Sunday, October 21, 2012

HOFU YA UCHOMAJI MAKANISA YATANDA WILAYANI UYUI -TABORA.


Na Hastin Liumba,Uyui
 
HOFU ya uchomaji makanisa, imetanda katika wilaya ya Uyui,mkoani
Tabora,kufuatia baadhi ya wananchi wa kata za Igalula na Goweko, kudai
kuna kikundi cha watu zaidi ya 20 wanakaa vikao nyakati za usiku
kupanga hujuma hiyo.

Chanzo kimoja cha taarifa toka kwa baadhi ya raia wema katika kata za
Igalula na Goweko,kimesema kuna kundi moja linalokaa vikao vyake hasa
nyakati za usiku wa saa tano, na kupanga njama hizo.

Wakizungumza na mwandishi wetu  kwa sharti la kutotajwa majina yao baadhi
ya wananchi walisema kundi hilo limekuwa likiketi vikao vyake katika
kata za Goweko na Igalula kupanga jinsi watakavyoteketeza makanisa
yaliyopo.

“Tumebaini njama hizo na majina ya wahusika tunayo tukifanikiwa hata
kuitwa na kuzungumza na vyombo vya usalama tutawataja ila iwe siri
maana kundi hilo limekuwa likishirikiana na waharifu mara
kadhaa.”walisema wananchi hao.

Aidha walisema kuwa njama hizo wameanza  kuziratibu na kuzipanga ndani
ya siku mbili ambapo wamenza toka juzi, majira ya saa tano na
kuendelea huku wengine wakiwa kata ya Goweko na wengine wakiwa kata ya
Igalula.

Wameongeza kuwa taarifa hizo zimevuja mapema baada ya mmoja kati ya
watu wanaotaka kuchoma makanisa kuvuruga plani hiyo kwa kutoa taarifa
kwa baadhi ya wananchi na uongozi wa kata.

Walisema licha ya kutoa taarifa hizo bado uongozi wa kata haujachukua
hatua za haraka kudhibiti hali hiyo ambayo imeanza kutengeneza chuki
kwani tayari waumini wa upande wa pili nao umejipnga kulipa kisasi
endapo uongozi wa wilaya na kata hautachukua hatua za kudhibiti kundi
hilo.

Walisema kundi hilo limekuwa likichangishana fedha kuweza kufanikisha
kazi hiyo ambayo wamepanga kutekeleza kipndi hiki cha mwezi huu.

Aidha wananchi hao wameongeza kuwa kundi hilo limedaiwa kumuunga mkono
Sheikh Ponda,ambaye ameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za uchochezi,
na kwamba wamekuwa wakiita wao ni zaidi ya dola wakijiita “Al-Shabab”.

Wananchi hao walipoulizwa ni vipi fedha wanazochangisha,wananchi hao
walisema wamegundua kuna mtandao mkubwa unaratibu zoezi hilo.

Wananchi hao walikwenda mbali zaidi kwa kuwataja kwa majina ambayo kwa
sasa yanahifadhiwa ambapo kundi hilo lina watu zaidi ya 20.

Aidha wananchi hao wamesema wanatarajia kufikisha taarifa hizo mbele
ya vyombo vya dola,huku mtendaji wa kata,Aloyce Shija, akiwa ameshapewa
taarifa.
 
Mwandishi wetu  alimtafuta diwani wa kata ya Igalula,Suleiman Kapalu na
diwani wa Goweko Ali Kawaka hawakupatikana katika kata zao ambapo
taarifa zinasema wako mjini Tabora ambapo simu zao hazikupatikana kila
zilipopigwa.

No comments:

Post a Comment