Thursday, October 25, 2012

MAGGID MJENGWA NA NENO LA LEO :AFRIKA HATUGOMBANI MATABIMBIKO

 

Ndugu zangu, 
Kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto, yaweza kuwa ni kazi ngumu sana. 
Ona, moto ulioanza kwenye nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka na hata kuteketeza kijiji kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa hatari ya kucheza na moto. Naam, binadamu usicheze na moto, labda iwe kwenye mazingaombwe.

Sisi sote ni ndugu, na hii ni Nchi Yetu. Hatuna haja ya kubaguana kwa misingi ya ukabila, dini na rangi. Tuna historia ya kujivunia. Ni historia yetu wenyewe. Kinyume na baadhi yetu wanavyofikiri au wanavyotutaka tufikiri, historia yetu haikuanzia enzi za Mwarabu , Mjerumani au Mwingereza. Historia yetu haikuanzia enzi za TANU wala Afro Shiraz. 

Na dini hizi za kimapokeo zinazotufanya sasa tufarakane zimekuja na kuzikuta dini zetu za asili, na bado tunazo. Na hakika, Afrika hatugombanii matambiko. Afrika kila ukoo una tambiko lake, hivyo basi, dini yake. Kamwe hutasikia Waafrika wanagombania matambiko. Hutasikia Waafrika wakigombana kwa tofauti za matambiko yao.

 Na sisi ni Waafrika. Hii leo mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na hata kufanikiwa kuwafanya wachinjane ni kwenye kwenye tofauti zao za imani hizi za kimapokeo; Uislamu na Ukristo.

 Naam, tusifike mahali tukagombana kutokana na tofauti za imani ama dini ambazo wala si za asili yetu. Imani au dini ambazo, kama ilivyo dini zetu za asili, nazo zinatutaka wanadamu tuishi kwa amani, upendo na maelewano. 

Na hilo ndilo Neno la leo.
 Maggid Mjengwa, 
Iringa. 
 0788 111 765, 0754 678 252
http://mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment