kushangilia kauli za kibaguzi, kejeli na matusi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa CCM.

"Rais na wasaidizi wake inaelekea hawajasikiliza hata kauli zinazotolewa na viongozi wa dini kuhusu rasimu ya Warioba, atuache twende kwa wananchi, wao ndio wataamua. Tumevumilia kwa kiwango fulani, lakini itafika mahali uvumilivu utaisha, kwani hatuwezi kuendelea kuzuiliwa kufanya mikutano na jeshi la polisi wakati mikutano ya CCM inafanyika kote nchini kutuchafua," alisema Mbowe.
 

CCM KIMEPANGA MKAKATI WA KUENGUA WATAKA URAIS WANAUME


migiro ec14d
Na Hudugu Ng'amilo
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga mkakati mpya wa kuengua wataka urais wanaume kwa kuingiza hisia za kijinsia kama walivyofanya kumdhibiti aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, alipotaka kugombea tena nafasi hiyo mwaka 2010.

Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wameliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa mkakati huo unalenga zaidi kumng'oa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye anaonekana tishio kwa wenzake wanaotajwa kutaka urais.
Kwa mkakati huo, kundi la wana CCM walio karibu na Rais Jakaya Kikwete, wameanza kuzungumzia jinsi ya kumpitisha Dk. Asha-Rose Migiro agombee urais katika uchaguzi mkuu ujao 2015.

Kisingizio wanachotumia katika kampeni yao ya siri, ni kusaka kura za wanawake.

Katika mkakati huo, wanamwandaa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, kuwa Waziri Mkuu. Tayari Membe ameshatangaza kuwa hatagombea ubunge mwaka 2015.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, Membe ndiye alikuwa akipigiwa chapuo zaidi miongoni mwa makada wa CCM ili kurithi mikoba ya Rais Kikwete, lakini kutokana na uhusiano wa kifamilia uliopo baina ya wawili hao, sasa ameshawishiwa kuwa atakuwa waziri mkuu endapo Dk. Migiro atashinda.

Wiki hii, gazeti dada la Tanzania Daima Jumatano liliripoti mkakati wa kumzima Lowassa asigombee urais, ambao unaendeshwa na mtoto wa kigogo akishirikiana na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

Dk. Migiro ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria, na pia Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano ya Nje wa CCM, tayari ameanza kuzungushwa mikoani ili kumjengea uwezo na uzoefu wa kisiasa.

Miongoni mwa wana CCM wanaotajwa kuutaka urais 2015 mbali na Lowassa na Membe, ni Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano), Stephen Wasira, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

"Ukiwalinganisha Membe na Lowassa kwa nguvu na umaarufu ndani ya CCM, hata vigogo wengine wanaotajwa kuutaka urais, utaona hakuna wa kumshinda Lowassa, sasa ndani ya chama wameamua kumchezea rafu.

"Kwa vile ana mtandao mrefu ndani ya CCM, wanafahamu wakikata jina lake itakuwa balaa, hivyo wameona waibuke na hoja ya zamu ya wanawake kama walivyomzima Samuel Sitta asigombee uspika wakampa Anne Makinda," alisema mtoa habari wetu.

Chanzo hicho kinaongeza kuwa mlengwa ni mtoto wa kigogo ambaye anaendesha mkakati wa kumchafua Lowassa ili 2025 ndiye awe mgombea urais baada ya Dk. Migiro kumaliza uongozi wake endapo atachaguliwa kwa vipindi viwili.

Pamoja na mkakati huo, kundi la Membe limeshauriwa kuendelea na harakati za kujiimarisha ili kuhadaa makundi mengine ndani ya chama yaamini kwamba naye ni miongoni mwa watakaochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais.

Hata hivyo, wakati CCM ikiendesha mkakati huo dhidi ya Dk. Migiro ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, baadhi ya wasomi wamemchambua mwanamama huyo wakisema hana uwezo huo.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alisema kuwa Dk. Migiro haonekani kubadilika licha ya kuwa na elimu kubwa.

"Nilimtembelea ofisini kwake akiwa UN kama Naibu Katibu Mkuu, nilikuwa na kazi za kitaifa kabisa kwa masuala yaliyoshirikisha mabalozi wa Ulaya, lakini aliponiona aliniuliza kwanini sitaki kurejea CCM.

"Huyu hawezi hata kubaini hapa tunazungumzia masuala ya kitaifa au kimataifa, yeye akili yake inawaza CCM tu kila wakati, hajaonyesha kutofautisha u-CCM wake na taaluma ili aweze kusaidia katika nyanja za kitaifa na kimataifa," alisema.

Dk. Slaa aliongeza kuwa aliposikia kuwa Dk. Migiro ndiye aliyeandaa rasimu ya kwanza na ya pili ya katiba kwa upande CCM ambazo zinaleta shida kwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba zikikinzana na rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, amedhihirisha kabisa udhaifu wake.

"Ukiangalia rekodi zake akiwa UN, huwezi ukaona matokeo yoyote, ndiyo maana Ban Ki moon hakutaka tena asaini mkataba kwa awamu nyingine kwani hakuwa na msaada kwake," alisema Dk. Slaa.

Dk. Azavery Lwaitama ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bukoba ambaye alisema kuwa Dk. Migiro sio mtu mwenye umaarufu wowote ambao unaweza kumfanya amweke katika orodha ya watu wanaoweza kuwa viongozi wa nchi hii.

"Aliteuliwa kuwa Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, akafanya kazi kipindi kifupi na baadaye akafanywa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa awamu ya Rais Kikwete.

"Kutokana na kunong'onezana kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon na Rais Kikwete, Dk. Migiro aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na baadaye kwa utaratibu huo huo wa kunong'onezana akarejeshwa tena nchini," alisema.

Dk. Lwaitama aliongeza kuwa vyombo vya habari vya nje viliandika vizuri kuhusu uwezo wa Dk. Migiro wakati akiwa Umoja wa Mataifa, lakini Watanzania hawakujishughulisha kuangalia yaliyoandikwa.

"Nilitarajia kuwa yeye atakuwa na mawazo tofauti katika mjadala wa rasimu iliyopo bungeni, lakini amerudi kwa wana CCM wenzake, anafikiri kama wao, analeta ushabiki wa makundi ya kisiasa, kwa utaratibu huo hawezi kuwa kiongozi anayefaa," alisema.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ambaye ni mwanafunzi wa Dk. Migiro, alisema haoni dalili au uwezo wowote wa yeye kuwa kiongozi katika wadhifa huo mkubwa wa urais.

"Huyu hajawahi kushiriki uchaguzi wowote akashinda, ukiwemo hata ubunge, isipokuwa nafasi za kuteuliwa ambazo hupewa na marais.

"Angalia kwa mfano katika Bunge hili la katiba ametoa mchango gani wa kukumbukwa na wananchi licha ya kuchangia na kubaki katika Bunge linalotoa matusi na kuacha kujadili rasimu?" alisema Lissu.

RAIS KIKWETE AONGOZA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MUUNGANO

CCM WILAYA YA TABORA MJINI WAADHIMISHA MIAKA 50 YA MUUNGANO KWA VITENDO!!!

Mjumbe wa kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tabora Bw.Emmanuel Mwakasaka akibeba udongo kwa ajili ya kuwasogezea mafundi katika ujenzi wa ofisi za chama hicho kata ya Kitete ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.
Baadhi ya viongozi wa CCM wilaya ya Tabora ambao walishiriki shughuli za ujenzi wa ofisi za CCM kata ya Kitete
Katibu wa siasa na uenezi wa CCM wilaya ya Tabora mjini Bw.Rashid Ramadhani au maarufu Kamanda Tolu

DIWANI LUZILA ASHIRIKIANA NA WANANCHI WA KATA YAKE KUCHIMBA MITARO KWA AJILI YA HUDUMA YA MAJI SAFI


Diwani wa Kata ya Tambukareli Bw.Salumu Luzila akishirikiana na wananchi wa kata hiyo mtaa wa Nkonkole kuchimba mtaro wa kuweka bomba la maji safi kwa ajili ya wananchi wa eneo hilo ambapo Mamlaka ya Maji Safi Tabora mjini wamelazimika kuweka huduma hiyo ya maji kwa wakazi hao.