Na Lucas Raphael,Tabora
Tatizo
la kuongezeka kwa umaskini kwa wananchi wa wilaya ya URAMBO mkoani TABORA
linatokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula na ulipaji wa madeni
ya mikopo ya pembejeo kwa ajili ya kilimo cha zao la tumbaku.
Wakizungumza
katika mkutano wa juu ya uelewa wa Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza
umaskini (MKUKUTA), wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali wilayani
URAMBO wamesema mikopo ya pembejeo na kutowajibika ipasavyo kwa wananchi katika
kilimo cha mazao ya chakula ni chanzo kikubwa cha kuendelea kuwepo kwa umaskini
wilayani humo.
Wamesema
licha ya wilaya ya URAMBO kuongoza nchini kwa kilimo cha tumbaku, lakini
wananchi wake wanaendelea kuwa maskini kwa sababu fedha wanazopata zinalipa
madeni ya pembejeo na fedha zinazobaki kununulia chakula.
Wameshauri
kwamba ili kuondoa umaskini, wananchi wanapaswa kuwajibika katika kulima mazao
ya chakula kukidhi mahitaji ya kaya zao na pia kutumia mapato ya tumbaku kwa
mahitaji mengine muhimu ya kijamii kwa vile afya, elimu kwa watotona ujenzi wa
nyumba bora badala ya kununulia chakula.
Katika
mkutano huo wa siku mbili ulioandaliwa na Shirika la JIDA la mjini TABORA
kwa ufadhili ya Shirika la Foundation for Civil Society (FCS) la jijini
Dar es salaam , washiriki pia walielimishwa juu ya umuhimu wa matumizi ya
mfumo wa kuhifadhi takwimu katika kupambana na umaskini.
JIDA
ni shirika lisilo la kiserikali mkoani TABORA linalohamasisha maendeleo ya watu
kwa kupambana na vikwazo vya maendeleo na kutoka huduma endelevu za jamii kwa
makundi yaliyo katika hatari ya kupata madhara zaidi.
No comments:
Post a Comment