Na Hudugu Ng'amilo
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimepanga mkakati mpya wa kuengua wataka urais
wanaume kwa kuingiza hisia za kijinsia kama walivyofanya kumdhibiti
aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, alipotaka kugombea tena
nafasi hiyo mwaka 2010.
Wachunguzi
wa masuala ya kisiasa wameliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa mkakati
huo unalenga zaidi kumng'oa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ambaye
anaonekana tishio kwa wenzake wanaotajwa kutaka urais.
Kwa
mkakati huo, kundi la wana CCM walio karibu na Rais Jakaya Kikwete,
wameanza kuzungumzia jinsi ya kumpitisha Dk. Asha-Rose Migiro agombee
urais katika uchaguzi mkuu ujao 2015.
Kisingizio wanachotumia katika kampeni yao ya siri, ni kusaka kura za wanawake.
Katika
mkakati huo, wanamwandaa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, kuwa
Waziri Mkuu. Tayari Membe ameshatangaza kuwa hatagombea ubunge mwaka
2015.
Kwa
mujibu wa vyanzo vyetu, Membe ndiye alikuwa akipigiwa chapuo zaidi
miongoni mwa makada wa CCM ili kurithi mikoba ya Rais Kikwete, lakini
kutokana na uhusiano wa kifamilia uliopo baina ya wawili hao, sasa
ameshawishiwa kuwa atakuwa waziri mkuu endapo Dk. Migiro atashinda.
Wiki
hii, gazeti dada la Tanzania Daima Jumatano liliripoti mkakati wa
kumzima Lowassa asigombee urais, ambao unaendeshwa na mtoto wa kigogo
akishirikiana na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Dk.
Migiro ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria, na pia Mkurugenzi
wa Idara ya Mahusiano ya Nje wa CCM, tayari ameanza kuzungushwa mikoani
ili kumjengea uwezo na uzoefu wa kisiasa.
Miongoni
mwa wana CCM wanaotajwa kuutaka urais 2015 mbali na Lowassa na Membe,
ni Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Mahusiano), Stephen Wasira, William Ngeleja na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
"Ukiwalinganisha
Membe na Lowassa kwa nguvu na umaarufu ndani ya CCM, hata vigogo
wengine wanaotajwa kuutaka urais, utaona hakuna wa kumshinda Lowassa,
sasa ndani ya chama wameamua kumchezea rafu.
"Kwa
vile ana mtandao mrefu ndani ya CCM, wanafahamu wakikata jina lake
itakuwa balaa, hivyo wameona waibuke na hoja ya zamu ya wanawake kama
walivyomzima Samuel Sitta asigombee uspika wakampa Anne Makinda,"
alisema mtoa habari wetu.
Chanzo
hicho kinaongeza kuwa mlengwa ni mtoto wa kigogo ambaye anaendesha
mkakati wa kumchafua Lowassa ili 2025 ndiye awe mgombea urais baada ya
Dk. Migiro kumaliza uongozi wake endapo atachaguliwa kwa vipindi viwili.
Pamoja
na mkakati huo, kundi la Membe limeshauriwa kuendelea na harakati za
kujiimarisha ili kuhadaa makundi mengine ndani ya chama yaamini kwamba
naye ni miongoni mwa watakaochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania
urais.
Hata
hivyo, wakati CCM ikiendesha mkakati huo dhidi ya Dk. Migiro ambaye
amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, baadhi ya wasomi wamemchambua mwanamama huyo wakisema hana
uwezo huo.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod
Slaa, alisema kuwa Dk. Migiro haonekani kubadilika licha ya kuwa na
elimu kubwa.
"Nilimtembelea
ofisini kwake akiwa UN kama Naibu Katibu Mkuu, nilikuwa na kazi za
kitaifa kabisa kwa masuala yaliyoshirikisha mabalozi wa Ulaya, lakini
aliponiona aliniuliza kwanini sitaki kurejea CCM.
"Huyu
hawezi hata kubaini hapa tunazungumzia masuala ya kitaifa au kimataifa,
yeye akili yake inawaza CCM tu kila wakati, hajaonyesha kutofautisha
u-CCM wake na taaluma ili aweze kusaidia katika nyanja za kitaifa na
kimataifa," alisema.
Dk.
Slaa aliongeza kuwa aliposikia kuwa Dk. Migiro ndiye aliyeandaa rasimu
ya kwanza na ya pili ya katiba kwa upande CCM ambazo zinaleta shida kwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba zikikinzana na rasimu ya Tume ya Jaji
Warioba, amedhihirisha kabisa udhaifu wake.
"Ukiangalia
rekodi zake akiwa UN, huwezi ukaona matokeo yoyote, ndiyo maana Ban Ki
moon hakutaka tena asaini mkataba kwa awamu nyingine kwani hakuwa na
msaada kwake," alisema Dk. Slaa.
Dk.
Azavery Lwaitama ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bukoba ambaye alisema
kuwa Dk. Migiro sio mtu mwenye umaarufu wowote ambao unaweza kumfanya
amweke katika orodha ya watu wanaoweza kuwa viongozi wa nchi hii.
"Aliteuliwa
kuwa Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, akafanya kazi kipindi kifupi na
baadaye akafanywa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wakati wa awamu ya Rais
Kikwete.
"Kutokana
na kunong'onezana kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon
na Rais Kikwete, Dk. Migiro aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa na baadaye kwa utaratibu huo huo wa kunong'onezana
akarejeshwa tena nchini," alisema.
Dk.
Lwaitama aliongeza kuwa vyombo vya habari vya nje viliandika vizuri
kuhusu uwezo wa Dk. Migiro wakati akiwa Umoja wa Mataifa, lakini
Watanzania hawakujishughulisha kuangalia yaliyoandikwa.
"Nilitarajia
kuwa yeye atakuwa na mawazo tofauti katika mjadala wa rasimu iliyopo
bungeni, lakini amerudi kwa wana CCM wenzake, anafikiri kama wao,
analeta ushabiki wa makundi ya kisiasa, kwa utaratibu huo hawezi kuwa
kiongozi anayefaa," alisema.
Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) ambaye ni mwanafunzi wa Dk.
Migiro, alisema haoni dalili au uwezo wowote wa yeye kuwa kiongozi
katika wadhifa huo mkubwa wa urais.
"Huyu hajawahi kushiriki uchaguzi wowote akashinda, ukiwemo hata ubunge, isipokuwa nafasi za kuteuliwa ambazo hupewa na marais.
No comments:
Post a Comment