Waumini wa kanisa la TAG tawi la Kitete Christian Center (KCC) la mjini Tabora wakiwa katika ibada ya sikukuu ya Krismas kanisa hapo jana (Picha na Allan Ntana) |
Na Allan Ntana, Tabora
WAKRISTO hapa
nchini wamekumbushwa kumtumaini Bwana Yesu katika maisha yao yote kwa kuwa
alikuja duniani ili wanadamu wote wakombolewe kutoka katika mateso ya aina
mbalimbali sambamba na ondoleo la dhambi.
Kuzaliwa kwaYesu kristo ni mpango kamili wa Mungu
kumkomboa mwanadamu kutoka katika taabu, mateso na kuonewa kwa namna yoyote ile
na shetani, ndio maana kila amwendeaye na kumwamini maisha yake yanabadilika.
Hayo yamebainishwa jana na Askofu Agustino Dedu
alipokuwa akihutubia mamia ya waumini wa kanisa la TAG katika ibada maalumu ya
maadhimisho ya sikukuu ya krismasi iliyofanyika jana katika kanisa la Kitete
Christian Centre lililopo katika Manispaa ya Tabora.
Alisema wakristu wana kila sababu ya kuadhimisha
sikukuu ya krismas kwa kuwa inawakumbusha umuhimu na makusudi ya kuzaliwa kwa
mkombozi wetu Yesu Kristu miaka 2000 iliyopita hapa duniani.
Aidha alisema Yesu Kristo alikidhi vigezo vyote vya
kuitwa mkombozi wa ulimwengu kwa sababu hata kabla ya kuzaliwa kwake
ilishatabiriwa kuwa atazaliwa mtoto wa mwanamume katika mji wa Bethlehemu na
jina lake ataitwa Emanuel yaani Mungu pamoja nasi na huyo atakuwa ni mkombozi
wa ulimwengu.
Kama hiyo haitoshi hata kutungwa kwa mimba yake
kulikuwa kwa miujiza kwani Mariamu
aliyekuwa bikira alipata ujauzito kwa uweza wa Roho Mtakatifu yaani pasipo
kulala na mwanamume yeyote na hata alipozaliwa ulimwengu wote ulitaharuki na
taarifa zake zilisambaa dunia nzima jambo ambalo si la kawaida mwanadamu wa kawaida
anapozaliwa.
‘Wakristu hatuna budi kumtumaini Yesu kwa kuwa
alitolewa kwa ajili yetu ili tuokolewe, tuwe huru na dhambi, tuwe na nguvu za
kuendelea kumshinda mwovu shetani, na zaidi ya yote tuishi maisha matakatifu ya
kumpendeza’, aliongeza.
Askofu
alifafanua kuwa mtu akiwa ndani yaYesu anakuwa kiumbe kipya kwa kuwa mtizamo
wake, tabia zake, fikra na mawazo yake yanabadilika pia, wala hawazi kutenda
uharibifu au jambo lolote lililo kinyume na mapenzi ya Mungu.
Naye Askofu wa Kanisa la TAG jimbo la Tabora Paul
Meivukie amewataka wakristu wote kuendelea kujishusha zaidi na kujiepusha na
mambo yote yaliyochukizo kwa Mungu ili wazidi kumpendeza sambamba na imani zao
kukua zaidi.
No comments:
Post a Comment