Tuesday, October 16, 2012

MWILI WA MAREHEMU RPC BARLOW KUAGWA JIJINI DAR-ES-SALAAM


Na Tamimu Adam- Jeshi la Polisi


Mwili wa aliyekuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Marehemu Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Barlow (52) ambaye alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, utaagwa Jumanne saa tano asubuhi katika kanisa la Katoliki lililoko Ukonga, jijini Dar es salaam.

 Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kamati ya maandalizi ya mazishi na kuthibitishwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Advera Senso, Mwili Marehemu utawasili siku ya Jumatatu jioni ukitokea mwanza.

 Siku ya Jumanne mwili wa marehemu utafikishwa nyumbani kwake Ukonga kabla ya kupelekwa katika kanisa la Katoliki Ukonga kwa shughuli za ibada na kutoa heshima za mwisho.

Aliendelea kusema kuwa viongozi mbalimbali wa Serikali, Maofisa wa waandamizi wa Polisi, Askari na wananchi watatoa heshima zao za mwisho  katika kanisa la hilo.

 Aliongeza kuwa baada ya ibada na shughuli ya kuaga kukamilika, mwili wa marehemu utasafilishwa kuelekea nyumbani kwao kilema, Moshi vijijini Mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika siku ya Jumatano mchana kwa taratibu zote za kidini na baadae kuhitimishwa kwa kufuata taratibu za kijeshi.

Marehemu kamanda Barlow alizaliwa katika kijiji cha Kyou Wilaya ya Moshi vijijini, Mkoani Kilimanjaro mwaka 1960, baada ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 1974 katika shule ya msingi Lombetha, alijiunga na elimu ya sekondari katika shule ya Maua Seminary na baadae kujiunga kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondary Milambo na kuhitimu mwaka 1981.
 
 Baaada ya kumaliza elimu ya sekondari, marehemu kamanda Barlow alilitumikia taifa katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Operesheni Imarisha katika kikosi cha Mafinga  JKT, Mkoani Iringa.

Mwaka 1982, Marehemu alijiunga na Chuo cha mafunzo cha Polisi Moshi (CCP) kwa ajili ya kusomea mafunzo ya awali ya sheria ya Uhamiaji na baadae kupangiwa kufanya kazi mpakani mkoani Mtwara akiwa kama Mkuu wa kituo cha Uhamiaji.

Marehemu kamanda Barlow aliajiriwa  na Jeshi la Polisi baada ya kumaliza shahada ya kwanza ya utawala  kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam  kwa kuomba kazi katika Idara ya Polisi mwaka 1987 katika ngazi ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi.

Kutokana na uadilifu wake katika kazi, Marehemu aliweza kuaminiwa na viongozi wake na kupandishwa vyeo mbalimbali mpaka kufikia ngazi ya Cheo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi, cheo ambacho kilimuwezesha kupewa madaraka ya kuwa Kamanda wa Polisi Mikoa mbalimbali ikiwemo Tabora na Mwanza.

 Kabla ya kufikia ngazi aliyokuwanayo, marehemu aliwahi kuaminiwa na kushika nyazifa mbalimbali akiwa kama Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID), Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) na Mkuu Upelelezi Mkoa (RCO) na hatimaye kupata wadhifa wa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa. 
Marehemu Kamanda Barlow hadi umauti unamkuta alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza na atakumbukwa  kwa juhudi zake za kupambana na kudhibiti uharifu.

No comments:

Post a Comment