Friday, July 18, 2014

21 WAHITIMU KOZI YA UKOCHA WA SOKA TABORA

Meneja masoko wa Benki ya Exim tawi la Tabora Jeremia Majebele akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya ualimu wa mpira wa miguu John Kilowoko ambaye ni mtumishi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora baada ya kuhitimu kozi ya ualimu wa soka ngazi ya kazi.
Na Allan Ntana, Tabora

WAALIMU 21 wanaofundisha timu za mpira wa miguu kutoka mikoa ya
Simiyu, Shinyanga, Mbeya na Tabora wamehudhuria na kuhitimu mafunzo ya
ukocha (intermediate course) yaliyofanyika katika uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora.

Mafunzo hayo yaliyochukua muda wa wiki 2 yaliendeshwa na Mkufunzi
mahiri hapa nchini Meja mstaafu Abdul Omar Mingange toka jijini DSM,
ambapo washiriki 22 walitoka mkoani hapa huku 2 wakitokea Shinyanga, 1
Simiyu na 1 jijini Mbeya.

Akikabidhi vyeti kwa waalimu hao, Meneja Masoko wa benki ya EXIM tawi
la Tabora Jeremia Bajebere aliyekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Meneja
wa tawi hilo Edwin Poul aliwataka wahitimu hao kujiendeleza zaidi ili
wawe na kiwango kikubwa kwani ukocha ni ajira nzuri sana siku hizi na
inalipa.

Mwenyekiti wa Chama cha Makocha (TAFCA) mkoani Tabora Mwl Mohamed Ali
Mozi alisema lengo la mafunzo hayo ni kuinua viwango vya makocha toka
ngazi ya awali kwenda ngazi ya juu ili waweze kutoa elimu bora
itakayosaidia kuinua kiwango cha soka kwa vijana katika mikoa yao.

‘Hawa waalimu wamepata taaluma nzuri sana ya mpira wa miguu, naamini
watasaidia sana kuinua soka la vijana mashuleni na katika vilabu
mbalimbali ikiwemo kutambua vipaji vya wachezaji na kuviinua’,
aliongeza.

Aidha alisema changamoto kubwa inayowakabili waalimu wa soka hapa
nchini ni uhaba wa vifaa vya michezo vya kufundishia sambamba na vyama
vya soka kutowatambua na kuwatumia ipasavyo makocha wazawa kama mtaji
wa kuinua vipaji katika mchezo huo.

Mkufunzi wa mafunzo hayo Meja mstaafu Abdul Omar Mingange amesifu
mwitikio mkubwa na kiwango kilichoonyeshwa na waalimu hao wakati wa
mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa nadharia na vitendo jambo ambalo
limewawezesha kufaulu kwa alama za juu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Tabora Yusuph Kitumbo
amepongeza hatua ya waalimu hao kujitokeza kwa wingi katika mafunzo
hayo kwani itaongeza idadi ya makocha wa soka mkoani humo huku
akiahidi kulipa gharama zote  za vyeti vya wakufunzi hao.

Alisema kuwa kuanzia sasa timu zote hapa Tabora kuanzia daraja la nne
na kuendelea ni lazima zifundishwe na makocha waliopitia mafunzo
maalumu yaliyoandaliwa na chama cha Makocha TAFCA ili waweze kutumia
elimu yao vyema.

No comments:

Post a Comment