Thursday, May 9, 2013

MAHAKAMA YA RUFAA YATENGUA MAAMUZI YAMREJESHEA DKT KAFUMU CCM UBUMGE‏


 

Na Lucas Raphael,Tabora

 
Mahakama ya rufaa nchini imetengua maamuzi ya mahakama kuu na kumrudishia ubunge wake Dkt Peter Dalali Kafumu – CCM wa jimbo la Igunga baada ya kuridhika ha hoja za upande wa mrufani kuwa jaji aliyesikiliza shauri hilo hakuzingatia matakwa ya kisheria.

Akisoma  uamunzi huo mwenyekiti wa jopo la majaji wa mahakama hiyo jaji Nathalia Kimaro akisaidiana na jaji William Mandia na jaji Semistrocles Kaijage amesema kuwa mlalamikiwa hakulipa ada ya mahakama kama sheria ya uchaguzi inavyoelekeza.

Aliongeza kuwa awali wakati shauri hilo namba  10/2011 linafunguliwa mahakama kuu jaji aliyelisikiliza hakusikiliza pingamizi la mrufani kwamba hakukuwa na ada iliyolipwa hivyo hakupaswa kuendelea na usikilzwaji wake.

“ kutolipwa ada ama kutokuwepo kwa kumbukumbu yoyote katika jalada la mahakama inayoonyesha kitu kiwekwa kama kinga ilikuwa ni sababu tosha ya kutosikiliza shauri hilo” walisema majaji hao katika maamuzi yao.

Katika hoja zake wakili  wa serikali Gabriel Malata  za kutaka yatenguliwe maamuzi ya mahakama kuu aliwaambia  majaji wa mahakama ya rufaa kuwa jaji aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kuanza kuisikiliza kwani mlalamikaji hakutimiza matakwa ya kisheria.

Malata alidai kuwa mlalamikaji hakulipa ada ya mahakama kiasi cha shilingi milioni moja alizotakiwa kutoa au hati ya nyumba kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa kama sheria ya uchaguzi kifungu na 111 inavyoelekeza.

Wakili Malata aliongeza kuwa kwa vile mjibu Rufaa Joseph Kashindye  na wenzake hakutekeleza sharti hilo  usikilizwaji wa shauri hilo pamoja na mwenendo mzima yakiwemo maamuzi vyote vilikuwa ni batili.

Aliongeza kuwa malalamiko yaliyopelekwa mahakama  ni ya kutengeneza kwani hayajawahi kuwasilishwa katika kamati ya maadili ya uchaguzi kama walivyofanya juu ya suala la mbunge wa Tabora mjini Ismali Aden Rage  ambaye alitozwa faini ya shilingi laki moja kwa kutembea na
silaha kwenye mkutano.

Hoja hizo na nyingine zilipingwa na wakili wa mjibu rufaa profesa Abdalah Safari ambaye aliitaka mahakama ya rufaa kuzitupilia mbali na kwamba Mahakama iliyosikiliza kesi hiyo iliridhika kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria wakati wa zoezi zima la uchaguzi wa jimbo la Igunga ndipo katengua matokea.

Kukatwa rufaa hiyo kunafuatia maamuzi ya Mahakama Kuu ya Tanzania iliyotengua matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani hapa baada ya kubainika kuwa uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, kampeni chafu na vitisho dhidi ya wapiga kura.

Jaji Mary Nsimbo Shangali wa mahakama kuu Agasti 21 mwaka jana alitangaza kutengua matokeo hayo baada ya mahakama hiyo kuridhika na hoja saba  zilizowasilishwa na upande wa mlalamikaji  kati ya hoja  19 zilizowasilishwa katika mahakama hiyo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Mlalamikaji aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Joseph kashindye, ambaye aliwakilishwa na wakili Maarufu nchini Profesa Abdallah Safari  ambapo alipinga matokeo ya uchaguzi huo akilalamikia kukiukwa kwa sheria ya uchaguzi mkuu.

Upande wa Utetezi  uliwakilishwa na  mawakili Mohamed Salum Malik na Gabriel Malata kutoka ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali,Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Igunga,  na mawakili Antony Kanyama na Kamaliza Kayaga waliokuwa wakimtetea mbunge wa Igunga Dkt Peter Dalali Kafumu.

Akisoma hukumu jaji Shangali alizitaja baadhi ya kasoro zilizopelekea kutengeliwa kwa uchaguzi huo ni pamoja na  Ahadi  iliyotolewa na Waziri wa Ujenzi  Dk. John Pombe Magufuli, kuhusu  ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo alidai kwamba  kama wananchi hawataichagua CCM daraja hilo halitajengwa, wakati ambapo katika kipindi hicho kulikuwa na shida kubwa ya usafiri katika eneo hilo.

Alisema Kitendo pia kilichofanywa na mbunge wa Tabora mjini Ismail Aden Rage, hakikuwa cha uungwana kwani alitumia lugha ya uongo kwa lengo la kupotosha wapiga kura ambapo alidai mgombea wa chama cha Demokrasia na Maendeleo  ( Chadema) amejitoa katika uchaguzi huo.

akizungumza na gazeti hili mara baada ya maamuzi hayo nje ya mahakama aliyekuwa mjibu rufaa  Joseph Kashndye  amekubali na kuridhika na maamuzi hayo  huku akiwalalamikia mawakili wake kwamba hawakumwelekeza kufanya hivyo.

“ Sikujua, sikuelezwa  hili ni tatizo la kiufundi  hivyo silaumu” alisema  Kashindye.

Umati wa wananchama wa chadema ambao ulijaa ndani ya chumba cha mahakama kwakweli uliondoka kwa uzuni eneo hilo la mahakama wakikibali matokeo huku wengine wakisema tukajipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao

Hata hivyo Dkt kafumu akuwepo mahakamani alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kwamba hukumu iliyotewa na mahakama ya Rufaa ndio haki kamili kwani mwanzo alikuwa na wasiswasi na jaji yule lakini alionekana anaongopa kuangushwa .
Alisema kwamba amerejeshwa ubunge wake kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wa Igunga bila kujali Itikadi ya chama chochiote cha siasa kwani waliompa kura na kumyima kura wote ni wananchi wa Igunga.

Dkt Kafumu alisema kwamba yale ambayo alikuwa hameyaanzisha ndio anataka kuendeleza kwa nguvu zake zote kwa ajili ya maendeleo ya Igunga na wananchi wake  kwa ujumla.

“mimi nijembe kama nilivyokuwa nasema wakati wa kampeni zangu kwamba mimi ni kwa ajili ya wananchi wa Igunga hasa vijana na wale wa vyama Rafiki na ccm “alisema Dkt Kafumu.

Aidha mwenyekiti wa ccm wilaya ya Igunga Costa Olomi alisema kwa ushindi wa kafumu ni wananchi wote wa Igunga sio wa chama bali ni kwajii ya maendeleo ya Igunga na mkoa wa Tabora .

Alisema kwamba baaada ya kurejeshwa umbunge wake chama cha mapinduzi kimepanga mapokezi makubwa ya kupokea mbunge huyo hapa mei 12 mwaka huu kwa ajili ya sherehe ya kupongeza .

MWISHO.


No comments:

Post a Comment