NA Lucas Raphael,Tabora
WANANCHI wa jimbo
la Bukene, wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamependekeza kwamba, kwenye katiba
mpya ijayo, kuwe na kipengele kitakachotoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwa
mtu yoyote atakaye bainika na kosa la kumpa mimba mwanafunzi wa kike
ilikupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi huo hasa maeneo ya mijini na
vijijini.
Kauli hiyo waliitoa
kwa nyakati tofauti walipokuwa wakichangia mawazo yao kwenye mdahalo wa
wananchi juu ya mchakato wa kupata katiba mpya, ulifanyika katika ukumbi wa
Igembe Nsabo mjini Bukene.
Bahati Ramadhani
ambaye alikuwa ni mmoja wa washiriki wa mdahalo huo, alisema kuwa
kwenye katiba mpya, kuwe na kifungu kitakachompa adhabu ya kunyongwa Mwanaume
yoyote atakaye tiwa hatiani na mahakama kuwa amempa mamba mtoto wa kike
anaesoma shule aidha ya msingi au sekondari.
Alisema kwamba
licha ya sasa kuwepo na adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu
anayempa mimba mwanafunzi wa kike, lakini watu hao bado wanaendeleza tabia hiyo
na kufanya maisha ya watoto hao wa kike kuwa magumu baada ya kupewa mimba
sanjali na kutelekezwa na kubaki wanahangaika na watoto wao.
“Hiyo adhabu ya
jela miaka 30 kwa mtazamo wangu mimi, haitoshi, hapa suruhisho ni kunyongwa tu,
maana wakishanyongwa kama watu wawili kwa kosa hilo nadhani wataogopa” alisema
Bahati.
“Harafu sioni kama
itakuwa dhambi kwa watu hao kunyongwa maana nao ni wauaji pia, hivi karibuni
mtoto wangu wa kidato cha pili, kapewa mimba na baada ya kupewa huo ujauzito
yule bwana alikimbia na hadi sasa hajulikani mahali alipo, sasa kwa nini huyu
mtu asinyongwe? Alihoji Bahati.
“Niwaombe wananchi
wenzangu watakapo kuja kina Wariaoba na tume yao tuwe makini kutoa maoni yetu
bila woga” alisisitiza ,Bahati.
Nae Sospeter Kasiga
alisema kwamba, katiba mpya ni lazima impunguzie madaraka Rais wanchi ili asiwe
na mamlaka ya kuteuwa mawaziri, wakuu wa Wilaya na mikoa kwa kuwa kufanya hivyo
ni kuwanyima haki ya msingi wananchi ya kuchagua viongozi wanaowataka.
“Bunge ni
moja ya mihimili mitatu ya nchi, sasa unapomteua tena mbunge kuwa Waziri
maana yake nini,huyo tayari ni mhimili anayetokana na bunge harafu unamteua
kuwa mhimili tena katika baraza la mawaziri, hayo ni matumizi mabaya ya
madaraka ya Rais yanayotokana na ubovu wa katiba iliyopo sasa” alisema
Kasiga.
Alibainisha kuwa
katika katiba mpya ijayo iainishe kwamba wakuu wa mikoa na wilaya wachaguliwe
kwa kupigiwa kura na wananchi badala ya ilivyo sasa kuteuliwa na Rais na kwamba
mawaziri wasitokane na ubunge bali watume maombi ya kazi.
Mdahalo huo
uliandaliwa na umoja wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wilayani Nzega
(UWAZIKI) na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society kutoka jijini Dar
es salaam, ambapo mwezeshaji wa mdahalo , Christopher Nyamwanji, alisema kuwa
lengo la kuu ni kutoa uamsho kwa jamii ili siku ya kutoa maoni kuhusu katiba
mpya ijitokeze na kutoa maoni yao bila woga.
Mwisho..
No comments:
Post a Comment