NA LUCAS RAPHAEL- KALIUA
SERIKALI wilayani Kaliua imepongeza jitihada za kutokomeza utumikishwaji watoto wadogo katika mashamba ya tumbaku na kazi za nyumbani zinazofanywa na mradi wa PROPSER kwa kuwa tatizo hilo limekuwa kikwazo kikubwa kwa watoto waliowengi mkoani Tabora kutopata fursa ya kwenda shule.
Pongezi hizo zimetololewa na mkuu wa wilaya ya Kaliua, Savery Maketta, katika kilele cha maadhimisho ya siku ya kupinga utumikishwaji  watoto duniani iliyofanyika  juzi katika kijiji cha Igwisi wilayani hapa ambapo pamoja na mambo mengine alisifu jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na taasisi ya Winrock International kupitia mradi wake wa PROSPER unaotekelezwa katika mkoa wa Tabora.
Akizungumza katika sherehe hiyo iliyohudhuria na wanakijiji kutoka vijiji vya Igwisi, Nsimbo, Mahalaja na Mpandamlowoka, mkuu wa wilaya kupitia  mwakilishi wake, Josephati Brown, ambaye ni Afisa Tarafa wa wilaya ya Kaliua alisema kuwa mradi wa PROSPER umekuwa mkombozi kwa maelfu ya watoto mkoani Tabora kwani jitihada zake za kuendelea kupinga kila namna ya utumikishwaji zimezaa matunda.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa wimbi la watoto wa mitaani limeendelea kuongezeka kwa kasi kubwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini huku watoto hao wakitumikishwa katika kazi za nyumbani,mifugo  na mashambani kwa ujira mdogo, jambo linalohitaji kupingwa vikali na serikali, wazazi, taasisi na wadau wote wa maendeleo.
Aidha mkuu huyo alisema jitihada zinazofanywa na taasisi hii zimefanikiwa kurejesha watoto zaidi ya 1500 shuleni baada ya wazazi wao kushindwa  ambapo kati yao 600 wamepewa mahitaji yote ya shule na wanaendelea na masomo na wengine wapatao 850 wamesajiliwa katika mpango maalumu wa  elimu baada ya muda wa masomo na michezo.
Akisoma taarifa fupi katika maadhimisho hayo  Mkurugenzi mtendaji wa Mradi wa PROSPER, Mary Kibogoya alisema  kuwa kwa kipindi cha mwaka 2012 kupitia mradi huo, watoto zaidi ya 2194 wavulana wakiwa 1164 na wasichana 1030 wameondolewa katika utumikishwaji huo uliokuwa ukifanywa na wazazi na walezi  ambao hawaoni faida ya kuwapeleka watoto wao shule na badala yake huwatumikisha katika mashamba ya tumbaku.
Alifafanua kuwa mradi wa PROSPER ambao unatekelezwa katika vijiji 20 unafadhiliwa na Umoja wa wadau wa zao la tumbaku Duniani ELCT na kutekelezwa na asasi tatu za Winrock International,TDFT na TAWLAE ambapo unalenga kuzuia na kuwatoa watoto 7,800 kwenye utumikishwaji katika mashamba ya tumbaku.
‘Hatari za kuacha watoto wazagae mitaani ni kubwa, na mradi huu umekuwa na juhudi nyingi za kuokoa maisha ya watoto hao katika wilaya za Sikonge na Urambo hapa mkoani Tabora , lakini nasikitika kwamba baadhi  ya wazazi waliowengi  bado hawajabadilika, naomba ieleweke wazi kwamba suala la kupeleka watoto shule ni la lazima na si ombi’, alisema.
Awali, wakisoma risala yao katika sherehe hiyo,  watoto wa shule za misingi waliiomba serikali, wazazi na taasisi zinginezo zisaidie kukomesha aina zote za utumikishwa wa watoto hapa nchini kwani wanapoteza haki yao ya msingi ya kupata elimu na hivyo kuzidi kutumikishwa au kubakia kuwa ombaomba mitaani.