…………………………………………………………………………..
Na Mwandishi Maalum, Santa Cruz, Bolivia
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amezitaka nchi wanachama
wa G77+China, kuhakikisha zinaboresha kilimo ili ziwe na hifadhi ya
kutosha ya chakula kwa wananchi wake.
Akihutubia mkutano wa mwaka kwa
nchi za G77+China ambao pia ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya
umoja wa nchi hizi, unaofanyika jijini St Cruz De Sierra, Dkt Bilal
alisema nchi za umoja huu zina maeneo mazuri kwa kilimo na hivyo ni
muhimu kuyatumia maeneo haya katika kuzalisha chakula kwa lengo la
kuhifadhi na kuwa na usalama wa chakula nyakati zote.
Dkt. Bilal alisema, nchi hizi
kwa pamoja zinahitaji kuwa na kauli moja kuhusu masharti yanayowekwa na
nchi kubwa hasa katika kilimo na kuelezea kuwa ili mafaniio makubwa
yapatikane, lazima uwepo uwekezaji wa ndani katika kilimo sambamba na
serikali za nchi hizi kuchangia shughuli za uzalishaji ili kuwa na
kilimo chenye tija kwa wakulima na kinachoweza kuchangia usalama wa
chakula.
Kuhusu suala la mazingira,
Mheshimiwa Makamu wa Rais aliwaeleza wajumbe wa G77+China kuwa, maazimio
yaliyofikiwa Rio+20 na mapendekezo kuhusu ‘Kesho tunayoitaka’
yanazihitaji nchi hizi kupaza sauti zake kwa pamoja kuhusu kukabiliana
na mabadiliko ya tabia nchi kwani suala hili kwa sasa haliwezi
kutatuliwa na nchi moja bali linahitaji nguvu ya kila mtu duniani.
Makamu wa Rais alifafanua kuwa
bila kuwa na mazingira bora maendeleo endelevu yatabakia ndoto na pia
kufanikisha Malengo ya Milenia kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa
itakuwa vigumu kama suala la mazingira litaachwa kwa kila nchi kufanya
inavyotaka.
“Kundi hili lina kazi kubwa
iliyo mbele yetu na hasa kuhusu malengo mapya ya maendeleo baada ya
kukamilika kwa muda wa Malengo ya Milenia mwakani. Tunahitajika kubuni
njia za kuzipatia nchi zetu maendeleo katika Nyanja za uchumi, kijamii
na mazingira ili tufanikiwe vema,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Katika hotuba hiyo Mheshimiwa
Makamu wa Rais pia alizungumzia kuhusu umuhimu wa nchi hizi kuweka
msisitizo wa kuwapa wananchi maji safi na salama, umuhimu wa kuwa na
nishati inayotosheleza matumizi ya uzalishaji, uwepo wa huduma bora za
afya na elimu ili kupiga hatua kwa haraka baina ya wananchi wa nchi
hizi. “Nafahamu kufanikisha haya yote ni kazi kubwa lakini hatuna muda
wa kusubiri. Ni lazima tufanye kazi ili kubadili hali
iliyopo,”alifafanua.
Mkutano huo ambao umekamilika
jana kwa mwenyeji wake Rais Evo Morales kuwashukuru wanachama wa
G77+China walioweza kushiriki mkutano huo, pia ulionesha nia kwa
wanachama wa nchi hizi kutafuta majibu ya changamoto ya ukosefu wa ajira
unaokabili wananchi wengi wa nchi hizi. Viongozi wengi walisisitiza
kuwa, suala la ajira hasa kwa vijana linatakiwa kutazamwa upya na hasa
ukizingatia rasilimali zilizopo katika nchi za G77+China ili zitumike
katia kutengeneza ajira mpya zitakazoweeza kusaidia kuboresha maisha ya
watu wa nchi hizi kwa miaka mingi ijayo.
No comments:
Post a Comment