Sunday, April 27, 2014

UKAWA WAMJIBU RAIS KIKWETE


ukawa5 eeb08
Na Hudugu Ng'amilo
SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) warudi bungeni akidai hawana sababu ya kwenda kushitaki kwa wananchi kwa sababu watawacheka na kuwasikitikia, umoja huo umemjibu wakisema wapo tayari kuchekwa.

Akihutubia vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi, siku moja kabla ya sherehe za miaka 50 ya muungano, Rais Kikwete alisema kuwa huko nje wanakotaka kwenda UKAWA siko na siku yake sio sasa, hivyo akawaomba wasipoteze fursa hiyo muhimu ya kutoa mawazo yao bungeni ili yafanyiwe kazi.

Alisema wananchi hawahusiki wala hawana namna ya kuwasaidia kwani mengi ya hayo yanayowakasirisha ni matatizo waliyoyazusha wao.

Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, aliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa
kama Kikwete anafikiri kwamba watarudi bungeni kwenye mijadala ya dharau, ubaguzi na matusi inayofanywa na wajumbe wa CCM, basi hajui chimbuko la tatizo.

"Kadiri anavyoendelea kuliacha Bunge liendelee na mijadala ya kibaguzi na matusi, taifa linazidi kupasuka na washauri wake hawamwelezi tatizo hilo," alisema.

Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema kuwa Rais Kikwete asipokuwa makini atalitumbukiza taifa kwenye machafuko ingawa yeye anafanya utani kwa kuipasua nchi na kushangilia kauli za kibaguzi, kejeli na matusi zinazotolewa na baadhi ya wajumbe wa CCM.

"Rais na wasaidizi wake inaelekea hawajasikiliza hata kauli zinazotolewa na viongozi wa dini kuhusu rasimu ya Warioba, atuache twende kwa wananchi, wao ndio wataamua. Tumevumilia kwa kiwango fulani, lakini itafika mahali uvumilivu utaisha, kwani hatuwezi kuendelea kuzuiliwa kufanya mikutano na jeshi la polisi wakati mikutano ya CCM inafanyika kote nchini kutuchafua," alisema Mbowe.
 

No comments:

Post a Comment