Sunday, October 14, 2012

ITAMBUE HISTORIA YA SHULE YA TABORA WASICHANA


 KIBAO CHA KUINGIA SHULENI 

 KITABU CHA MAPOKEZI ENZI HIZO 
 WANAFUNZI WAKICHUTA MAJI
 MMOJA YA WAFANYAKAZI WA SHULE HII
 ENEO LA SHULE YA TABORA WASICHANA

Tabora
Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora (pichani juu) iko karibu na shule ya Tabora Boys, ni miongoni mwa shule kongwe, zilizosifika na bado inaendelea kusifika kwa kiwango cha elimu watoacho.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1928 kama shule ya msingi kwa wakati huo wa ukoloni, ilijulikana kwa jina la African Girls School. Shule hiyo yenye ukubwa wa hekta zaidi ya 97, ilianzishwa na wakoloni wa Kiingereza kwa madhumuni ya kutoa elimu kwa watoto wa kike wa machifu.

Mwaka 1957, shule ilipewa hadhi ya kuwa sekondari ya wasichana ambapo mwaka 1972 ilianza kusajili wanafunzi wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ulemavu wa ngozi (albino) na wasioona.

Kaulimbiu ya shule ni strive to excel yaani kazana ufanikiwe, huu ni ukweli unaobainishwa na uwepo wa wanataaluma waliobobea katika fani ya sheria, udaktari, uhandisi, ualimu na hata katika siasa waliosoma katika shule hiyo.

Miongoni mwa viongozi waliosoma katika shule hiyo ni pamoja na Mke wa Rais mstaafu na Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa sawa kwa Wote (EOTF), Mama Anna Mkapa, aliyewahi kuwa Rais wa Bunge la Afrika na Mbunge wa Ukerewe, Getrude Mongella.

Wengine ni aliye kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margareth Sitta na aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Batilda Buriani.

Pia aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Celina Kombani, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (UWT- Taifa) Anna Abdallah, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dk. Joyce Ndalichako.

Wamo pia Jaji mstaafu Julie Manning, Jaji wa Mahakama Kuu, Eusebia Munuo na aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Makazi Duniani (UN Habitat), ambaye sasa ni Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Nidhamu ya shule hiyo ni jambo ambalo linawasaidia wanafunzi wasomao shuleni hapo kuwafungulia milango ya mafanikio katika maisha yao.

No comments:

Post a Comment