Msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni mjini Tabora. |
Katika hali ambayo haikutarajiwa kutokea msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni mjini Tabora,hivi sasa kumekuwa na hali ya kukaniana baina ya Waislamu wa pande mbili waliogawanyika katika msikiti huo mkuu.
Waislamu wa mjini Tabora wakiwemo waumini wa msikiti huo wamegawanyika kutokana na kile kinachodaiwa kuwa mtafaruku wa baadhi ya viongozi wa dini ya kiislam ambao walimwandikia na kumlalamikia Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Simba kuhusu ubadhirifu unaofanywa na viongozi wa Msikiti huo wakiongozwa na Sheikh Mkuu wa mkoa wa Tabora Shaaban Salum ambaye amesimamishwa wadhifa wake kutokana na malalamiko hayo.
Uamuzi wa Mufti wa Tanzania Shaaban Simba wa kumvua madaraka Sheikh wa mkoa wa Tabora umewachukiza baadhi ya waumini wa dini ya kiislam mkoani Tabora na kuamini kuwa mbali ya kumdhalilisha Sheikh Shaaban Salum pia umedhalilisha uislamu kwakile walichoeleza kuwa Shaaban Salum ni kiongozi wa kwanza kuonesha nia ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika msikiti huo kwakuwa tangu aingie madarakani amekuwa akifanya miradi mbalimbali ya maendeleo kutokana na michango midogo ya fedha zinazochangwa na Waislam katika msikiti huo.
Mufti ambaye anaaminika ndio kiongozi mkubwa wa dini ya kiislamu nchini alimteua Sheikh Ibrahim Mavumbi kushika wadhifa wa Sheikh wa mkoa wa Tabora jambo ambalo limendelea kupingwa na wengi licha ya kuwa Mufti Shaaban Simba alijaribu kufika mkoani Tabora kwa nia ya kutaka kutoa ufafanuzi kuhusu uamuzi aliouchukia ingawa ufafanuzi huo aliutoa kwa njia ya Redio za Kijamii jambo ambalo halikuwafurahisha baadhi ya Waumini wa dini ya kiislam.
Askari wa Jeshi la Polisi wamelazimika kuendelea kuzunguukia eneo la Msikiti huo nyakati za Ibada kulinda usalama kwakile kilichoelezwa kuwa baadhi ya waumini wa dini ya kiislam hawamtaki Sheikh mteule Ibrahimu Mavumbi aendeshe ibada katika msikiti huo mkuu wa Ijumaa ambao wanadai ni mali ya Waislam kuliko inavyoaminiwa na upande wa pili wa mgogoro huo ambao umekuwa ukidai ni mali ya Baraza kuu la Waislamu nchini Bakwata.
Hata hivyo wachunguzi wa mambo wameshauri kuwa ni vema pande hizo mbili za Waumini wa dini ya kiislam wakae katika meza ya mazungumzo badala ya kuwepo kwa mvutano huo wa ushabiki unaoelekea kupoteza amani katika msikiti huo.
No comments:
Post a Comment