Tuesday, April 16, 2013

RUFAA KESI YA UCHAGUZI WA JIMBO LA IGUNGA

 
Na Lucas Raphael,Tabora
 
Mahakama. Ya rufaa nchini  jana imeahirisha  rufaa ilifunguliwa na
mwanasheria wa serikali kupinga maamuzi yaliyomnyanganya ubunge wa
jimbo la Igunga Peter Kafumu – CCM  hadi tarehe 3/05/2013 ili
kusikiliza kwa pamoja rufaa nyingine iliyowasilishwa na mgombea huyo .
 
Uhamzi huo ulifikiwa na jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa
lilichini ya uenyekiti wa jaji Nathalia Kimaro baada ya kuridhika na
hoja za mawakili wa pande hizo mbili ambapo kwa upande wa walalamikiwa
kulikuwa na Profesa Abdalah Safari na Kamaliza Kayaga huku upande wa
serikali ukiwakilishwa na wakili Malata.
 
Jopo hilo la majaji wa mahakama ya rufaa lilitoa hoja kwa mawakili wa
pande hizo kwamba maombi ya rufaa  na 18/2013 iliyowasilishwa na
mwanasheria wa serikali na yale yaliyofunguliwa na Peter Kafumu
yanafanana na yanawahusisha watu wale wale ni vizuri yakasikilizwa kwa
pamoja.
 
Kabla ya kutolewa kwa uhamzi huo prof Safari aliiambia mahakama hiyo
kuwa wateja wao Joseph Kashindye na Wenzake kupitia chama cha
Demokrasia na Maendeleo -  CHADEMA wamechelewa kupata nakala ya hoja
za muomba rufaa na ili kutenda haki shauri hilo lisogezwe mbele.
 
Chumba cha mahakama kilijazana wafuasi na wanachama cha CHADEMA
waliokuwa wakiongozwa na mwenyekiti wa mkoa huo Kansa  Mbarouk na wale
wa wilaya za Igunga na Tabora mjini.
 
Kufuatia  uhamzi huo jopo hilo la majaji akiwemo jaji William Mandia
na jaji Semistrocles Simon Kaijage wameahirisha rufaa hiyi hadi mei
tatu mwaka huu waweze kusikiliza rufaa hizo kwa pamoja.
Kukatwa rufaa hizo kunafuatia maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Tabora, iliyotengua matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo la
Igunga mkoani hapa baada ya kubainika kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na
vitendo vya rushwa, kampeni chafu na vitisho dhidi ya wapiga kura.
 
Jaji Mary Nsimbo Shangali wa mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora,
alitangaza kutengua matokeo hayo baada ya mahakama hiyo kuridhika na
hoja saba  zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji  kati ya hoja  17
zilizowasilishwa katika mahakama hiyo.
 
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mlalamikaji aliyekuwa mgombea wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Joseph kashindye, ambaye
aliwakilishwa na wakili Maarufu nchini Profesa Abdallah Safari  ambapo
alipinga mtokeo ya uchaguzi huo akilalamikia kukiukwa kwa sheria ya
uchaguzi mkuu.
 
Upande wa Utetezi  uliwakilishwa na  mawakili Mohamed Salum Malik na
Gabriel Malata kutoka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali, Msimamizi
wa Uchaguzi jimbo la Igunga,  na mawakili Antony Kanyama na Kamaliza
Kayaga waliokuwa wakimtetea mbunge wa Igunga Peter Dalali Kafumu.
 
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua saa nne, Jaji Shangali alisema kuwa
mahakama imeridhika na upande wa mlalamikaji katika malalamiko yake
saba, ambayo alisema yanathibitika na kuonyesha kuwa uchaguzi huo
mdogo wa jimbo la Igunga haukuwa huru na haki.
 
Alivitaja baadhi ya kasoro zilizopelekea kutengeliwa kwa uchaguzi huo
ni pamoja na  Ahadi  iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi  Dk. John Pombe
Magufuli, kuhusu  ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo alidai kwamba  kama
wananchi hawataichagua CCM daraja hilo halitajengwa, wakati ambapo
katika kipindi hicho kulikuwa na shida kubwa ya usafiri katika eneo
hilo.
 
Alisema Kitendo pia kilichofanywa na mbunge wa Tabora mjini Ismail
Aden Rage, hakikuwa cha uungwana kwani alitumia lugha ya uongo kwa
lengo la kupotosha wapiga kura ambapo alidai mgombea wa chama cha
Demokrasia na Maendeleo  ( Chadema) amejitoa katika uchaguzi huo.
 
Jaji Mary pia alisema kitendo cha serikali kugawa mahindi ya msaada
kwa wakazi wa Igunga katika kipindi cha kampeni kitu ambacho kimeleta
fadhaa kubwa kwa wapiga kura, huku akihoji je ni nani aliyekufa njaa
katika kipindi hicho na kwamba kulikuwa na umuhimu gani wa kugawa
mahindi katika kipindi cha kampeni.
 
MWISHO.

No comments:

Post a Comment