Wednesday, September 12, 2012


Na Mohammed Mhina, Zanzibar 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeainisha mpango wa matumizi ya fedha shilingi Bilioni 14.8 zilizotolewa kama msaada na Serikali ya China kwa SMZ.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake leo mjini Zanzibar, Waziri wa Fedha wa SMZ Mh. Omar Yusuf Mzee, amesema kuwa kipaumbele cha kwanza katika fedha hizo itakuwa ni kuboresha huduma za Afya, Elimu na miundombinu ya maji pamoja na uwekaji wa taa za sola kwenye baadhi ya barabara za mji wa Zanzibar.
Akizungumzia huduma za Afya, Waziori huyo wa fedha amesema kuwa sehemu ya fedha hizo zitasaidia upanuzi na ujenzi wa Hospitali ya Mkoani Kisiwani Pemba na kuifanya kuwa ya rufaa.
Waziri Mzee amesema taratibu zote za ujenzi wa Hospitali hiyo imekamilika na kwamba mara ujenzi huo utakapokamilika hakutakuwa na haja tena ya wagonjwa mahututi kul;etwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja kwa vile Hospitali hiyo itakuwa na kila aina ya vifaa na madawa ya tiba.
Amesema fedha hizo pia zitasaidia kuwasomesha wataalamu wa afya, Walimu wa masomo ya sayansi na kuboresha shule ya msingi ya Mwanakwerekwe kwa kuongeza ujenzi wa vyumba 12 vya madarasa.
Mh. Mzee amesema kuwa sambamba na hayo, fedha hizo pia zitasaidia kuweka taa za sola katika kwenye baadhi ya barabara za mji wa Zanzibar na kuboresha miundombinu ya maji mijini na Vijijini.
Amesema visima virefu na vifupi vitachimbwa ili kuongeza rasilimali ya maji katika maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba na kupunguza adha ya upatikanaji wa maji mijini na Vijijini.
Amesema fedha hizo zitasaidia kusomesha wataalamu wakiwemo Madaktari na Wataalam wa fani mbalimbali wakiwemo wa masuala ya kilimo na ufugaji.
Katika hatua nyingine Waziri Mzee pia amezungumzia suala la ununuzi wa Meli ya Serikali itakayokidhi huduma za usafirishaji wa abiiria na mizigo kati ya Kisiwa cha Unguja na Pemba.
Amesema Wizara yake inaendelea na mchakato wa ukusanyaji wa fedha shilingi Bilioni 17.6 kutoka katika vifungu 19  vya bajeti ya ndani kupitia kwenye wizara mbalimbali ili kununulia Meli ya Serikali itakayokidhi mahitaji ya usafiri wa abiria na mizigo kati ya Zanzibar na Pemba.
Amesema meli hiyo ambayo itagharimu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 12, itatengenezwa kwa muda wa miezi 18 na itasimamiwa na Kampuni ya Rowdies ya nchini Uingereza.
Amesema kuwa kinachofanyika sasa ni kuboresha michoro ya muundo wa meli hiyo ili ikidhi vigezo na viwango vya usafiri katika ukanda huu wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Waziri Mzee amesema wakati Serikali ikiendelea na mchakato huo, kuna juhudi zingine zinazochukuliwa na baadhi ya Makampuni ya usafiirishaji majini ikiwemo ya Azam Marine za kutaka kuingiza nchini meli nyingine kubwa ili kusaidia kupunguza adha ya usafiri wa abiria na mizigo kati ya Kisiwa cha Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment