MADEREVA
Madereva nchini wametakiwa kuwa wangalifu na
kufuata sheria za barabarani kikamilifu ili waweze kuokoa
maisha ya wasafiri na kupunguza ongezeko la ajali za barabarani hapa
nchini.
Wito huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya Kaliua mkoani
Tabora, Saveli Maketta, alipokuwa akikabidhi vyeti kwa madereva wa magari na
pikipiki waliopatiwa na mafunzo na chuo cha udereva cha Dodoma, ambacho
kinatambuliwa na serikali.
Alisema iwapo kama madereva watafuata sheria na
taratibu za usalama barabarani hakuna shaka kwamba ajali zinazoikabili taifa
hivi sasa zitapungua na hivyo kusaidia kuokoa maisha ya watu wanaokuwa
safarini.
Alisema udereva usiozingatia nidhamu na sheria umekuwa
chanzo kikubwa cha ajali za barabarani hapa nchini ambapo alitumia nafasi hiyo
kuwaasa vijana walioingia katika fani hiyo kuwa makini na kuepukana na tabia ya
kuleta mzaha wawapo barabarani.
Mkuu huyo wa wilaya ya Kaliua, alikabidhi vyeti vya
udereva kwa vijana 154 katika wilaya hiyo, ambao walifundishwa na
mkufunzi wa udereva anayetambuliwa na chuo cha usafirishaji cha Taifa
(NIT) Marijani Majani.
Mwenyekiti wa chama cha madereva nchini (TDA) mkoa wa
Tabora, Ali Kitenge, aliishukuru serikali kutokana na kuweka program za mafunzo
kwa madereva hali ambayo alisema itasaidia uwepo wa umakini kwa madereva wenye
sifa zinazotakiwa kuendesha magari na hivyo kupunguza ajali za barabarani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment