Sunday, October 21, 2012

SHEIKH FARID WA UAMSHO ZANZIBAR KAPATIKANA,..VIPEPERUSHI VYAWATIA HOFU WAKRISTO.


 
Habari zilizotufikia muda si mrefu ni kwamba kiongozi wa jumuiya ya Uamsho, Ustaadh Farid amepatikana akiwa katika hali nzuri na kwa sasa yupo kwao kwa mzazi wake akipumzika.
VITISHO:-
Vipeperushi vinavyotishia uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar vimepeperushwa mjini hapa kufuatia ghasia zinazoendelea kwa siku ya tatu mfululizo.
 
Kipeperushi kimojawapo kinasema: “CCM kosa letu kuwatia mbwa msikitini. Sasa tunasema kuwa basi tena litakalokuwa na liwe kwa sisi CCM basi tena umoja na CUF. Nyie CUF/Muamsho Abubakari Khamis Bakar (Waziri wa Katiba), Mussa (Kamishna wa Polisi) na Azizi (Kamanda wa Polisi Mkoa) mmeshazoea fujo na sisi sera yetu CCM sera yetu amani sasa mujiuzulu mumpishe Rais afanye kazi zake, Tumechoka na nyinyi juu ya mauaji ya askari wetu. Ondokeni murudi kwenu.


Wewe Abubakar hukuanza leo na jana ufisadi kazi ya ufisadi umeizoweya hadi ulifungwa jela na mafisadi wenzako, mwishowe huku SMZ kumekuokoa.”
 
Wakati huo huo kuna waraka umesambazwa ambao umewatisha khofu waumini wa dini ya kikristo nchini ukisema wote watakatwa vichwa waraka huo ambao unasemekana umetolewa na watu wenye kujiita jumuiya ya Uamsho umeandikwa na kusambazwa katika maeneo mbali mbali huku wenyewe wakristo wakipelekewa maofisini kwao.
 
Akizungumza na masikitiko Askofu wa Kanisa la Anglikan Mkunazini Emmanuel Masoud amesema ni waraka ambao umewastusha wakristo kutokana na maneno mazito yalioandikwa humo ambapo ndani ya waraka huo. “Maneno yaliandikwa humu yametushitua sana sisi waumini wa dini ya kikristo hapa Zanzibar  kwa kweli sio jambo la kupuuzia ikiwa wanasema watatukata vichwa ni jambo la hatari kabisa” alisema Masoud.
 
Wakizungumzia ukweli juu ya suala hilo Sheikh Azzan amesema jumuiya yake haihusiki na waraka wa aina hiyo na wao kama waislamu hawana sababu ya kuwatisha watu kwa kuwa wanaamini uislamu sio dini ya kuwabagua watu wala kuwatisha watu.
 
Azzan alisema wapo baadhi ya watu ambao wanatumia propaganda mbaya za kutaka kuwagawa wazanzibar katika kipindi hiki na ndio wanatumia kila sababu za kuwagawanya lakini aliwatahadharisha wananchi kuepukana na propaganda kama hizo kwani zinaweza kuitia nchi katika pahala pabaya na kutoweka kwa amani.
 
“Sisi hatuhusiki na waraka huo aliyetoa waraka huo ni watu ambao wanapingana na amani iliyopo lakini pia ni watu wenye kueneza propaganda mbaya za kutaka kuwagawa wazanzibari jambo ambalo sisi tunaamini hatuna ugomvi na wazanzibari wote sisi ni dugu hatubagui awe ni mkristo au muislamu awe mweupe au mweusi hatuwezi kubaguana kwa kuwa misingi ya dini yetu imekataza kubaguana” alisema Azzan

No comments:

Post a Comment