Wednesday, October 22, 2014

SERIKALI YAFUTA MAFUNZO YA UALIMU NGAZI YA CHETI


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr.Shukuru Kawambwa akizungumza wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana

 

SERIKALI imefuta kozi zote za mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti kuanzia mwaka huu kwa lengo la kuboresha kiwango cha elimu hapa nchini.

Tamko hilo limetolewa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr Shukuru Kawambwa alipokuwa akizungumza na wanachuo wa Chuo Cha Ualimu Tabora kilichoko katika Manispaa ya Tabora.

Alisema kuanzia mwaka huu serikali imeamua kuondoa mafunzo ya ualimu ngazi ya cheti ikiwa ni mkakati maalumu wa kuanza kuboresha kiwango cha elimu hapa nchini ambapo waalimu watakaoajiriwa kufundisha shule za msingi na sekondari watatakiwa kuwa na elimu ya kiwango cha diploma na kuendelea.

Alieleza kuwa kuanzia sasa wizara yake inataka ubora wa elimu upatikane kutokana na ubora wa waalimu huku akibainisha kuwa waalimu wote watakaoajiriwa katika shule za msingi na sekondari kuanzia mwaka huu lazima wawe na elimu ya kiwango cha kuanzia diploma na kuendelea huku akifafanua kuwa wale wasiokuwa na diploma watapewa fursa ya kujiendeleza bila tatizo lolote.

Aidha alisema waalimu wa shule za msingi na sekondari na wahitimu wa kidato cha sita waliopata daraja la 1-3 waliochaguliwa kujiunga na kozi maalumu ya mafunzo ya ualimu tarajali ngazi ya cheti wote watapelekwa vyuoni kupata masomo ya ngazi ya diploma katika vyuo maalumu vilivyoandaliwa.

Aidha katika kuhakikisha mpango huu mpya unatekelezwa, Dr Kawambwa alisema wizara inaandaa waraka maalumu wa maelekezo utakaotumwa kwa wakurugenzi wote wa halmashauri zote hapa nchini.


Akijibu swali la wanafunzi wa chuo hicho waliotaka kujua ni kwa nini mda wa  kwenda kufanya mazoezi (BTP) umepunguzwa na kuwa wiki 3 badala ya siku 60, waziri alisema utaratibu huo ni wa dharura tu kutokana na uhaba wa fedha ila akaahidi kuwa watajitahidi kurekebisha hali hiyo kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu.

Aidha kuhusiana na ombi la kuongezwa posho ya mazoezi kutoka sh 4500 wanazolipwa sasa wanafunzi hao wa mafunzo ya ualimu hadi sh 7500 wanazolipwa wanafunzi wa ngazi ya shahada, waziri aliahidi kulifanyia kazi kutokana na bajeti ya wizara yake itakavyokuwa.

Aidha waziri aliwataka wanafunzi wote wa vyuo vya ualimu kuhakikisha wanafaulu masomo yao yote wanayofundishwa chuoni ili waweze kuajiriwa na serikali vinginevyo watalazimika kukaa benchi.

‘Wakati naingia wizarani  nilisema sitaajiri waalimu waliofeli na nitaendelea na msimamo huo huo kwa nia njema kabisa, jitahidini kufaulu masomo yenu yote ya kufundishia na yale ya ziada vinginevyo hatuwapi kazi, alisema Dr Kawambwa.

No comments:

Post a Comment