KASI ya uharibifu wa mazingira katika mkoa wa TABORA
imeelezwa kuwa ni kubwa mno kutokana na
kukithiri kwa shughuli mbalimbali za kijamii zisizozingatia kanuni za utunzaji mazingira
katika manispaa ya Tabora na maeneo mengineyo.
Hayo yameelezwa na meneja miradi wa taasisi ya MSEA
(Mwanza Sustainable Environment Association) kanda ya Magharibi Bw. Stan Fusi alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari mjini Tabora.
Alisema kuwa hali hiyo inatokana na wananchi walio
wengi kutokuwa na elimu ya utunzaji wa mazingira katika maeneo yao na kutoelewa
matumizi bora na uhifadhi wa maeneo yanayowazunguka.
Aidha alisema taasisi yake kwa kushirikiana na
serikali ya mkoa wa TABORA wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira kwa
kuwawezesha kushiriki zoezi la upandaji
miti kupitia mradi wa miombo.
Akifafanua zaidi alisema elimu hiyo imelenga
kuwasaidia wananchi kuzalisha mazao ya ‘timbau’ ambayo yanatokana na misitu
zikiwemo mbao, magogo na mazao mengine yasiyo ‘timbau’ mfano ufugaji nyuki na
kilimo cha mseto bila kuathiri mazingira katika maeneo hayo.
Meneja huyo alibainisha kuwa jitihada za kutoa elimu
hiyo mpaka sasa zimefikia kaya 12,500 kwa wilaya nne za mkoa wa TABORA lengo likiwa kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira
kuanzia maeneo yanayowazunguka hadi katika misitu.
Alizitaja wilaya hizo kuwa ni Urambo,Tabora
Manispaa, Uyui na Sikonge ambapo aliwaasa wananchi wake kuzingatia elimu
wanayoipata kwa kuepuka athari za uharibufu wa mazingira
Akizungumzia shughuli zinazochangia uharibifu wa
mazingira Fusi alisema ni ukataji miti ovyo na uchomaji misitu na mkaa unaofanywa
na wakulima na wafugaji kwa ajili ya kilimo na maeneo ya kulishia mifugo yao
pamoja na uchimbaji holela mchanga wa kufyatulia tofali.
Hivyo akaasa wakulima na wafugaji hao kufuata kanuni,
taratibu na ushauri unaotolewa na maofisa kilimo na mifugo na wadau wengineo
ili shuguli hizo zisiendelee kuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira
badala ya kuboresha mazingira hayo.
Aidha aliwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea
kuunga mkono jitihada zinazofanywa na uongozi wa serikali ya mkoa zikiongozwa
na mkuu wa mkoa huo Fatma Mwassa, Katibu
Tawala Kudra Mwinyimvua na wadau wengine ili kuboresha mazingira ya mkoa huo.
Aliongeza kuwa pamoja na elimu inayoendelea kutolewa
na serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wa misitu ikiwemo MSEA bado wananchi
walio wengi hawana mwamko wa kutosha wa kusimamia miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment