Monday, August 13, 2012

UFISADI MANISPAA YA TABORA


Na Lucas Raphael ,Tabora
Ufisadi:
Baraza la madiwani la halmashauri ya manispaa ya Tabora, limekataa kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo baada ya taarifa hizo kuwa na kasoro na kuonyesha uwepo wa vitendo vya ubadhilifu na kifisadi.

Baraza hilo lililokutana katika kikao maalum kwa ajili ya kujadili  hoja maalum ya kupokea taarifa hizo za miradi ya maendeleo lilikuwa kali na mara kadhaa madiwani walimpa onyo na tahadhari mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwa makini na Wataalam wake.

Akitoa hoja kuhusu kasoro za taarifa hizo, Diwani wa Kata ya Mbugani, Idd  Kapama, alisema kwamba kumekuwa na  taarifa za mashaka kuhusu ujenzi wa barabara za manispaa ya Tabora ambapo kiwango cha fedha kilichotolewa ni kidogo ikilinganishwa na makisio.

Hata hivyo alisema kuwa katika taarifa moja inaoonyesha kuwa  ujenzi wa barabara hiyo umekamilika lakini utekelezwaji wake ni asilimia 30, huku vifusi vikiwa bado havijasambazwa lakini mkandarasi amelipwa malipo yote ya gharama za ujenzi ambazo shilingi milioni 150.

Kuhusu udhaifu wa halmashauri ya manispaa ya Tabora kutokuwa  imara katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato Diwani wa Kata ya Ndevelwa, Selemani  Maganga alisema kuwa  inasikitisha kuiona halmashauri kubwa kama hii ikiwa haina fedha.

Kisha akalalamikia kitendo cha Halmashauri ya Manispaa kuendelea kudaiwa na watumishi ama wazabuni na madeni husika kuongezeka na kufikia viwango vikubwa bila ya kuwepo kwa sababu za kueleweka hali ambayo imeifanya halmashauri kudhoofika.

 Mkurugenzi wa manispaa ya Tabora, Mariam  Makandawa, alisema kuwa hali ya kifedha katika halmashauri si nzuri na kwamba halmashauri imekuwa ikiweka mikakati itakayohakikisha kwamba wadai wa halmashauri hiyo wanalipwa ikiwa ni pamoja na kuongea nao ili kupata maridhiano.

Hata hivyo kikao hicho kilikataa kupokea taarifa zote zilizowasilishwa na kuamua kwa kauli moja kumuomba mkuu wa mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, aunde tume kwa ajili ya kuchunguza vitendo vya ubadhilifu na ufisadi vinavyofanywa na baadhi ya watumishi na wakuu wa idara katika halmashauri ya manispaa ya Tabora.

Hii ni mara ya kwanza kwa Baraza la madiwani la Halmashauri ya manispaa hiyo kutoa maamuzi ya kumtaka mkuu wa mkoa aunde tume kwa ajili ya kuchunguza ubadhilifu na vitendo vya kifisadi toka halmashauri hiyo ilipoanzishwa mwaka 1984.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment