Thursday, January 3, 2013

HEREHE ZA MIAKA 49 YA MAPINDUZI KUANZA KESHO ZANZIBAR

Na Maelezo Zanzibar  
Sherehe za miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar zinaanza rasmi kesho kwa kazi za kufanya usafi wa mazingira katika Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa Ratiba iliyotolewa na Kamati ya Sherehe na maadhimisho ya kitaifa imeonesha kuwa Miradi ipatayo 62 inatarajiwa kuzinduliwa katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete atafungua Skuli mpya ya Sekondari ya Mlimani, iliyopo Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni Shamra shamra za Sherehe hizo.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein naye atazindua miradi mbalimbali ikiwemo Ufunguzi wa Jengo la Chuo cha Utawala wa Umma huko Tunguu Wilaya ya Kati Unguja.

 Pia atafungua mradi wa E-Government katika Wilaya ya Magharibi Unguja na kufungua Skuli mpya ya Sekondari ya Umoja, iliyopo Uzini Wilaya ya Kati Unguja pamoja na kuzindua Barabara kutoka Mfenesini hadi Bumbwini Wilaya ya Kaskazini B Unguja.

 Hali kadhalika Dkt.Shein atafungua Mradi wa kuhama kutoka Teknolojia ya Analojia kwenda Dijitali na Ufunguzi wa Studio ya kurikodia Sanaa na Muziki ambapo kwa upande wa Pemba atafungua Skuli mpya ya Sekondari ya Shamiani iliyopo Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
  Mbali na Shughuli hizo siku ya kilele hapo January 12 kwenye Uwanja wa Amani Rais Shein atakagua Gwaride lililoandaliwa na Vikosi vya ulinzi na usalama na Vikosi vya SMZ pamoja na kulihutubia Taifa na Usiku kuhudhuria Taarab rasmi huko katika Ukumbi wa Salama Hoteli ya Bwawani

 Naye Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad atafanya uzinduzi mbali mbali kwa ufunguzi wa Skuli na Maabara wakati Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Idd atafanya Shughuli kama hizo kwa ufunguzi wa Skuli na Majengo mapya ya nyumba za Wazee zilizopo Sebleni Wilaya ya Mjini Unguja.

 Mbali na shughuli hizo baadhi ya Marais wastaafu,Mawaziri mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Muungano watafanya shughuli za ufunguzi wa Miradi mingine ikiwemo ya Maji, Skuli na Mradi wa Mnara wa Radio wa Masafa ya Kati uliopo Bungi Wilaya ya Kati Unguja.

No comments:

Post a Comment