Tuesday, February 11, 2014

CHADEMA YAITUHUMU CCM KUPANGA KUVURUGA UCHAGUZI KILOLO


scaled1 1dad5
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepeleka malalamiko Jeshi la polisi mkoa wa Iringa juu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupanga kuvuruga uchaguzi wa udiwani kata za Ibumu na Ukumbi wilayani Kilolo.

Mwenyekiti wa CHADEMA nyanda za juu kusini, Dkt. Stephen Kimondo anasema wamepata taarifa kuwa CCM kati ya Februari 5 na 6 imepeleka walinzi wake (Green Guard) 50 kwenye kata hizo, 10 kata ya Ibumu wakiongozwa na Ali Simba na 40 kata ya Ukumbi.


Anaongeza kuwa wanafahamu kuwa kazi ya walinzi hao inayofanyika ni kupiga na kutesa wanachama wa CHADEMA lengo likiwa ni kuvuruga uchaguzi unaofanyika leo.

Katika barua yao kwa jeshi la polisi ambayo Mwananchi imepata nakala yake, inatahadharisha kuwa kama jeshi la polisi halitachukua hatua kuzuia walinzi hao wasifanye chochote hali hiyo inaweza kuhatarisha amani na kuwa iwapo jeshi halitachukua hatua za kuhakikisha usalama basi wanachama wao wataamua kujilinda wao wenyewe dhidi ya walinzi wa CCM jambo ambalo litavunja amani katika maeneo hayo.


Kwa mujibu wa jeshi la polisi Iringa CCM na CHADEMA wanatuhumiana kila mmoja kupeleka walinzi wake katika kata zinazofanya uchaguzi.
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi anasema wamepata taarifa hiyo na nyingine kutoka CCM wakidai CHADEMA kupeleka Red Brigade na kuwa hiyo ni joto la uchaguzi.


Anaongeza kuwa kazi ya kulinda usalama si ya red brigade wala green guard kama vyama vinavyofanya, ni ya jeshi la polisi na wanafanya hivyo.
 

Anasema hali ya usalama kwa vituo vyote ni nzuri ambapo kila kituo kitakuwa na askari, watu wajitokeza kupiga kura kwa amani.


Kumekuwepo na vurugu katika Kampeni za uchaguzi wa marudio wa udiwani katika kata tatu mkoani Iringa ikiwemo ya Nduli ambapo Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa alifikishwa mahakamani akituhumiwa kujeruhi kada wa CCM.  

Chanzo: Hakimu Mwafongo

No comments:

Post a Comment