Wednesday, January 14, 2015

SIKONGE WAMPONGEZA RAIS KIKWETE KWA JITIHADA ZAKE ZA KUPUNGUZA UMASKINI

 

Washiriki wa warsha ya kunusuru kaya maskini iliyoandaliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF wilayani sikonge mkoani Tabora,wa kwanza kulia na mbunge wa jimbo la Sikonge Juma Nkumba anayefuata ni kaimu mkurungezi wa Tasaf Peter lwanda na wa kati kati ni mkuu wa walaya ya Dikonge Hanifa Selengua. aliyakaa kulia kwa mkuu wa wilaya ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge na aliyevaa suti nyeusi ni Mkurungezi mtendaji wa wilaya ya Sikonge Shadrack Mhagama

HALMASHAURI ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora imempongeza Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa jitihada na dhamira yake ya dhati ya kupambana na umaskini hapa nchini kupitia mpango wa kuzinusuru na kuziwezesha kaya maskini kiuchumi.

Pongezi hizo zimetolewa juzi na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Robert Kamoga alipokuwa akihitimisha warsha ya kujenga uelewa wa wadau kuhusu mpango wa kunusuru kaya maskini unaoasisiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu.

Alisema uongozi wa Rais Jakaya Kikwete umeimarisha zaidi dhamira ya nchi kupunguza umaskini kupitia mikakati yake mbalimbali na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii ambazo ni pamoja na elimu, afya na maji kwa ushirikiano mkubwa na wananchi.

‘Nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhesh.Dr Jakaya Mrisho Kikwete kwa uongozi wake ambao umeonyesha dhamira ya dhati ya nchi hii kupunguza umaskini wa wananchi sambamba na kuboresha huduma za kijamii’, alisema Kamoga.

Alisema kitendo cha Rais Kikwete kuzindua Mpango maalumu wa Kunusuru Kaya Maskini mnamo tarehe 15 Agosti 2012 kule Dodoma na utekelezaji wake kuanza mara moja mwezi Februari 2013 kwa azma ya kufikia jumla ya halmashauri 161 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba kililenga kutokomeza na kundokana na umaskini katika kaya husika sambamba na utekelezaji wa miradi mingine kwa nia ya kuzipatia kaya maskini uwezo wa kujikimu.

Kamoga alibainisha kuwa madhumuni ya mpango huu wa awamu ya tatu ya TASAF ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji yao muhimu na familia zao mpango ambao utatekelezwa kwa awamu katika kipindi cha miaka 10. 

Aidha aliwakumbusha wanawarsha kuwa TASAF ni chombo cha serikali kilichopewa jukumu la kuwezesha kufikia azma ya serikali ya kupunguza umaskini kama ilivyoainishwa katika awamu ya pili ya MKUKUTA kwa kutumia dhana ya ushirikishwaji jamii.

Aliongeza kuwa tangu nchi yetu ipate uhuru miaka 50 iliyopita, serikali imekuwa ikipambana na maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga na maradhi lengo likiwa kumwondolea mwananchi kero na vikwazo mbalimbali vya kimaendeleo.

Kamoga alieleza kuwa serikali kwa kutambua kwamba umaskini bado ni mkubwa miongoni mwa jamii hasa kule vijijini, ndio maana imeandaa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini ili kufikia malengo yake iliyoazimia katika Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA ) awamu ya pili.

Awali akizungumza katika warsha hiyo Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw.Peter Luanda alisema mpango huo wa kunusuru kaya maskini umelenga kuzinufaisha kaya masikini zilizo katika hali duni kule vijijini na katika mitaa mbalimbali hususani watoto wenye umri chini ya miaka 5 na wanaosoma shule na akina mama wajawazito.

 Alisema kaya hizo zitanufaika kwa kupewa ruzuku za aina mbili moja ni ruzuku ya msingi itakayotolewa kwa kaya maskini iliyomo kwenye mpango huo na ruzuku ya pili walengwa ni wale wanaotakiwa kutimiza masharti ya elimu na afya ili waweze kupatiwa huduma za elimu na afya bure.

Akizungumza baada ya warsha hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya Sikonge Shadrack Mhagama alipongeza ujio wa mpango huo wa TASAF wa kunusuru kaya maskini na kuongeza kuwa utasaidia kuboresha maisha ya wananchi wake kwani wengi wao wamekuwa wakishindwa kuchangia hata shughuli za maendeleo kutokana na kuwa na hali duni.

No comments:

Post a Comment