Tuesday, April 16, 2013

WANAFUNZI 1605 WA KIDATO CHA KWANZA URAMBO ‘HAWAJARIPOTI SHULENI’

 
Na Lucas Raphael, Urambo
JUMLA ya wanafunzi 1605 kati ya 4604 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu katika wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, wameshindwa kuripoti katika shule za sekondari walizopangiwa kwa ajili ya kuanza masomo licha ya kupewa muda wa kutosha kuripoti katika shule hizo.
Hayo yalibainishwa jana na ofisa elimu (taaluma) anayeshughulikia elimu ya sekondari wilayani  Urambo, Grace Nghambi Monge, katika taarifa iliyoandaliwa na idara hiyo ikionyesha idadi halisi ya wanafunzi walioingia kidato cha kwanza mwaka huu, ambapo taarifa hiyo inaonyesha kwamba wanafunzi 1605 sawa na 35%  ya waliotakiwa kuingia sekondari hawajaripoti.
Nghambi alieleza kuwa kati ya wanafunzi hao 1605 wavulana ni 800 na wasichana ni 805, na walioripoti mpaka sasa hivi ni 2989 sawa na 65% tu ambapo wavulana ni 1713 na wasichana ni 1276, aliongeza kuwa idadi hiyo ya watoto walioshindwa kuripoti ni kubwa sana ukilinganisha na mikakati waliyokuwa wamejiwekea.
Nghambi alibainisha sababu zilizochangia wanafunzi hao kushindwa kuripoti shuleni kuwa ni baadhi yao kuolewa mapema, kukosa ada na mahitaji muhimu yanayotakiwa shuleni ikiwemo sare  za shule, madaftari, kalamu na kadharika, na hii inatokana na umaskini wa wazazi walio wengi katika wilaya hii ambao unawafanya kuwa na mwamko mdogo katika suala la elimu.   
Nghambi aliongeza kuwa mambo mengine yaliyochangia kutoripoti ni kitendo cha wazazi kuwatumikisha watoto wao katika shughuli za kilimo hasa tumbaku na wazazi wengine kuwazuia watoto wao kuendelea na masomo kwa kisingizio cha kupoteza nguvu kazi katika kilimo hicho.
Aidha Nghambi aliongeza kuwa watoto wengine hususani wale wanaotoka katika jamii ya wafugaji wameshindwa kuripoti sekondari kwa sababu ya kuhamahama kwa wazazi wao kwa ajili ya kutafuta malisho ya mifugo yao, jambo linalowafanya kuishi umbali mrefu na mahali shule ilipo.
Akizungumzia mikakati ya kupambana na changamoto hizo, Nghambi alisema kwamba halmashauri ya wilaya hiyo imekusudia kuwasaka na kuwafungulia mashtaka wazazi wote waliowazuia watoto wao kujiunga na wenzao sambamba na kuwaelimisha wazazi hao juu ya umuhimu wa kumsomesha mtoto na madhara ya kumkosesha haki hiyo ya msingi.
Aidha, halmashauri hiyo pia imekusudia kuongeza nyumba za waalimu na hosteli za wanafunzi kwa baadhi ya shule ili kupunguza kero ya umbali mrefu uliopo kati ya shule na makazi ya watu.
Naye Coleta Hassan, ambaye ni Ofisa elimu idara ya msingi, akizungumzia mikakati iliyowekwa na halmashauri hiyo katika suala la kuboresha elimu, alisema kuwa wamekusudia kukarabati madarasa, ofisi, nyumba za waalimu, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wazazi  kuchangia chakula ili kuanzisha utaratibu wa kuwapatia chakula cha mchana wanafunzi wote wanapokuwa shuleni.

No comments:

Post a Comment