Tuesday, October 21, 2014

455 WAHITIMU CHUO KIKUU AMUCTA -TABORA

 

www.kapipijhabari.com



WANAFUNZI 455 wamehitimu mafunzo ya kozi mbalimbali ikiwemo shahada ya
uzamili katika Chuo Kikuu cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (AMUCTA)
ambacho ni Chuo Kikuu kishiriki cha Mtakatifu Augustino katika
mahafali ya pili ya Chuo hicho yaliyofanyika jana mjini Tabora.

Akizungumza katika mahafali hayo Mwenyekiti wa bodi ya Chuo hicho
Mhashamu Baba Askofu Mkuu Paulo Ruzoka ambaye pia ni Askofu wa Jimbo
Kuu la Tabora aliwataka wahitimu hao kuwa kioo katika jamii na
kutekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa ili kukiwakilisha vyema chuo
hicho.

Askofu Ruzoka aliwakumbusha kuwa elimu waliyopata ni kwa faida ya
Watanzania wote hivyo wanapaswa kuitumia kwa manufaa yao na jamii
inayowazunguka mahali popote watakapokuwa sambamba na kushiriki kazi
zote kwani jamii ina mategemeo makubwa sana kwao.

Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Askofu Ruzoka aliwakumbusha wahitimu
hao kusoma kwa makini katiba iliyopendekezwa ili zoezi la kupiga kura
litakapofika wafanye uamuzi sahihi na sio ushabiki tu wa makundi.

Aidha aliwakumbusha kuwa ili wawe na sifa ya kupiga kura ni lazima
wajiandikishe kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wakati
utakapofika.

Askofu Ruzoka alisisitiza zaidi wahitimu hao kuhamasishana wao kwa wao
wakiwemo wananchi wenye umri wa kupiga kura kwa pamoja wajiandikishe
kupiga kura ili haki yao ya msingi isipotee bure.

Aliwataka kuwa waelimishaji wazuri kwa jamii katika masuala mbalimbali
yanayolenga mustakabali wa maendeleo ya taifa kwa ujumla sambamba
kujiendeleza zaidi kielimu.

Katika hotuba yake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora
(AMUCTA) Padre Dr. Juvenalis Asantemungu alipongeza jitihada za bodi
na uongozi mzima wa chuo hicho ambazo zimekiwezesha kukua kwa kasi na
ongezeko kubwa la wanafunzi, wahadhiri na kozi mbalimbali.

Akizungumzia mkakati wa kuinua kiwango cha elimu hapa nchini Dr
Asantemungu alisema Chuo hicho kinampango wa kuanzisha kozi ya diploma
ya elimu kwa walimu wanaofundisha shule za msingi kozi ambayo itakuwa
inafundishwa siku za Ijumaa na Jumamosi ili kutoa fursa kwa walimu hao
kusoma huku wakiendelea na kazi zao lengo likiwa kuiwezesha serikali
kutimiza mpango wake wa ‘matokeo makubwa sasa’.

Akitoa takwimu za wanafunzi waliohitimu mwaka huu alisema wanafunzi 18
wamehitimu Shahada ya Uzamili katika Utawala wa Elimu na Mipango
(Maters of Education Management and Planning) na 345 Shahada ya kwanza
ya Elimu Jamii na Ualimu (Bachelar of Arts with Education).

Wahitimu wengine ni 48 wa Shahada ya kwanza ya Sosholojia (Bachelar of
Arts in Sociology) na 37 waliohitimu kozi za Astashahada katika fani
za Uongozi wa Biashara, Ununuzi na Ugavi, Ukutubi na Utunzaji wa
kumbukumbu.

Aidha Dr.Asantemungu aliwasisitiza kuwa mabalozi wazuri huko waendako
na wazidi kujiendeleza zaidi kwa shahada za Uzamili na Uzamivu kwa
kuwa elimu ni chachu kuu ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii
ulimwenguni kote huku akisisitiza uvumilivu wanapopambana na
changamoto katika safari yao kimaisha.

No comments:

Post a Comment