Na mwaanshi wetu Sikinge
HALMASHAURI
ya wilaya ya Sikonge mkoani Tabora licha ya kuendelea kutekeleza
majukumu yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wake inakabiliwa na
changamoto nyingi katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku kwa
sababu ya upungufu wa watendaji katika idara mbalimbali za halmashauri
hiyo.
Akizungumza
na mwandishi wetu, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo
Bw. Paul Nkulila alibainisha kuwa athari zinazotokana na upungufu huu wa
watumishi ni utoaji wa huduma usioridhisha, pamoja na watumishi kukosa
ari ya kufanya kazi kwa kuwa mtumishi mmoja kwa wastani anafanya kazi ya
watu wawili hadi watatu jambo ambalo huchangia ucheleweshaji wa
shughuli nyingi za kimaendeleo ndani ya halmashauri hii.
Bw. Nkulila alisema kuwa idara zilizoathirika kwa upungufu wa watendaji kwa kiasi kikubwa ni idara ya Afya,
idara ya Elimu ya Msingi na Sekondari, Utawala, Kilimo, Mifugo na
Ushirika. Idara zingine zenye mapungufu kidogo ni Manunuzi, Ukaguzi wa
ndani, Ujenzi, Sheria na Maji.
Aidha
Bw. Nkulila alitaja sababu kuu za upungufu huu wa watumishi kuwa ni
mazingira yasioridhisha kufanyia kazi ambayo huwafanya watumishi wengi
kufika na kuhama baada ya muda mfupi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa
nyumba za kuishi watumishi wanaofanyia kazi vijijini mfano walimu na
watoa huduma za afya.
Akitoa takwimu za upungufu wa watumishi katika halmashauri hii Afisa Utumishi wa halmashauri hii Bi. Flora Malima alisema kuwa idara ya Afya ina upungufu wa watumishi 271 katika vituo mbalimbali vya Afya kati ya mahitaji ya watumishi 511, idara ya Elimu ya Msingi ina upungufu wa waalimu 270 kati ya 876 wanaohitajika wakati Elimu ya Sekondari inaupungufu wa waalimu 129 kati ya 270 wanaohitajika.
Aidha Bi. Malima aliongeza
kuwa idara ya Utawala katika kada zake zote kuanzia maofisa wa vijiji,
kata hadi wilaya ina upungufu wa watumishi 63 kati ya 150 wanaohitajika,
idara ya Maji ina upungufu wa watumishi 6 kati ya 20 wanaohitajika,
idara za Ushirika, Kilimo na Mifugo kwa pamoja zina
upungufu wa watumishi 53 kati ya 116 wanaohitajika wakati idara ya
Manunuzi ina upungufu wa watumishi 4 kati ya 6 wanaohitajika na idara
zilizobaki zina upungufu wa watumishi kati ya 1 na 2.
Bi.Malima
akifafanua mikakati ya kumaliza tatizo hilo , alisema kuwa mwaka jana
waliomba kibali cha kuajiri ila hawakupata, hivyo wamepanga kuomba tena
mwaka huu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya kujaza nafasi
za kada mbalimbali.
Aidha
Bi. Malima alitaja mkakati mwingine kuwa ni kuongeza nyumba za
watumishi ambapo kwa kuanzia tayari wamepata fedha kiasi cha sh. million
200 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 10 za watumishi wa afya kwa mwaka huu
wa fedha, lakini pia wanafikiria uwezekano wa kuwa na utaratibu wa
kuwalipia pango watumishi wanaopangiwa kituo cha kazi hapa wilayani
Sikonge.
No comments:
Post a Comment