Wednesday, September 12, 2012

WANAHABARI MKOA WA SINGIDA WAANDAMANA KUPIGA MAUAJI YA MWANGOSI


Na Elisante John,Singida

Septemba 12,2012.

WANAHABARI Mkoani Singida wameungana na wenzao nchini kwa maandamano ya kulaani na kupinga kitendo cha jeshi la polisi kuhusika na mauaji ya mwandishi wa kituo cha Channel Ten mkoani Iringa Daudi Mwangosi, wakati akiwa kazini.

Kupitia umoja wa klabu yao ya habari mkoa Singida(SINGPRESS),  maandamano hayo yakisindikizwa na askari polisi yalianzia eneo la Benki ya NBC na kuendelea barabara ya Kawawa hadi kituo cha mafuta Esso.

Baadaye yaliingia barabara ya Soko kuu, msikitini, Mghandi, Ipembe, Karume, Kinyeto na kumalizikia kwenye ofisi ya klabu, kabla ya kupokelewa na Mwenyekiti wa SINGPRESS, Seif Takaza.

Akizungumza na waandishi 19 wa mkoa Singida walioshiriki maandamano hayo, Takaza alisema kitendo cha polisi kuhusika na mauaji hayo kimedhalilisha chombo hicho, pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu, kulingana na mafunzo yao ya kijeshi.

“Mauaji ya mwangosi ni ya makusudi, hasa ikizingatiwa alikuwa chini ya mikono ya polisi, lakini mwisho wa siku akafia mikononi mwao….jambo hili lazima lipingwe kwa nguvu zote na watetesi wa haki za binadamu,”alisema.

Alisema mauaji hayo ni ya uonevu, kikatili na yanalifedhehesha taifa ambalo tangu lipate uhuru mwaka 1961 limejipatia sifa kubwa ya kudumu katika hali ya amani na utulivu kiasi cha kuitwa jina la kisiwa cha amani.

Aidha wanahabari hao wameomba kudumishwa kwa mahusiano ya jeshi la polisi na waandishi wa wa habari ili kuondoa uwezekano wa kutokea mauaji mengine kama hayo.

Hata hivyo wananchi wengi, waliyaunga mkono maandamano hayo na kuwakipunga mikono waandishi huku wakitamka neno la ‘Poleni’, kila ambako wanahabari walipita katika barabara mbalimbali za mjini Singida.



Askari wa usalama barabarani akiongoza maandamano ya wanahabari wa Singida walioandamana kupinga mauaji ya mwenzao
Baadhi ya waandishi wa habari mkoa Singida-SINGPRESS wakiwa ofisi za klabu wakimsikiliza Mwenyekiti waoo, Seif Takaza

 Maandamano yakiendelea katika barabara mbalimbali manispaa ya Singida

 Mwenyekiti wa SINGPRESS, Seif Takaza(katikati), mratibu wa klabu hiyo Evarista Lucas(kushoto) na Shabani Msangi


Wanahabari wa mkoa wa Singida wakiwa kwenye maandamano kwenye moja ya barabara za manispaa Singida kupinga mauaji ya mwandishi

No comments:

Post a Comment