Monday, October 15, 2012

GIZA NENE MAUAJI YA RPC MWANZA


Na George Ramadhan


Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi akisaini kitabu cha maombolezo cha kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia juzi eneo la Kitangiri Jijini Mwanza jana.
Wakati  maswali magumu yakiendelea kuwatatiza wananchi wengi juu ya kisa hasa cha mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, jeshi hilo limesema linaamini kwa asilimia 100 kuwa litawatia mkononi wauaji waliohusika.

Hata hivyo, polisi wameamua kuchukua hadhari kali juu nini waseme na nini wasiseme ikiwa ni pamoja na kutokutaka kusema kama kweli kuna mali za RPC Barlow alizoporwa baada ya kuuawa zimekwisha kupatikana zikiwa mikononi mwa raia kama ambavyo uvumi umezaa jijini Mwanza.

Kamanda Barlow aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia juzi katika eneo la Kitangiri kwenye barabara ya kuelekea Bwiru alipokuwa amekwenda kumrejesha nyumbani kwake, mwanamke aliyejulikana kwa jina la Doroth Moses.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola, alisema msako dhidi ya wauaji unaendelea kila kona ya Jiji la Mwanza na vitongoji vyake na kwamba kuna matumaini makubwa ya kuwatia mbaroni.

“Kwa jinsi tulivyojipanga, tunayo imani kubwa wauaji watapatikana, tupeni muda kidogo tutawaita na kuwapeni taarifa tukishawatia mbaroni,” alisema Kamanda Matola.

Aliongeza kwamba kwa sasa maofisa wa polisi wanaendelea kukusanya taarifa kwa njia za kawaida na pia kupitia mtandao wa simu (cyber), hivyo hakuna mahali ambako wauaji hao wanaweza kukwepa mkono wa Jeshi hilo.

Kuhusu kuwapo kwa taarifa kwamba kuna watu wamekamatwa wakiwa na baadhi ya vitu alivyokuwa navyo Kamanda Barlow kabla ya kuuawa, Matola alisema kwamba ni mapema sana kuzungumzia taarifa hizo, lakini wakati muafaka ukifika taarifa rasmi zitatolewa.

KUAGWA LEO NYAMAGANA


Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, leo anatarajiwa kuongoza wakazi wa mkoa wa Mwanza na mikoa jirani kuuaga mwili wa Barlow.

Matola alisema jana kuwa zoezi la kuuaga mwili wa Barlow linatarajiwa kufanyika leo kwenye uwanja wa Nyamagana kuanzia saa 2:30 asubuhi na kisha jioni marehemu atapelekwa uwanja wa ndege wa Mwanza kupelekwa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Matola, mwili wa Kamanda Barlow utafikishiwa nyumbani kwake Ukonga Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa fursa kwa ndugu, jamaa na marafiki kumuaga kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.

Makamanda wa Polisi kutoka mikoa jirani ya Mara, Kagera, Shinyanga, Geita, Simiyu na Kanda Maalum ya Tarime na Rorya ni miongoni mwa wanaotarajiwa kutoa salaam za rambirambi wakati wa kuuaga mwili wa Kamanda Barlow.

NCHIMBI: TUTAWASAKA KWA NGUVU ZOTE


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema majambazi waliomuua Barlow wataswakwa kwa nguvu zote za dola.

Alionya kuwa majambazi wanaoua raia kwamba serikali itapambana nao kikamilifu.

“Polisi ni walinzi wa raia na mali zao, wanapotokea watu wanaoua kingozi wa polisi inaleta hofu kwa wananchi, hivyo serikali itapambana nao kikamilifu,” alisema Dk. Nchimbi, jijini Mwanza jana.

LUKUVI: NI UKATILI USIOVUMILIKA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi, ambaye jana alifika katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza kusaini kitabu cha maombolezo, alizungumzia mauaji ya Kamanda Barlow na kusema ni ukatili ambao serikali haiwezi kuuvumilia.

“Ni kifo cha ajabu, kimemshtua kila mtu, huu ni ukatili usiovumilika, lazima wahusika wasakwe na kutiwa mbaroni. Kama watu wanadiriki kumuua kiongozi wa polisi hii ni hatari sana sijui itakuwaje kwa raia wa kawaida,” alisema Lukuvi.

Alitoa wito kwa wakazi wa Mwanza kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha wahusika wa mauaji hayo wanatiwa mbaroni kwa sababu lazima watakuwa wanafahamika.

“Wauaji hawakushuka kutoka kusikojulikana, wasingeweza kutekeleza mauaji hayo bila wananchi kujua chochote, jambo la msingi hapa ni kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa ambazo zitasaisia wahusika kutiwa mbaroni,” alisema.

Mbali na Waziri Lukuvi, kiongozi mwingine aliyefika kusaini kitabu cha maombolezo ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha-Rose Migiro ambaye pia alifika nyumbani kwa marehemu kuwafariji wafiwa.

MANUMBA AVUTA PUMZI

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba, ambaye alifika jijini hapa juzi kuongeza nguvu ya upelelezi wa mauaji hayo, alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote, lakini wakati utakapofika atasema.

“Kwa sasa siwezi kusema chochote tunaendelea na kazi ya upelelezi wakati ukifika nitazungumza kwa hiyo tuendelee kuvuta subira,” alisema Manumba.

TAARIFA YA MAZISHI

Mwili wa Barlow, unatarajiwa kuzikwa keshokutwa mkoani Kilimanjaro.

Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Jeshi la Polisi makao Makuu, Advera Senso ilisema: “Kamati ya mazishi kwa niaba ya Inspekta Jenerali wa Polisi, inapenda kuwataarifu wananchi wote kuwa mwili wa Kamanda Barlow utaagwa jijini Mwanza kesho (leo).”

Advera alisema kuwa leo jioni mwili huo unatarajiwa kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, na utawekwa nyumbani kwake Ukonga na kesho utaagwa nyumbani kwake kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani Kilimanjaro na kwamba mwili huo utazikwa mkoani humo Jumatano.

Advera aliongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu maziko hayo zitaendelea kutolewa.

CHADEMA YATOA POLE


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa
masikitiko na kinalaani mauaji ya Kamanda Barlow.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa Chadema kinatoa pole kwa familia ya marehemu, Jeshi la Polisi na wote walioguswa na msiba huo.

“Chadema kinafuatilia taarifa zinazoendelea kutolewa kuhusu utata wa chanzo cha kifo cha Barlow, hivyo kwa kuzingatia mazingira hayo badala ya Jeshi la Polisi kutegemewa pekee katika kuchunguza chanzo cha kifo cha kamanda wao, ni muhimu uchunguzi huru ukafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania.

Chadema kinaitaka Serikali kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria hiyo ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa wa Habari wa Chadema, Tumaini Makene.

“Ikumbukwe pia kwamba matukio ya mauaji ya raia katika mikoa ya  Mbeya, Mara, Arusha, Ruvuma  na mikoa mingine nchini yameelezwa kwa kina na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Taifa na wasemaji wengine wa kambi rasmi ya upinzani  inayoongozwa na Chadema wakati wa mkutano wa nne wa Bunge mwaka 2011 na Mkutano wa nane wa Bunge mwaka 2012 bila ya hatua kuchukuliwa.”

Makene alisema Chadema kinatoa wito kwa Rais Jakaya Kikwete kwa niaba ya Serikali na CCM kwa upande mwingine kutumia msiba huu kutafakari na kuchukua hatua endelevu za kushughulikia mauaji hayo na mengine ya raia ili kulinda ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya msingi wa raia wote.

Hata hivyo, kifo cha Barlow kimetokea siku moja tu baada ya kutoa kauli ya kutatanisha juu ya tukio la polisi kummiminia risasi Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mwanza, Albert Buchafwe, kwamba aliingia katika mtego wao na kwamba ilikuwa auawe kwa kupigwa risasi.

Akizungumza na NIPASHE alhamisi iliyopita Barlow alisema kuwa:" Ni kweli kuna tukio kama hilo, lakini yalikuwa ni mashambulizi ya gizani kwa sababu askari walimfananisha ofisa uhamiaji na jamabzi waliyekuwa wamemuwekea mtego, nadhani ana bahati kwanindiyo akwaida yetu hutubembelezani na majambazi."

Pamoja na kauli hiyo kamanda huyo hakueleza kwa jinsi gani ofisa huyo haliingia katika mtego huo kwani hakuwa katika tukio la uporaji.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment