Tuesday, October 23, 2012

KONGAMANO LA HAKI ZA WANAWAKE NA KATIBA LINAFANYIKA UKUMBI WA BLUE PEARL HOTEL JIJINI DAR ES SALAAM


KUTOKA KUSHOTO NI HALIMA SHARIF,RUTH MEENA  MWENYEKITI WA (WFT) MGENI RASMI LETICA MUKURASI NA BI. SHAMSAD REHLI (OSIEA) WAKIWA KATIKA MKUTANO HUO KABLA YA KUFUNGULIWA RASMI
BAADHI YA WASHIRIKI WKONGAMANO HILO WAKIFUATILIA KWA MAKINI MADA ZILIZOKUWA ZIKITOLEWA KATIKA KONGAMANO HILO.
…………………………………………..
Tangu 2011, Tanzania imekuwa ikiendesha mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba ya nchi katika jitihada za kutengeneza katiba mpya ifikapo 2015. Asasi ya Women Fund Tanzania (WFT) (au Mfuko wa Wanawake Tanzania), iliyojikita katika kutetea haki za wanawake nchini, ikishirikiana na wadau wengine walio katika harakati hizi, wameandaa mkutano wa siku tatu utakaojadili maswala muhimu ya wanawake katika katiba mpya. Mkutano huo utafanyika Oktoba 22 hadi 24, 2012, katika hoteli ya Blue Pearl Ubungo, Dar es Salaam.
 Washiriki wa mkutano huo wanatoka katika nyanja na mashirika mbali mbali nchini na wataibua na kujadili mapungufu yaliomo katika katiba ya sasa, na kutengeneza mikakati ya kuyashughulikia mapungufu haya. Wanaharakati wanawake na wakereketwa wa maswala ya haki za wanawake wanatarajiwa kwa pamoja kuainisha maswala muhimu ya wanawake yanayostahili utetezi ili yazingatiwe katika katiba mpya.
 Mkurugenzi wa WFT, Mary Rusimbi amesema: “Mkutano huu unatoa nafasi muhimu kwa wanawake kujadili kwa kina na kuimarisha uelewa wao juu ya maswala nyeti yanayogusa haki zao katika mchakato unaoendelea hivi sasa. Pia ni fursa kwa wanawake kujifunza mbinu zinazokubalika katika kujenga sauti moja na msimamo wa pamoja katika mchakato huu.”
 Asasi ya WFT na washirika wake wanaendeleza harakati hizi kutokana na umuhimu wa ushikishwaji wa wanawake katika maswala ya kikatiba na hasa katika nchi ambayo bado ina baadhi ya sheria i zinazomkandamiza mwanamke.
 Katiba ya sasa ya Tanzania ya mwaka 1977 inadai kutomkandamiza mwanamke kwa jinsi yake au jinsia, japokuwa kuna sheria kadhaa zinazotoa kipaumblele kwa taratibu za kimila, na hivyo kutozingatia haki za wanawake. Sheria hizi zinahusu maeneo mbalimbali kama vile ndoa, talaka, afya ya uzazi, elimu uongozi, siasa, na maswala ya kujikimu kimaisha.
 Wanawake 100 kutoka Tanzania bara na Zanzibar, wamealikwa kuhudhuria mkutano huo unaotarajiwa kutoa mpango kazi utakaoongoza harakati za kutetea haki za wanawake katika katiba mpya.
 Washiriki watatokea makundi mbalimbali yakiwemo yale ya kijamii, ya kibiashara, vyama vya wafanyakazi, taasisi za elimu ya juu, vyama vya kisiasa, mashirika ya kidini, vyombo vya habari, teknologia ya habari, asasi za mazingira, afya, utamaduni, na wafanyabiashara.

No comments:

Post a Comment