Katika
hali ambayo haikutarajiwa na wengi,baadhi ya waislamu Tabora kwa
kushirikiana na viongozi wa Msikiti mkuu wa Ijumaa Tabora mjini
wamekusudia kumfikisha mahakamani Sheikh mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban
Simba kufuatia mgogoro uliopo baina ya viongozi wa msikiti huo na baraza
kuu la Waislam Tanzania Bakwata ambao umesababisha mgawanyiko wa
waislamu wa mkoani Tabora.
Taarifa
zilizotufikia zimeeleza kuwa tayari taratibu za mahakamani
zimekwishafanyika katika kufungua mashtaka dhidi ya kiongozi huyo mkubwa
wa dini ya kiislamu hapa nchini na kwamba wakati wowote kuanzia sasa
atafikishwa katika mahakama kuu kanda ya Tabora kukabiliana na shitaka
lake ambalo inadaiwa limemuunganisha yeye(Mufti),Bakwata na Katibu mkuu
wa Bakwata.
Aidha
ikumbukwe kwamba katika siku za hivi karibuni Sheikh mkuu wa Tanzania
Mufti Shaaban Simba aliwasimamisha madaraka viongozi wa msikiti mkuu wa
ijumaa na kumvua wadhifa wake Sheikh wa mkoa wa Tabora Shaaban Salum
jambo ambalo lilipingwa na idadi kubwa ya waumini wa dini ya kiislamu na
hivyo kusababisha kuwa chanzo cha vurugu katika msikiti mkuu wa
Ijumaa Gongoni Tabora mjini.
Katika
muendelezo wa mgawanyiko na mgogoro huo wa waislamu Tabora mjini ambao
ukielezwa kuwa ni wa kwanza kutokea ndani ya miaka zaidi ya 80 iliyopita
ambapo Sheikh mkuu wa Tanzania Mufti Shaaban Simba alimteua Sheikh
Ibrahim Mavumbi kuwa Sheikh wa mkoa katika kipindi cha miezi Sita hadi
hapo uchaguzi utakapofanyika hatua ambayo pia iliendelea kuleta mzozo
mkubwa hata kufikia hatua kwa baadhi ya waumini kupinga kuongoza ibada
kwa Sheikh mteule katika msikiti mkuu wa Ijumaa Gongoni na hivyo
kusababisha aliyekuwa Sheikh mkuu Shaaban Salumu kukamatwa na Polisi na
hatimaye kufikishwa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora akituhumiwa
kwa kosa la kutaka kuleta fujo eneo la kuongozea Ibada msikiti mkuu wa
Ijumaa Gongoni akiwa na wafuasi wengine watano.
Hata
hivyo hali hii bado imeendelea kuzua mashaka makubwa kutokana na kuwepo
kwa tetesi kwamba wapo baadhi ya viongozi wa Serikali na wanasiasa
wamesimama nyuma ya pazia la Mgogoro huo unaoendelea kuwagawa waislamu
ingawa hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa Serikali aliyejipambanua kuwa
anashiriki katika vuguvugu la sakata hilo la waislamu lililoingia
katika sura mpya ya mgongano wa maslahi binafsi kwa baadhi ya kikundi
cha watu.
No comments:
Post a Comment