Friday, January 18, 2013

RPC TABORA KUYAFUNGIA MAKAMPUNI YA ULINZI

 

Jeshi la Polisi mkoani Tabora limeahidi kuyafungia makampuni ya ulinzi ambayo yanashindwa kutekeleza  masharti yaliyopewa  kwa kuajiri  walinzi wasio  waadilifu ambao wamekuwa wakila njama za kufanya uharifu wa wizi kwenye taasisi ambazo wameingia nazo  mkataba wa ulinzi.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora  ACP  Anthony  Rutha  akizungumza  na  mwandishi wetu  ofisini kwake,alikiri kuwepo kwa  baadhi  ya  makampuni  ya ulinzi ambayo hayafuati taratibu za ajira za walinzi huku akiapa kuyashughulikia ipasavyo kwakuwa  baadhi ya makampuni hayo yamekuwa yakiajiri walinzi wasio na sifa.

''Ninatarajia kuendesha oparesheni maalumu ya kuyafuatilia makampuni haya ya ulinzi na endapo kama kuna kampuni ambalo halijafuata taratibu na kanuni zilizowekwa tutalifungia haraka"alisema kamanda Rutha



Kuhusu matukio ya hivi  karibuni  ya  wizi  uliofanyika katika Shirika lisilo la kiserikali  la  Total Landcare  ambalo lilipata  hasara ya zaidi ya shilingi mil.kumi baada  ya  walinzi wa kampuni  ya ulinzi  ya Alliance Day & Night hapa  mjini  Tabora  ambao  wanadaiwa kula  njama na kufanya wizi wa kuvunja ofisi za Shirika hilo,Kamanda Rutha alisema bado Polisi wanaendelea na uchunguzi lakini mlinzi mmoja wa kampuni hiyo  anayefahamika kwa jina la Said Kayungilo alitoweka kabla ya kukamatwa.

Rutha alisema wakati wa kufuatilia tukio hilo Polisi ilibaini kuwa pamoja na mambo mengine lakini pia ajira ya mlinzi huyo Said Kayungilo katika kampuni hiyo ya ulinzi ilionesha kutatanisha kwakuwa hata wadhamini wake nao wamekimbia na hivyo kutia shaka kuwa huenda mtandao huo wa wizi umekuwa ukishirikisha walinzi na wadhamini wao katika mashirika wanayoajiriwa.

Alisema kwasasa Jeshi la Polisi litafuatilia ajira ya kila mtumishi au mlinzi aliyeajiriwa kwenye makampuni ya ulinzi ili kujiridhisha kama taratibu zimefuatwa ikiwa ni pamoja na makampuni hayo kuwapeleka walinzi wao ofisi za Jeshi la Polisi Tabora  kuchukuliwa alama za vidole ambazo zitapelekwa makao makuu ya Jeshi hilo jijini Dar kwa ajili ya uchunguzi zaidi na ili kubaini kama walinzi wanaoajiriwa na makampuni hayo hawajawahi kujihusisha na makosa mbalimbali ya uharifu.

Hata hivyo imebainika kuwa baadhi ya makampuni ya ulinzi hapa mkoani Tabora yameajiri watu ambao hawajawahi kupitia hata mafunzo ya mgambo wakiwemo walioacha kufanya kazi kwenye baa,mahoteli na kibaya zaidi wengine ni wale wanaojihusisha na matukio ya wizi wa uvunjaji na tayari taarifa zao ziko bayana.
Kwaupande mwingine baadhi ya walinzi wanaofanyakazi katika makampuni ya ulinzi hapa mkoani Tabora,kwa masharti ya kutopigwa picha wala kutajwa majina yao walisema tatizo kubwa la wamiliki wa makampuni hayo ya ulinzi ni kupenda kuajiri walinzi kwa mshahara mdogo ndio sababu ya kufikia kuajiri watu wasio na sifa.

"Unavyotuona ndugu mwandishi mishahara tunayoipata ni aibu tupu kutaja mbele za watu,...utakuta kwenye mkataba umeandikwa tunalipwa shilingi elfu themanini,lakini siku ya kuchukua pesa unajikuta umepokea elfu hamsini na tano au arobaini,kisha zinazushwa sababu eti ulichelewa kuingia kazini mara hujapiga pasi sare za kazi,yaani ilimradi tu udhulumike"alisema mmoja wa walinzi wa kampuni la ulinzi la Alliance

''Mdogo wangu najua huwezi kumwambia mtu mimi inafikia hatua usiku naacha lindo nakwenda kuendesha baiskeli ya daladala ili nipate hela ya unga na chai ya watoto asubuhi ninaporudi nyumbani,maana najua kuiba au kushirikiana na waharifu waje wavunje kwenye lindo langu siwezi hivyo nalazimika kutumia njia hiyo ingawa nayo ni kuomba Mungu tu"alisema mlinzi  mmoja wa kampuni ya Salu Security ya hapa mjini Tabora.     

Pamoja na kuwepo kwa matukio hayo  ya uharifu  katika ofisi mbalimbali zinazolindwa na baadhi ya makampuni ya ulinzi,jambo linaloshangaza zaidi ni vipi walinzi hao washiriki uharifu huo na tena kwanini wizi huo uwe ni ule unaohusisha nyaraka na vitu vinavyotunza nyaraka hizo zilizo muhimu.

Uchunguzi  wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi  ya  makampuni ya ulinzi  hapa mkoani Tabora mbali ya kuajiri watu wasio na sifa lakini pia malipo ya mishahara  kwa  watumishi  imekuwa ni tatizo  sugu  na hivyo  kusababisha  baadhi  ya  walinzi  kuwa rahisi kushawishika na kujiingiza katika vitendo hivyo vya kiharifu kwa lengo la kutafuta namna ya kujikimu kimaisha.  
Pamoja na kuwa baadhi ya makampuni ya ulinzi kupata dhamana ya kulinda ofisi na mali za taasisi mbalimbali lakini cha ajabu dhamana hiyo imeanza kuingiwa dosari kwa kile kinachodaiwa kuwa ndio yamekuwa mzizi au mhimili mkuu wa vuguvugu la uharifu wa kuaminiwa.    

No comments:

Post a Comment