Tuesday, October 16, 2012

MWANZA WALIVYOMUAGA KAMANDA BARLOW



Na George Ramadhan,Mwanza.
 
MAJONZI, simanzi na kauli za kulipa kisasi ni miongoni mwa masuala yaliyogubika shughuli ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Liberatus Barlow aliyeuawa kwa kupigwa risasi usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita eneo la Kitangiri Jijini hapa.
 
Mwili wa Barlow uliagwa jana na wakazi wa Jiji la Mwanza na mikoa ya jirani katika shughuli iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana kabla ya jioni kusafirishwa kwa ndege kuelekea Jijini Dar es salaam ambapo unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda kijijini kwake huko Vunjo mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
 
Akizungumza mbele ya umati mkubwa wa wakazi wa Jiji la Mwanza waliojawa na majonzi, Mkuu wa mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo alisema kifo cha Barlow sio mwisho wa serikali kupambana na uhalifu na wahalifu.
 
Alisema hivi sasa vyombo vyote vya dola vipo kazini vikifanya uchunguzi wa tukio hilo la mauaji na kuhakikisha wahusika wanatiwa mbaroni haraka iwezekanavyo.
 
“Leo Kamanda na Jemedari wetu katika mapambano dhidi ya uhalifu ameondoka, lakini nataka niwahakikishie kwamba tupo vitani, hatupaswi kuweka silaha chini, kama mkoa tuweke silaha zetu vizuri hadi ushindi utakapopatikana”alisema
 
Aliongeza kusema kwamba jamii ya Mwanza na Tanzania kwa ujumla iwe na imani kuwa waliohusika na mauaji ya RPC Barlow hawako salama, kwani lazima watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
 
“Naomba niwahakikishie kwamba vyombo vyote vya dola viko kazini, waliotenda mauaji haya hawako salama, watakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na jambo hili litafikia tamati mapema iwezekanavyo”alisisitiza Ndikilo.
 
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Robert Manumba aliwaambia waombolezaji kwamba taarifa ambazo Jeshi la Polisi limezipata kutoka kwa wananchi zimeongeza kasi ya upelelezi wa mauaji hayo.
 
Aliwataka askari kuwa watulivu katika kipindi hiki cha majonzi lakini akawataka kulipa kisasi dhidi ya mauaji ya RPC Barlow kwa kuhakikisha wanawakamata wote waliohusika.
 
“Umma utambue kwamba hatutalala hadi tuwatie mbaroni wauaji, na hii inapaswa kuwa ndiyo kawaida yetu kuhakikisha uhalifu wa aina yoyote unashughulikiwa kwa uzito ule ule kama tunavyofanya hivi sasa katika mauaji ya RPC Barlow”alisema Manumba.
 
Akitoa salaam za rambirambi, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Absalom Mwakyoma alisema kwamba iwapo kuna wananchi wenye taarifa za watu waliohusika na mauaji hayo wampelekee yeye na atazifanyia kazi.
 
“Ningependa kuwaambi wananchi wenye taarifa za muaji ya RPC Barlow kama wanaona shida kuzipeleka kwingine waniletee mimi tutazifanyia kazi”alisema Mwakyoma ambaye alimfananisha Barlow sawa na kitabu cha marejeo (encyclopedia) kutokana na jinsi alivyokuwa akimsaidia kutatua masuala mbalimbali.
 
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera Phillip Kalangi alisema kwamba idadi ya wahalifu ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya raia wema  hivyo ana imani wakiunganisha nguvu ushindi utapatikana.
 
Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Salum Msangi alisema kwamba Jeshi la Polisi halitakata tamaa kupambana na wahalifu licha ya Kamanda Barlow kuuawa.
 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Lenard Paul na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora Anthony Ruta, katika salaam zao za rambirambi walisema kwamba Jeshi la Polisi limepoteza Kamanda shupavu, mkweli, mweledi na mwalimu kwa makamanda wengine.
 
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Clement Mabina alisema kwamba Kamanda Barlow alizingatia sana sheria katika utendaji wake wa kazi na alikuwa tayari kuitika wito hata kama ni usiku wa manane.
 
Katibu Mwenezi wa Chadema wilaya ya Ilemela Carlos Majura alisema kifo cha Barlow ni pigo kwa wapenda amani wote, hivyo wananchi watumie nguvu ya umma kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
 
Wakati hali ikiwa hivyo katika kuuaga mwili wa Kamanda Barlow, baadhi ya walimu wa shule ya msingi Nyamagana wameelezea kusikitishwa kwao na jinsi tukio hilo la mauaji ya RPC lilivyotokea mbele ya mwalimu mwenzao Doris Moses.
 
Mwalimu Doris ndiye aliyekuwa na RPC Barlow ndani ya gari wakati watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walipowavamia na kumuua kwa kumpiga risasi Kamanda huyo wa polisi.
 
Katika mahojiano na Nipashe, Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo Mary Ngalula alisema kwamba kimsingi wanamuonea huruma mwalimu mwenzao kutokana na kushuhudia tukio hilo la kuogofya.
 
Alisema kwamba wanamsikitikia kwa sababu jamii imeanza kumfikiria vibaya kwa kudhani anahusika kwa namna moja ama nyingine katika mauaji hayo.
 
“Tunamuonea huruma mwalimu mwenzetu kutokana na maneno tunayoyasikia, lakini sisi tuko pamoja naye kwa sababu tunamfahamu ni mtu safi, na hivi tunajiandaa kwenda kumuona na kumtia moyo ili amudu kuilea familia yake kwani ni mjane”alisema.
 
Mwalimu Baraka Magafu yeye alisema kwamba tofauti na hisia za baadhi ya watu kuhusu uhusiano wa Mwalimu Doris na Kamanda Barlow, wao (walimu) wanafahamu kuwa ni watu wa kabila moja wanaotoka kijiji kimoja huko Vunjo mkoani Kilimanjaro.
 
Alibainisha kuwa Mwalimu Doris amekuwa ni mtu anayejihusisha sana na shughuli mbalimbali za watu wa kabila lake (wachaga), hivyo hakuna sababu ya kumfikiria vibaya kwa sababu tu mtu aliyekuwa amemsindikiza nyumbani wakitokea kwenye kikao cha maandalizi ya harusi aliuawa kwa kupigwa risasi.
 
 “Ukifuatilia mwenendo wa tukio lote, utaona kwamba kilichotokea ni bahati mbaya na kingeweza kumtokea yeyote, kwani Barlow alikuwa akimsindikiza Mwalimu Doris nyumbani kwake, na hata baada ya tukio, alipowapigia simu wenzao waliokuwa nao kwenye kikao walikuwa ndo na wao wanafika majumbani mwao”alisema.
 
Aliongeza kwamba katika mazingira kama hayo ni makosa kuwa na mtazamo hasi dhidi ya Mwalimu Doris kama ambavyo baadhi ya watu wameanza kuvumisha kuwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
 
Wakati huo huo habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza kitengo cha upelelezi zimeeleza kwamba simu ya upepo (radio call) ndiyo iliyomponza Kamanda Barlow na kumsababishia kifo.
 
Mmoja wa maofisa upelelezi ambaye hata hivyo hakupenda jina lake litajwe alisema kwamba baada ya Kamanda Barlow kuwa amemfikisha Mwalimu Doris nyumbani kwake, walitokea watu wawili waliokuwa na tochi ambao walimtaka azime taa za gari lakini yeye (Barlow) akagoma.
 
Alibainisha kuwa upelelezi zaidi unaonyesha kwamba walipomsogelea walimlazimisha azime taa za gari lakini aliendelea kushikilia msimamo wake huku akiwaambia kuwa yeye ni RPC.
 
Aliendelea kusema kwamba ghafla walitokea watu wengine takribani watatu ambao inaonekana bado hawakuamini kama kweli huyo ni RPC,lakini alipotoa radio call ili kufanya mawasiliano ndipo walipomfyatulia risasi na kumuua.
 
MWISHO.

No comments:

Post a Comment