Saturday, August 25, 2012

MWENYEKITI CCM UYUI AKANUSHA KUTUMIA FEDHA ZA MABALOZI


Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM anayemaliza muda wake wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Abdalah Kazwika amekanusha vikali kuhusika na ubadhilifu wa fedha za mabalozi kama inavyoenezwa na baadhi ya wagombea wenzake.

Hivi karibuni kumekuwepo na uvumi kwamba Mwenyekiti huyo alitafuna fedha ya mabalozi kila mmoja shilingi 5,000 ambavyo hulipwa kila mwezi kama posho ya kujikimu.

Kazwika alitoa kauli hiyo katika ofisi ya chama hicho wilaya ya Uyui,  muda mfupi mara baada ya  kurejesha fomu ya kuomba kutetea wadhifa wake tena kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.


Alisema kuwa kumekuwepo na maneno mengi na hasa kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi ndani ya chama, kwamba anahusika upotevu wa shilingi milioni 12 ambazo zilitolewa na CCM makao makuu kwa ajili ya kuwalipa viongozi wa CCM kata, matawi na mabalozi.

“Nashangaa sana kuhusishwa na hizo pesa mimi sio mtendaji na pesa hizo zilikuja kwa katibu wangu, anapo simama mtu na kunituhumu mimi eti nimekula hizo pesa ananione.

“Hapo niwe mkweli hizo pesa nilizisikia na pia zilisomwa katika kikao cha kamati ya Siasa lakini mimi mwenyewe kuziona sijaziona hata kidogo, na kiutaratibu wa CCM mimi kama Mwenyekiti siruhusiwi kugawa pesa, mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Katibu na si vinginevyo” alisisiza Kawika.

Aidha alisema kuwa kila anapoenda katika ziara zake amekuwa akikumbana na maswali kama hayo na hasa la fedha za mabalozi.

Alieleza kwamba kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipita kwa wana-chama wa CCM sehemu mbalimbali na kumpaka matope kuwa yeye ndiye amechakachua fedha za mabalozi hao pamoja na viongozi ngazi ya kata na matawi, kitu ambacho ni uzushi utupu ambao unalenga kumchafulia jina ili asichaguliwe tena kushika wadhifa huo.

Kuhusu uhai wa chama, Kazwika alijinasibu kwamba wakati anashika madaraka yake kwa mara ya kwanza mwaka 2002 ya kuwa Mwenyekiti wa wilaya hiyo, alikuta kunawanachama 17000 elfu tu, lakini kwa sasa ameweza kukusanya jumla ya wanachama hai 38000 elfu.

Alibainisha kuwa iwapo atachaguliwa tena kukiongoza chama katika wilaya hiyo atahakikisha anaua makundi yote ndani ya chama na kuleta umoja, amani, upendo na mshikamano baina ya wana CCM.

Mwisho

1 comment: