Vilio na simanzi vilitanda Jumatano iliyopita Mwananyamala Kisiwani, jijini Dar kufuatia mtoto wa mwaka mmoja, Rahim Rajab kufariki dunia kwa kuangukiwa na watu watatu, akiwemo baba yake mzazi, Rajab Said..
Tukio la watu hao kumwangukia mtoto huyo
lilitokea Jumatatu iliyopita na lilisababishwa na ugomvi mkubwa wa CD
yenye nyimbo za mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’
ulioibuka ndani ya chumba cha kulala kati ya mama wa marehemu na
mpangaji mwenzake aitwaye Aisha.
Akizungumza kwa machungu kuelezea tukio
hilo, mama mzazi wa marehemu Rahim, Habiba Ally alikiri kuwa kisa cha
kifo cha mwanaye ni CD tu.Akasema:
" Kwa kweli hakuna kingine zaidi ya CD, naamini hivyo kwa kuwa mimi sikuwa na ugomvi wowote na Aisha. Tulikuwa tunaishi kawaida tu ukiacha mikwaruzo ya hapa na pale.”
Akaongeza: Jumamosi iliyopita, Aisha alikuja ndani kwangu na CD zake tatu, ya Diamond, Kingwendu na ya Coast Modern Taarab. Alipomaliza kuangalia aliziacha, akaondoka zake.
“Jumapili mimi nikaenda nazo kwa mama zote tatu kwa ajili ya kuziangalia, tulipomaliza na mimi niliziacha huko.“Jumatatu usiku Aisha akaja kunidai, nikamwambia zipo kwa mama. Kwa kuwa anapajua anapoishi mama, si mbali akaenda kuzichukua zote tatu.
Ajabu aliporudi tu, akaja tena kwangu na
kusema hajapewa CD ya Diamond kitu ambacho si kweli na ndipo ulipozuka
ugomvi wote huo hadi kusababisha kifo cha mwanangu.”
Akizungumza msibani juzi, bibi wa
marehemu, Jamima Hassan alisema siku ya tukio alipigiwa simu na mkwe
wake (baba wa marehemu) akamwambia kuna ugomvi nyumbani kwake unaohusu
CD kati ya mkewe na mpangaji mwenzake ambapo bibi huyo aliamua kwenda
kutatua ugomvi huo.
“Niliondoka muda huohuo kwani huyo Aisha alitoka kwangu kuchukua CD zake muda mfupi tu, sasa nilijiuliza ni CD gani wanazogombania?
“Nilipofika nilikuta ugomvi umepamba moto, baba wa mtoto na mume wa Aisha aitwaye Shaban Sangali walikuwa wameungana kumtoa nje ya chumba Aisha bila mafanikio.“Wakati naingia, Aisha alikuwa akitukana matusi mazito na tulipojitahidi kumtoa nje alitusukuma kwa nguvu. Ndipo yeye, mume wake na baba wa mtoto waliwaangukia watoto waliokuwa wamelala kitandani,” alisema bibi huyo.
Akaendelea: Tulipowaangalia watoto ambao
ni mapacha, hali zao zilikuwa mbaya, tukaamua kwenda kwa mjumbe wa mtaa
kuripoti, akatupa barua, tukaenda Kituo cha Polisi Mwinyijuma, pale
wakatupa PF3 ya kuwapeleka Hospitali ya Mwananyamala ambako walilazwa
kwa matibabu.
Bibi huyo alisema siku iliyofuata, Rahim
alifariki dunia, ikabidi waende Polisi Oysterbay ambapo walifungua
shitaka lenye faili kwa kumbukumbu No. OB/RB/1150/2013 MAUAJI.
Watuhumiwa katika RB hiyo ni Aisha na mumewe, Sangali ambao walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi.
Majirani waliozungumza na mwandishi wetu
walisema wakati ugomvi kati ya Aisha na Habiba unatookea, mume wa
Habiba alikuwa anarudi kutoka kazini, akakutana na kimbembe hicho.
Walisema aliingilia kati kuamua bila
mafanikio. Wakati huo mume wa Aisha alikuwa chumbani kwake na
amefungulia muziki wa redio kwa sauti ya juu hivyo hakujua nini
kinaendelea kwenye chumba cha mpangaji mwenzake.
Ikaelezwa kuwa, kuna watu walikwenda kumgongea na kumwambia mkewe anapigwa na mume wa Habiba kwa kushirikiana na mkewe.
Ilibidi mwanaume huyo atoke mbio hadi
chumbani kwenye ugomvi ambako alikuta baba wa marehemu akijitahidi
kuwaamulia wawili hao bila mafanikio.
Habari zinasema mwanaume huyo aliingilia
kati kuongeza nguvu lakini katika hali ya kuwalemea,Aisha aliwasukuma
wote na kisha wao kuwaangukia watoto hao mapacha waliokuwa wamelala
kwenye kitanda kimoja.
Katika hali ya kusikitisha, marehemu amemuacha pacha mwenzake aitwaye Rahima Rajab ambaye ni kulwa.
Wengi wanaamini kuwa maisha ya Rahima
yangekuwa ya furaha zaidi kama Rahimu angekuwepo na kwamba itamsononesha
sana akikua na kusikia mwenzake alifariki dunia kwa ugomvi wa mama yake
na mpangaji mwenzao kisa ni CD ya nyimbo za mwanamuziki.
No comments:
Post a Comment