Na Lucas Raphael,Mpanda

Mazingira.

Halmashauri ya wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imesema kuwa itaanza kuwashughulikia watu wote waliovamia misitu na kuishi katika maeneo ya hifadhi za wanyamapori na  mazingira kinyume cha sheria.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Naomi Nnko, amesema kuwa uamuzi huo unafuatia vitendo va uharibifu wa mazingira vinavyoendelea kushamiri katika wilaya hiyo na kuleta kero na athari katika mfumo wa ikolojia.



Akiongea na waandishi wa habari mjini Mpanda, Nnko, alisema kuwa ni wajibu wa halmashari hiyo kutumia sheria na taratibu zilizopo katika kukabiliana na wahamiaji hao ambao alisema wamekuwa wakishindwa kufuata sheria na taratibu zinazotakiwa kabla ya kuhamia katika vijiji vya wilaya hiyo.

Matokeo yake alisema kuwa kutokana na kushindwa kukidhi viwango vinavyotakiwa na taratibu hizo, wahamiaji hao wamekuwa wakivamia mapori na kwenda kuishi hivyo kujikuta wakiwa ndani ya maeneo ya hifadhi za misitu ama zile za wanyamapori.

Alisema kutokana na hali hiyo kiwango cha uharibifu wa misitu katika halmashauri hiyo kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka na hivyo athari zinazotokana na ukosefu wa misitu zimeanza kujitokeza.

Alisema wahamiaji hao wanaosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira katika wilya hiyo  wamekuwa wakitoka katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania kama Tabora, Shinyanga, Mwanza, Musoma, Simiyu na Geita ambapo alisema mara kadhaa wakuwa wakiendesha shughuli za kilimo katika maeneo ya hifadhi za misitu na wanyama.

Alisema halmashauri hiyo kwa kushirikiana na serikali kuu imejiandaa kukabiliana na wahamiaji hao haramu ambao alisema wamekuwa wakileta athari kubwa katika mkoa huo na hivyo kusababisha kero kwa viumbe na wanyama wanaoishi katika maeneo ya yaliyohifadhiwa.

Afisa maliasili wa wilaya ya Mpanda, Josephine Rupia Kapufi, alipoulizwa kuhusu athari zinazojitokeza katika hifadhi ya taifa ya Katavi ambapo wanyama aina ya viboko wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na ukame alisema hiyo inatokana taizo hilo la uhamiaji haramu.

Alisema kulingana na tafiti mbali mbali imebainika kuwa kuna watu wanaooendesha shughuli za kilimo katika maeneo yasiyotakiwa na hivyo kusababisha mtiririko wa maji kuingia katika mbuga hiyo kuzuiwa na hivyo kusababisha maji kukauka.

Alisema inasikitisha kuona hali kama hiyo ikijitokeza lakini kuna ushahidi unaoonyesha watu wakichepusha maji ya mito yanayoelekea katika hifadhi hiyo ambayo hutuama na kuwasaidia wanyama wakati wa kiangazi yakielekezwa katika mikondo tofauti.

Alisema kwa kiwango chetu tumekuwa tukijitahidi kupambana na tatizo hilo, lakini tunahitaji msaada kubwa wa kitaifa kwa sababu wavamizi hawa ni wengi na inahitajika fedha nyingi kwa ajili ya kuendesha zoezi la kutoa katika maeneo waliyoyavamia.

Wavamizi na wahamiaji haramu katika vijiji mbali mbali vya wilaya ya Mpanda wanakadiliwa kuharibu kiasi cha hekta 1990 katika misitu ya hifadhi ya Isanginya, Tongwe na Inyonga katika wilaya hiyo.

Mwisho